Mabadiliko ya tabia-nchi ni tishio la usalama.

Katika siku za hivi karibuni,wito umetolewa wa kuwekwa kwa mikakati ya kukinga dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia-nchi.

Wanasiasa wakuu ulimwenguni sasa wanadai kuwa iwapo hatukutakuwepo na hatua za haraka za kuzuia athari zaidi,huenda dunia ikakumbwa na tishio la usalama.Mmoja wa hao ni waziri wa maswala ya nje ya Ujerumani ambaye amesema ulimwengu unahitaji kufikiria mikakati zaidi kuzuia mabadiliko ya tabia-nchi.

Aidha,Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pamoja na waziri Mkuu wa Uingereza,Boris Johnson wameungana na kusema kuwa dunia yafaa kulinda mazingira ili kuzuia ongezeko la joto duniani.

Ikumbukwe kuwa ulimwengu mzima umeshuhudia ongezeko la joto pamoja na kukauka kwa vidimbwi vya maji hivyo kuongeza migogoro kuhusu rasilimali chache zinazosalia.

Kumewepo na wito wa kupunguza matumizi ya gesi zinazochafua hewa na kuharibu utando wa ozoni.

Nchi kadhaa zimekuwa na ukosefu wa chakula kutokana na ukosefu wa maji ya kunyunyizia mimea shambani ili yakue.

Nimeyapeza mapenzi.

NIMEYAPEZA MAPENZI

1 Kumbatio la mwandani
Nilalapo mapajani
Niwe juu yeye chini
Nimeyapeza mapenzi

2 Kudeka anidekeze
Siri nizimueleze
Sauti ailegeze
Nimeyapeza mapenzi

3 Kwa ufundi anilishe
Bafuni aniogeshe
Chachandu azinogeshe
Nimeyapeza mapenzi

4 Anipikie vitamu
Nile nikiwa na hamu
Penzi ni jambo achumu
Nimeyapeza mapenzi

5 Na tushikane mikono
Anipe vilo vinono
Akitikisa kiuno
Nimeyapeza mapenzi

6 Aniite jina zuri
Penzi ja liwe johari
Aliridhie Qahari
Nimeyapeza mapenzi

7 Melipeza penzi hili
Niwe na yangu asali
Tuwe kama silisili
Nimeyapeza mapenzi

8 Ni wapi nitalipata
Liwe kama la Anita
Kila siku iwe chata
Nimeyapeza mapenzi

(Malenga ni Abuuadillah )

Nilipofikia.

NILIPOFIKIA
Jamani salamu, nawasalimia
Tena kwa nidhamu, zitawafikia
Kisha ninudhumu, nilodhamiria
Bora kunywa sumu, nilipofikia

Maneno matamu, kwangu yanishia
Leo nafahamu, ni chungu dunia
Rafiki makamu, wamenikimbia
Bora kunywa sumu, nilipofikia

Mja sina hamu, nawasimulia
Wangu ukarimu, umenivundia
Wapenzi wa damu, wamenitungia
Bora kunywa sumu, nilipofikia

Kama ni karamu, wanganiambia
Mbuzi wanywe damu, wema kulipia
Watie na ndimu, na limau pia
Bora ninywe sumu, nilipofikia

Wengi maharimu, walonichimbia
Nikalifahamu, walokadhiria
Kashika hatamu, na kunifukia
Bora kunywa sumu, nilipofikia

Hakika hadimu, siachwi huria
Nateswa kwa zamu, mwili wanishia
Ningawa sanamu, kinywa kufungia
Bora kunywa sumu, nilipofikia

Natupa kalamu, mwana najilia
Namwomba karimu, nionyeshe njia
Japo kwa yaumu, nijehubiria
Maisha magumu, niloyapitia.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Mupashe wangu habiba.

MUPASHE WANGU HABIBA

Njoo hapa weye njiwa, harakisha nikutume,
Nikutume majaliwa, jambo liwapo liseme,
Weye meshateuliwa, pote pale na uvume,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Hii ya kwangu barua, ya wino ulokolea,
Mengi nimedadavua, kisha na kuelezea,
Bayana atang’amua, mahaba yanapotea,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Mombasa alihamia, Kilifi hayupo tena,
Ndiko anafundishia, muda hatujaonana,
Arafa kinitumia, eti nusu twaonana,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Mwambie na hali yangu, upweke umenizidi,
Unauma moyo wangu, anapokosa zaidi,
Kisha hali ya mawingu, umenizidi baridi,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Umwambie kila kitu, ongeza hata na chuku,
Umwambie sili kitu, namuwaza kila siku,
Mahaba mekuwa butu, hii hali naishuku,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Mtafute kwa makini, kwa weupe peke yake,
Jaribu pia shuleni, kwa walimu wenzake,
Weusini samahani, siyo tena rangi yake,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Habiba ‘kiipokea, narai sipinde shingo,
Jaribu kujitolea, wala siwe kwa maringo,
Wajua twajitolea, tupae kwenye ulingo,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Mwandani wako natua, nimekuwa namba wani,
Hini ya kwangu hatua, dhahiri upo moyoni,
Jaribu kujikwatua, wenye wivu watamani,
Vale’tino yawadia, mupashe wangu habiba,

Toney Francis Ondelo
“Chomsky Mswahili/ Malenga Mjalisiha”
Ndhiwa- Homabay

Malimwengu.

MALIMWENGU

Jamani jama wandani, moyoni ninaumia,
Naloa damu kwa ndani, lazma mle tagandia,
Hata huku wajihini, kunyanzi yanivamia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Najiita hayawani, kwa udhia wa dunia,
Masumbuko manyumbani, uzee unaingia,
Matusi ya hadharani, matumbo yanaumia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Hata ninapojaribu, mathalani kuridhia,
Hayupo wa kunitibu, kukichapo ninalia,
Majanga yananisibu, wapi n’takimbilia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Nimejaribu jirani, yote haya kumwambia,
Kumbe sivyo nivyodhani, jirani anazamia,
Ashaikula yamini, rohoye kujikatia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Hata nao marafiki, mijini wamehamia,
Wote walioashiki, siwezi kuwafikia,
Wengineo mafasiki, maisha wanojutia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Nilijaribu kusoma, kazi kuikimbilia,
Vitabuni nilizama, aushi kupigania,
Haya yanoniandama, sikujua tapitia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Rahimu mwenye huruma, jikaze hima Jalia,
Mpaji wa yalomema, nipe nije furahia,
Vicheko vije kukoma, nami nije shangilia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

(Malenga ni Francis Ondelo)

Penzi wangu ucjali.

Maisha hapa chuoni, ni magumu mno sana
Nafunga yangu machoni, ili kesho kuiona
Sembe sukuma mezani, kutia tukizi sana
Penzi wangu usijali nilikwacha nijikimu

Nguo moja nimekita, sio eti ninapenda
Hata nywele sijikata, juu juu zinapanda
Nyayo kwako nimekata, taniua nishakonda
Penzi wangu usijali, nilikwacha nijikimu

Kazi yake muhazili, sitaweka hata chapa
Kwa rehema za Jalali, hitatupwa kwebye pipa
Kwa hakika sina hali, ni maisha nanichapa
Penzi wangu usijali, nilikwacha nijikimu

Za kukwenda kwenye mesi, hata kumi mimi sina
Mkopaji kwenda mesi, limekuwa langu jina
Ninajuta hiyo kasi, likwendavyo hilo jina
Penzi wangu usijali, nilikwacha nijikimu

*Kevin* *Akong’o*
Akongokevin6@gmail.com

Yanga bingwa pinduzi.

***YANGA BINGWA MAPINDUZI***
**
*
Paka havuki bahari, kwenda kuifunga Yanga /
Katu hii siyo siri, kule Zenji wamelonga /
Icheki yao dosari, ni baada ya kipyenga /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Imedhihiri #sadfa, kisiwa cha Zanzibari /
Yanga kuipata sifa, ndani hii januari /
Simba kapata kifafa, kalambwa kombe shuburi /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Viza kwenda kisiwani, Paka koko wamekosa /
Wakashindwa ushindani, goli tukenda wanasa /
Wananchi burudani, Simba tumempapasa /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Ni kombe la Mapinduzi, siye tumeshalitwaa /
Mtani hawezi kazi, mcheki ameduwaa /
Amewamba bumbuwazi, muda ulimuhadaa /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Kombe latua Jangwani, tumemfunga mtani /
Pale uwanja Amani, tumewapa tamrini /
Mato yao yapo chini, waona hawaamini /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Yanga daima ni mbele, kurudi nyuma ni mwiko /
Tumewachoma mishale, ilowafanya mideko /
Msimbazi ni kelele, ngebe nazo hadaiko /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Aibu yao wenyewe, tumewagongea Zenji /
Wamebaki na kiwewe, tumewaachia chenji /
Hakuna sandakalawe, tumewapigia tanji /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Siyo pila biriani, sasa pila mashendea /
Na njaa haliiwini, bali mewaongezea /
Hawa Simba matopeni, kushindwa wamezoea /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Kaditama kipembuzi, #Khamicyzo ninakaa /
Weka wako uchambuzi, kufungwa Simba adaa /
Halikwepo pingamizi, sie kwetu si ajaa /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani

(Malenga ni Bin Omary)

Nampenda.

NAMPENDA😍😍😍

Nimezama mapenzini
Na sitamani kutoka
Nimempenda Fulani
Na yeye ameridhika
Hata mi mnipe nini
Mimi kwake nimefika
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Kumuacha abadani
Nathubutu kutamka
Nyonga mkalia ini
Huyu wangu muhibaka
Amenikaa moyoni
Katu hawezi kutoka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Amenijaa kichwani
Siachi kumkumbuka
Hata nikiwa ndotoni
Sautiye yasikika
Namuomba RAHMANI
Marengo kutimizika
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Nampa vitu laini
Meno yasije kun’goka
Biriani ya maini
Ale pindi akitaka
Nae kaniganda yani
Hawezi kuchoropoka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Anipenda si utani
hatamani kuchepuka
Mimi kwake ndie shani
Nanga’ra nanawirika
Pindi akinita hani
Naitika rabaika
Nampenda kweli kweli
Kumuacha abadani

Pole ya yule Fulani
Kwangu alieondoka
Hakwona yangu thamani
Ndio akachoropoka
Nimempata hayuni
Na Mimi ametosheka
Nampenda kweli kweli
Kumuacha abadani

Kuachana abadani
Labda mola akitaka
Nasi twamwomba manani
Upendo kuimarika
Sote tufike ndoani
Kwa uwezo wa rabbuka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Kalamu nashusha chini
Nimechoka kuandika
Anipende daimani
Katu nisije achika
Mahasidi wa pembeni
Waishie kuumbuka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

(MTUNZI: Bintrasool)

Hana Taraka.

HANA TARAKA.

Na tena mkitengana, hawara hana taraka,
Wala hatongozwi tena, hawara ukimtaka,
Tena mnapokutana, ya nyuma kuyakumbuka,
Hana taraka hawara, ukweli nimebaini..

Nilikuwa ninabisha, kukataa jambo hili,
Yanayo mengi maisha, mengine sio ya kweli,
Hili nimethibitisha, kwa macho yangu mawili,
Hana taraka hawara, ni kweli sio utani.

Usije kudanganyika, Aseme wameachana,
Mambo yatavurugika, siku watapokutana,
Yalio sahaulika, yote watakumbushana,
Hana taraka hawara, Chunguza utabaini..

Wasema umempata, na umfute machozi,
Alomliza hufwata, tena bila ya ajizi,
Akitakacho hupata, na kupeana mapenzi,
Hana taraka hawara, hilo weka akilini..

(Malenga ni Ibn Kimweri.

Jitokeze nikuone.

JITOKEZE NIKUONE

Yuko wapi nauliza, mwenye mapenzi ya dhati?
Kipusa wa kupendeza, mtego kwa ‘tanashati?
Asiyependa kuliza, na akipenda hasiti?
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.

Aliye na umbo nzuri, aibuaye hisia?
Mtamu kama sukari, ‘kimbusu najifia?
Nihisi mie ushwari, na akinikisi pia?
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.

Fundi wa kusasambua, tena bila kusumbua?
Na kiuno kunengua, tena bila kutegua?
Katu sitomzingua, ‘tampenda atambue,
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.

(MTUNZI:Kongowea)