Shairi la ukara.

ANGEKOSEKANA BABAKati ya walodunia, yupo ninamthamini,
Asilimia ya mia, yake yashinda tisini,
Yeye ninamsifia, ndiye wa kwangu mwandani,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.Vipo vingi achangia, hasazo za aushini,
Kokote na familia, yeye ndiye tumaini,
Wana humkumbilia, anaporudi nyumbani,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.Watoto humlilia, wanapotoka shuleni,
Karo wamuulizia, hata kikosa jamani,
Naye anawapatia, kwa mengi matumaini,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.Alituleta dunia, kwa jina lake Manani,
Akatulinda tangia, kwenye raha na huzuni,
Mabaya yakiingia, yeye huleta amani,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.Asingewepo sikia, tungekosa duniani,
Tukose kujivunia, tulosomea shuleni,
Baraka zake ndo njia, zimetupisha shidani,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.Kisha kati ya mamia, asalia kileleni,
Ndiye kichwa si mkia, nyumbani ni namba wani,
Hata kizeeka pia, simtusi asilani,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.Baba baba tawalia, si kinyonga abadani,
Alewapo vumilia, zihifadhi za utani,
Katu sijemvamia, aweza kukulaani,
Je kweli tungezaliwa, kama hangekuwa baba.(Toney Francis Ondelo “Chomsky Mswahili” Ndhiwa-Homabay)

Shairi la ukaraguni.

Tumekosa Nini?

Mungu muumba dunia, mimea na wanadamu,
Nimekuja nikilia, pasi kujali kaumu,
Wewe ndiwe waridhia, pita nasi hali ngumu,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Kamwe uwezo hatuna, tungeishika dunia,
Tuweze kutakasana, mawele sijeingia,
Na hongo tungepeana, hasa kwa korona pia,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Yarabi tumejifunga, kwa vyumba pasi kutoka,
Hata na hewa kupunga, mekuwa shida hakika,
Halafu kutangatanga, pia imezuilika,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Au wafundisha nini, tuweze kulifahamu,
Magoti tupige chini, kwa toba situhukumu,
Tughofire kwa yakini, kwa korona loharamu,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Woga umetukithiri, toka juu hadi chini,
Twajiogopa si siri, pasi hata walakini,
Fukara na matajiri, hawana matumaini,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Kama ni kukesha pia, nimefika wiki mbili,
Chochote hujanambia, nijue unatujali,
Wana nao wanalia, wachukizwa hii hali,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Tunusuru hili janga, lisije kutumaliza,
Upulike kwetu mwanga, ututoe kwenye giza,
Gizani tutajitenga, tunahitaji mwangaza,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Kaditama tukupeni, ng’ombe au gari kubwa,
Kafara tukufanyeni, tuweze kukombolewa,
Tulaze matumaini, tusiwe katu watumwa,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

(Toney Francis Ondelo
“Chomsky Mswahili”
Ndhiwa-Homabay)

Aina Za Ndege.

 1. Dudumizi/Shundi/Gude/Tipitipi-Huyu ni aina ya ndege asiyejenga kiota.
 2. Kanga-Huyu ni kuku wa porini aliye na madoadoa meupe.
 3. Kasuku-Ndege aliye na rangi nyingi za kupendeza na hodari wa kuiga.
 4. Kigotago-Ndege ambaye hupigapiga mti kwa mdomo ili kupata vidudu.
 5. Hondo-Ndege aliye katika jamii moja ya shundishundi aliye na maji ya kunde na hupaza sauti kwa kawaida yake.
 6. Chozi-Ndege mdogo aliye na rangi ya manjano.
 7. Chiriku-Ndege mdogo ambaye hupiga kelele nyingi sana.
 8. Keremkeremu-Ndege ambaye hupenda sana kula nyuki.
 9. Korongo-Ndege aliye na miguu mirefu na shingo ndefu.
 10. Kware-Ndege mdogo kuliko kuku aliye na miguu myekundu na na mwili hudhurungi.
 11. Mbuni-Huyu ni ndege anayekwenda kwa kasi na ambaye ni kubwa na hana uwezo wa kuruka.
 12. Mnandi-Ndege mkubwa mwenye shingo ndefu,miguu mifupi mithili ya bata, tumboni ana rangi nyeupe na hupenda kuishi majini kuwinda samaki.
 13. Minga-Ndege mwenye rangi kijani,miguu myekundu,hula nazi na hupatikana katika jamii ya tetere.
 14. Njiwa-Ndege ambaye hufugwa nyumbani na huwa katika jamii ya tetere.
 15. Sigi-Ni ndege mdogo aliye na manyoya meusi kichwani na rangi ya kijivu kifuani.
 16. Shakwe-Ndege wa pwani anayefafana na membe na anayependa kula samaki.
 17. Tetere-Ndege mdogo mwenye rangi ya kijivujivu,hufafana na njiwa.
 18. Yangeyange/Dandala-Ndege mweupe na ana kishungi.
 19. Tongo-Hili ni jina la jamii la ndege wadogo warukao katika makundi.
 20. Mumbi-Ndege mkubwa anayeaminika kuleta msiba kila mahali aendapo.
 21. Kirumbizi-Ndege mdogo mwenye mkia mrefu na ushungi, hupiga kelele alfajiri.
 22. Kunguru-Ndege mweusi ambaye mara nyingi huwa na doa jeupe shingoni.
 23. Kipanga-Ndege ambaye hula wanyama na ndege wadogowadogo.
 24. Batabukini-Huishi zaidi majini,ni sawa na bata.
 25. Bata-Ndege anayependa matope.Ni mkubwa wa kuku.

Aina Za Wadudu.

 1. Funza/Tekenya-Huyu ni mdudu anayefafana sana na kiroboto na ambaye hupenya ngozini na kutaga mayai.
 2. Nzige-Mdudu ambaye husafiri masafa marefu na ambaye huharibu mimea kwa wingi.
 3. Tandu-Mdudu mwenye miguu mingi na ambaye huuma na ana sumu.
 4. Nondo-Mdudu anayefanya na kipepeo na hupenda kuruka usiku.
 5. Mbu-Mdudu ambaye hufyonza damu na kuuma watu na ambaye huhusika katika uambukizaji wa ugonjwa wa malaria.
 6. Mbungo-Mdudu mkubwa kuliko nzi, hufyonza damu na huhusika katika uambukizaji wa maradhi ya malale.
 7. Kiroboto-Mdudu ambaye huishi mwilini mwa mbwa,paka na hata wanyama wengine.
 8. Nyenze-Mdudu ambaye hutoa sauti kali usiku na hufanana sana na panzi.
 9. Kupe-Mdudu ambaye huganda mwilini mwa wanyama na kufyonza damu yao.
 10. Nyigu-Mdudu mwenye kiuno chembamba, huuma na aliye katika jamii ya ya nzi na nyuki.
 11. Kipepeo-Mdudu mwenye mbawa za kupendeza na aliye kama nondo ila ni mkubwa.
 12. Kumbikumbi-Mdudu ambaye huonekana katika makundi hasa nyakati za mvua.
 13. Kerengende-Ndege mkubwa mwenye jamii ya nzi.
 14. Jongoo-Mdudu mwenye miguu mingi myekundu na mwili mweusi.
 15. Chungu-Mdudu mweusi, mwenye jamii ya mchwa.
 16. Chawa-Mdudu ambaye hupenda kuishi kwenye nywele chafu na kunyonya damu.

Vipengele Vya Fani Katika Fasihi.

Mambo muhimu tunayohitaji kuzingatia tukiangazia fani ni kama yafuatayo.

 • Mtindo-Huu ni utaratibu maalum ambao mtunzi wa kazi wa fasihi amefuata kujenga kazi yake.Hutofautiana katika hali ya mtunzi na mtunzi.
 • Wahusika-Huweza kujumuisha watu, wanyama na viumbe vingine hai na hata mizimwi.Huwakilisha tabia maalum katika jamii.
 • Mazingira/Mandhari-Hapa ndipo mahali ambapo matukio yote ya fasihi hutendeka.Huweza kuwa mazingira halisi au ya kubuni.
 • Matumizi ya lugha-Ni mpangilio wa maneno, tamathali za semi kwa ufundi kulingana na mahitaji ya kazi yao.
 • Muundo-Hii ni sura nzima ya kazi ya fasihi.

Aina za Viambishi.

Kuna aina mbalimbali ya viambishi kama ifuatavyo.

 1. Viambishi awali-Hivi ni viambishi vinayopachikwa/kuambatanishwa kabla ya mzizi wa kitenzi.K.m a-na-pik-a.a-na ni viambishi awali.
 2. Viambishi tamati-Hivi ni viambishi vinayopachikwa/kuambatanishwa baada ya mzizi wa vitenzi.K.m a-na-kul-a.a ni kiambishi tamati.

Dhima ya viambishi.Viambishi Awali.

 • Huonyesha nafsi, wakati na idadi.K.m a-na-chek-a.Hapa tunapata nafasi ya tatu, umoja, wakati uliopo,hali ya kuendelea.
 • Huonyesha uyakinishi/ukanushi.K.m a-naongea katika hali ya uyakinishi na ha-taongea katika hali ya ukanushi.

Viambishi Tamati

 • Hukamilisha maana ya neno.K.m a-na-kimbi haina maana bila kiambishi tamati a.
 • Huzalisha maneno mapya.K.m anapiga,anapigana

Fani za Lugha Katika Fasihi.

Ni ufundi wa uteuzi wa maneno katika kupamba lugha inayovutia hisia mseto kwa msomaji/hadhira.

Aina ya fani za lugha zinazotumika katika fasihi ni kama zifuatazo.

 1. Utohozi-Hii ni mbinu ya uswahilishaji wa maneno yasiyo ya Kiswahili kuwa ya Kiswahili.K.m Bicycle-Baisikeli
 2. Kuchanganya ndimi-Hii ni mbinu ya kutumia maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili.Nitaenda supermaket kesho asubuhi.
 3. Maswali ya Balagha-Hii ni mbinu ya kuuliza maswali yasiyo na majibu ili kusisitiza jambo.
 4. Methali-Hii ni mbinu ya kutumia misemo ya hekima yenye maana fiche.K.m Bura yangu sibadili na rehani.
 5. Taswira-Hii ni mbinu ya kutumia maneno yanayoleta picha fulani kwenye akili ya msomaji ili kufafanua maswala fulani.
 6. Takriri-Hii ni mbinu ya kurudiarudia maneno au fungu la maneno ili kusisitiza jambo.K.m Yule kijana anachekacheka ovyo.
 7. Majazi-Hii ni mbinu ya hali inayotokea katika kazi ya fasihi ambapo tabia za wahusika zinaambatana na hali yao halisi.
 8. Lakabu-Hii ni mbinu ya mhusika wa kazi ya fasihi kupewa jina linaloendana na sifa zake.
 9. Tashbihi-Hii ni mbinu ya kutumia maneno ya kulinganisha ili kutoa mfanano fulani wa vitu viwili au hali mbili tofauti.K.m Baba hunguruma kama simba.
 10. Tanakuzi-Hii ni mbinu ya kuambatanisha maneno yanayokinzana au yanayoonyesha kinyume katika kazi ya fasihi.
 11. Tashihisi-Hii ni mbinu ya kupatia vitu visivyokuwa na uhai uwezo wa kufanya vitu kama binadamu.K.m Nyumba ililia na kupiga magoti.
 12. Chuku-Hii ni mbinu ya kutumia maneno ambayo hutia chumvi katika jambo na kuonekana kupita mipaka ili kumiminia sifa kitu au mtu.
 13. Tanakali za sauti-Hii ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au milio ya vitu mbalimbali.K.m Alianguka chini pu!
 14. Istiara-Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili au hali mbili tofauti pasina kutumia maneno ya kulinganisha.K.m Baba ni simba.
 15. Taashira-Hii ni mbinu ya kutumia maneno ya ishara ili kuonyesha hali fulani.

Fani za Uandishi/Kisanaa.

Hizi ni mbinu za Kiufundi zitumikazo na mwandishi/msimulizi wa kazi yoyote ya fasihi ambayo humlazimisha msomaji/hadhira kuisoma hadithi nzima ili kuzitambua.
Baadhi yazo ni kama vile:

 • Sadfa-Hii ni hali ambapo matukio hutendeka kwa pamoja bila ya kupangwa.
 • Kisengerenyuma-Hapa mwandishi hurejelea matukio yaliyofanyika nyuma.Hivyo humlazimu kubadilika wakati kuyasimulia tena.
 • Kisengerembele-Hapa mwandishi husimulia mambo yatakayotokea siku za halafu kwa kubadilisha wakati wa masimulizi.
 • Njozi-Hapa mwandishi hutumia ndoto kujaribu kufichua yaliyotendeka/yatakayotokea katika masimulizi/hadithi yake.
 • Upeo wa juu-Hapa mambo hufanyika kulingana na matakwa ya hadhira.
 • Upeo wa chini-Hapa mambo hufanyika kinyume na matarajio ya hadhira.Mara nyingi hutokea baada ya upeo wa juu.
 • Kinaya-Hii ni hali ambapo mambo hufanyika kinyume na matarajio katika hadithi.
 • Kejeli-Hapa kuna matumizi ya maneno ya dharau kwa madhumuni ya kukashifu kitendo fulani/mtu fulani katika hadithi.
 • Taharuki-Hii ni hali matukio ya hadhira/masimulizi humwacha msomaji/hadhira kinywa wazi na kumpatia hamu ya kutaka kusoma zaidi.Aghalabu hujitokeza paruwanja mwishoni mwa hadithi.
 • NGELI YA KI-VI.

  Hii ngeli husheheni maneno mengi ya lugha ya Kiswahili.Baadhi yazo ni yale yaliyowekwa katika udogo kwa kupachikwa kiambishi Ki mwanzoni mwa kila neno.Mifano ni kama Kiguo,kijishamba,kijitu,kijipanya n.k
  Mifano ya maneno mengine yanayopatikana katika ngeli hii ni kama vile kiatu,kikombe, kinyonyi, kibarua, kivumishi, kitengo n.k

  Muundo wa ngeli ya A-WA

 • Kwa kuna maneno yanayoanza na kiambishi‘Ki’ na kutamatika na kiambishi ‘Vi’.K.m Kifusi-Vifusi
 • Kuna maneno yanayoanza na kiambishi ‘Ch’ na kutamatika na kiambishi ‘Vy’.K.m Chakula-vyakula.
 • Aina za vihusishi.

  Vihusishi ni aina ya maneno yanayoonyesha uhusiano baina/kati ya neno moja na jingine.Kuna aina mbalimbali za vihusishi kulingana na utendakazi wao.Dhima za vihusishi ni kama zifuatazo.

  • Hutumika kuonyesha uhusiano kiwakati.K.m Wanafunzi walienda darasani baada ya kusikiliza hotuba ya mwalimu mkuu.
  • Hutumika kuonyesha uhusiano wa mahali.K.m Walitembea kando ya barabara.
  • Hutumika kuonyesha uhusiano wa umilikaji.K.m Wageni waliokuja kwangu wameondoka.
  • Hutumika uhusiano wa sababu.K.m Polisi walimkamata kwa ajili ya wizi.
  • Hutumika kuonyesha uhusiano wa kulinganisha.K.m Yeye alipata alama ishirini zaidi ya mimi.

  Kutokana na dhima za vihusishi tunapata aina zifuatazo za vihusishi.

  1. Vihusishi vya sababu
  2. Vihusishi vimilikishi
  3. Vihusishi vya kulinganisha
  4. Vihusishi vya kifaa/chombo/ala
  5. Vihusishi vya namna
  6. Vihusishi vya mahali
  7. Kihusishi ‘na’ cha mtenda