Msamiati wa malipo.

 1. Masrufu-Pesa za kukidhi matumizi ya nyumbani au safarini.
 2. Karadha-Mkopo wa muda mfupi usio na riba.
 3. Kiinuamgongo/Bahashishi/Pensheni-Malipo anayopewa mwajiriwa mwishoni mwa kipindi chake cha ajira.
 4. Koto-Ada ya kumsajili mwanafunzi chuoni.
 5. Nauli-Pesa za kusafiria.
 6. Kiangazamacho/Kiokozi/Machorombozi-Pesa anayopewa mtu kama ya kuokota kitu na kumrudishia mwenyewe.
 7. Riba-Pesa za ziada anazopata mtu kama faida ya kuwekeza benkini/pesa za ziada anazopata mkopeshaji wa fedha.
 8. Ridhaa-Pesa anazolipwa mtu kwa sababu ya kuharibiwa sifa.
 9. Kiingilio-Ada anayotozwa mtu ili kuingia katika burudani kama vile michezo.
 10. Karisaji-Malipo anayopewa mtu kwa kufanya kazi ya ziada.
 11. Dhamana-Ada anayolipa mshtakiwa ili kuwachiliwa kwa muda kesi ya inapoendelea.
 12. Honoraria-Malipo anayopewa mtu kwa kufanya kazi ya kiweledi.
 13. Fungule-Malipo kwa mganga/daktari baada ya kukamilisha kazi ya yake za uganga.
 14. Pango-Malipo anayolipa mpangaji kwa mwenye jengo baada ya muda uliokubaliwa.
 15. Karo-Malipo anayotoa mwanafunzi ili kugharimia masomo yake.
 16. Kodi-Ada inayotozwa na serikali kwa pato la mshahara wa mtu/biashara.
 17. Marupurupu-Pesa za ziada anazopewa mfanyakazi kando na mshahara wake ili kugharimia mahitaji mengine kama vile nyumba na usafiri.

Msamiati wa watu na kazi zao.

Watu katika jamii wana taaluma au kazi mbalimbali wanapopata posho na riziki zao.

 1. Mhasibu-Huyu ni mtu anayeweka rekodi za matumizi ya pesa.
 2. Sogora-Huyu ni fundi wa kupiga ngoma.
 3. Ngariba-Huyu ni mtaalamu wa kupasha wavulana tohara.
 4. Mfawidhi-Huyu ni mtu aliyeteuliwa kuongoza shughuli katika kitengo au idara.
 5. Mfasiri/mkalimani/mtarujumani-Huyu ni mtu anayeeleza maelezo yaliyosemwa katika lugha moja hadi nyingine.
 6. Kuli-Huyu ni mtu anayefanya kazi ya kupakia na kupakua mizigo bandarini.
 7. Mwandisi-Huyu ni mtaalamu wa kuunda vifaa na kurekebisha vilivyoharibika.
 8. Mkutubi-Huyu ni mtu anayefanya kazi ya kuazima na kuhifadhi vitabu maktabani.
 9. Kocha-Ni mwalimu wa mchezo.K.m kandanda.
 10. Mpigaramli-Huyu ni anayebashiri kwa kupiga bao.
 11. Dalali-Mtu anayeuza bidhaa katika soko la mnada.
 12. Mzegazega-Mtu anayeuza maji kwa kutembeza.
 13. Mhadhiri-Huyu ni mwalimu wa chuo kikuu.
 14. Nokoa/mnyapara-Mtu anayesimamia watu wanaofanya kazi shambani.
 15. Hakimu-Mtu anayeamua kesi mahakamani.Pia huitwa jaji.
 16. Mnajimu-Mtu mwenye elimu ya nyota.
 17. Dobi-Mtu anayefua na kupiga pasi nguo za watu wengine kwa malipo.
 18. Chura-Mtu anayefagia na kuzoa taka chooni au barabarani.
 19. Tarishi/Katikiro-Mtu anayeajiriwa ofisini ili kutoa huduma ya kupeleka barua au ujumbe.
 20. Utingo/taniboi-Mtu anayekusanya nauli kwenye basi au matatu.
 21. Mkufunzi-Mwalimu wa chuo cha ualimu au diploma.
 22. Mwashi-Mtu ajengaye vyumba kwa kutumia mawe.
 23. Mhunzi-Mtu anayefua/kutengeneza vifaa vya madini kama vile vyuma.
 24. Msarifu-Mtu mwenye mamlaka ya kusimamia,kutunza na kuidhinisha matumizi ya fedha katika taasisi au asasi maalum.
 25. Rubani-Anayeendesha ndege.

Matumizi Ya Ki.

Kiambishi ‘Ki’ kinatumika kwa njia mbalimbali kama zifuatazo.

 1. Ki ya Masharti.K.m Ukisoma kwa bidii utafaulu maishani.
 2. Ki ya kuwakilisha Ngeli ya KI-VI.K.m Kikombe hiki ni safi sana.
 3. Ki ya udogo.K.m Kiguo hiki kimechafuka.
 4. Ki ya mfanano.K.m Mtoto yule amelala kifudifudi.
 5. Ki ya kuonyesha kitendo kinachofanyika kwa wakati mmoja.K.m Mama anakula akiona runinga.
 6. Ki ya kukanusha kauli ya kutendeka.K.m Yule mwanabondia hapigiki.

Umbo la shairi.

Umbo la shairi ni sura ya shairi.Tunapoangazia umbo la shairi tunajikita katika mishororo,vina,mizani,ubeti na kibwagizo.Unapoeleza umbo la shairi zingatia yafuatayo.

 • Idadi ya mishororo katika kila ubeti.Hii itakusaidia kutambua aina ya shairi.K.m Shairi lililo na mishororo tano kwa kawaida hufahamika kama Takhmisa.
 • Idadi ya mizani katika kila kipande na mshororo kwa ujumla.K.m Tarbia huwa na mizani nane katika kila kipande na mizani kumi na sita katika kila mshororo.
 • Idadi ya vipande.K.m Ukwapi,utao, mwandamizi na ukingo.Hii itakusaidia kutambua bahari ya shairi maalum.
 • Urari wa vina vya kati na mwisho.
 • Kibwagizo/kiitikio/mkarara iwapo mshororo wa mwisho umerudiwa au kiishio iwapo mshororo wa mwisho haujarudiwa.

Istilahi za ushairi.

Kuna misamiati mingi ambayo hutumika katika ushairi.

 1. Mazda-Hii ni kuongeza silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani.
 2. Inkisari-Hii ni kupunguza idadi ya silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani.
 3. Dhamira-Hii ni lengo au nia ya mtunzi wa shairi.
 4. Maudhui-Hii ni ujumbe unaojitokeza katika shairi.
 5. Utohozi-Hii ni kuswahilisha maneno.K.m Facebook-fesibuku.
 6. Tabdila-Hii ni kubadilisha silabi ya mwisho ya neno bila kuathiri idadi ya mizani.
 7. Ukiukaji wa sarufi/kuboronga lugha.K.m Anapika mama chakula badala ya mama anapika chakula.

Aina za mashairi.

Kuna aina mbalimbali za mashairi kwa kuzingatia kigezo cha mishororo.

 • Tathmina-Hili ni shairi lenye mshororo mmoja katika kila ubeti.
 • Tathnia-Hili ni shairi lenye mishororo miwili katika kila ubeti.
 • Tathlitha-Hili ni shairi lenye mishororo mitatu katika kila ubeti.
 • Tarbia-Hili shairi lenye mishororo minne katika kila ubeti.
 • Takhmisa-Hili ni shairi lenye mishororo tano katika kila ubeti.
 • Tasdisa-Hili ni shairi lenye mishororo sita katika kila ubeti.
 • Usaba-Hili ni shairi lenye mishororo saba katika kila ubeti.
 • Unane-Shairi lenye mishororo minane katika kila ubeti.
 • Utisa-Shairi lenye mishororo tisa katika kila ubeti.
 • Ukumi-Shairi lenye mishororo kumi katika kila ubeti.

Aina za bahari ya mashairi.

Kuna aina mbalimbali za mashairi kwa kuzingatia kigezo cha bahari.

 1. Sakarani-Hili ni shairi lenye bahari zaidi ya moja.
 2. Ukara-Hili ambalo vina vya kipande kimoja hubadilika kutoka ubeti moja hadi mwingine ilhali vina vyaupande mmoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
 3. Ukaraguni-Hili ni shairi ambalo vina vya kati na vile vya mwisho hubadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
 4. Kikwamba-Hili ni shairi ambalo neno au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa ili kutanguliza mshororo au ubeti unaofuata.
 5. Mtiririko-Hili ni shairi ambalo vina vya kati vya mwisho havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi ule wa mwisho.
 6. Mathnawi-Hili ni shairi ambalo lina vipande viwili yaani ukwapi na utao.
 7. Ukawafi-Hili ni shairi ambalo lina vipande vitatu yaani ukwapi,utao na mwandamizi.
 8. Ngojera-Hili ni shairi la majibizano kati ya watu wawili.
 9. Madhuma-Hili ni shairi ambalo kipande kimoja hutoa swali na kipande kingine hutoa jawabu.
 10. Sabilia-Hili ni shairi lisilokuwa na kibwagizo.
 11. Msuko-Hili ni shairi ambalo mshororo wake wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo ya awali.
 12. Pindu/Mkufu/Nyoka- Hili ni shairi ambalo neno la mwisho/Kifungu cha maneno cha mwisho katika kila ubeti hutumika kuanza ubeti ufuatao.
 13. Utenzi-Hili ni shairi ambalo ni ndefu na lina kipande kimoja katika kila ubeti.

Matumizi Ya Kiambishi Na.

Kiambishi ‘na’ hutumika kwa njia tofauti katika sentensi ili kuonyesha maana mbalimbali kama ifuatavyo:

 • Hutumika kuonyesha dhana ya wakati uliopo.K.m Mama anapika chakula.
 • Hutumika kama kiunganishi katika sentensi.K.m Neema na Fadhili wanacheza mpira.
 • Hutumika kuonyesha dhana ya umilikaji.K.m Juma ana kalamu nzuri.
 • Hutumika kuonyesha mtendaji wa kitendo.K.m Mpira huo ulipigwa na Mwadime.
 • Hutumika kuonyesha kauli ya kutendana na kutendeana.K.m Jana wanamasumbwi walipigana kwenye uwanja wa Tononoka/Wanafunzi walipigiana kelele.
 • Hutumika kuonyesha hali.K.m Yule mjane ana huzuni baada ya kifo cha mumewe.
 • Hutumika kufupisha nafsi.K.m Nao waliendelea kucheza densi.

Aina za vitenzi.

Kitenzi ni neno linalofafanua jinsi kitendo fulani kilivyofanyika.Pia hufahamika kama kiarifa.Kuna aina mbalimbali za vitenzi kama zifuatazo:Kitenzi Kikuu/Halisi.(T)Hiki ni kitenzi kinachosheheni ujumbe muhimu wa kiarifu cha sentensi.K.m Baba anafyeka.Majukumu ya vitenzi vikuu ni:

 • Kuonyesha hali ya tendo
 • Kuonyesha nafsi
 • Kueleza tendo lililofanywa na mtenda/mtendwa
 • Kuonyesha wakati tendo lilipofanyika
 • Kuonyesha kauli mbalimbali za tendo

Kitenzi Kisaidizi.(Ts)Hiki ni kinachotoa taarifa kuhusu uwezekano,hali au wakati wa jambo kutendeka.Jukumu kuu ni kupiga jeki kitenzi Kikuu kufikisha ujumbe.K.m Anapaswa kusoma, alikuwa anapika, alitaka kufyeka n.kVitenzi visaidizi lazima vitumike na vitenzi halisi kwa kuwa hubeba viambishi vya wakati.Kitenzi Kishirikishi.(t)Hiki ni kitenzi kinachounganisha vipashio vingine katika sentensi.Majukumu ya vitenzi vishirikishi ni kama yafuatayo:

 • Kuonyesha sifa fulani ya mtu
 • Kuonyesha umilikishi wa kitu chochote
 • Kuonyesha kazi au cheo anayofanya mtu
 • Kuonyesha mahali
 • Kuonyesha umoja wa vitu au watu
 • Kuonyesha msisitizo

Kuna aina mbili za vitenzi vishirikishi:Vitenzi vishirikishi vikamilifu.Hivi huchukua viambishi viwakilishi vya nafsi ,njeo na hali.Vitenzi vishirikishi vipungufu.Hivi havichukui viambishi viwakilishi vya nafsi,njeo na hali.

Aina Za Nomino Za Kiswahili.

Nomino ni jina la kitu chochote k.v mnyama, binadamu,mimea,wadudu,vitu visivyokuwa hai k.m mawe n.kKatika lugha ya Kiswahili kuna aina mbalimbali za nomino kama vile tutaziainisha kama ifuatavyo:Nomino ya Pekee/halisi/mahususi.Haya ni majina maalum ya mahali, wanadamu, kampuni, bidhaa, vitabu, gazeti n.kMfano ni kama vile Nairobi,Kisumu,Khadija,Adoyo, Standard Media n.kNomino Za Makundi/Jamii.Haya ni majina ya makundi ya vitu k.v wanyama,watu,mimea n.k.Aghalabu vitu hivi hutokea kwa mikusanyiko yaani vikundi.Mfano ni kama vile halaiki ya watu,chane la ndizi n.kNomino Za Dhahania.Haya ni majina ya vitu visivyoweza kuonekana katika upeo wa macho bali huweza kufikirika.Mifano ni kama vile wivu,uchungu, upendo n.kNomino Za Wingi.Haya ni majina ya vitu visivyoweza kuhesabika.Mifano ni kama vile sukari,maji,mafuta,maziwa n.kNomino Za Kawaida.Haya ni majina ya vitu vinavyoweza kutumika kwa niaba ya vitu mbalimbali k.m wanyama, wanadamu n.kMfano ni kama vile muuguzi,ndege,kuku,baba n.kNomino Za Vitenzi-jina.Haya ni majina yanayotokana na vitenzi yaani yameundwa kutoka kwa vitendo.Mfano ni kama vile kuimba,kulia,kuchezaNomino Mguso.Haya ni majina ya vitu vinavyoweza kushikika.Mfano ni kama vile ng’ombe,ngoma,kalamu n.k

Advertisements