Matawi Ya Isimu.

Isimu-ubongo– ni tawi la isimu linalochunguza mahusiano kati ya lugha na
michakato ya kiakili (ubongo), uzalishaji wa matamshi katika ujifunzaji wa lugha.
Msingi mkubwa katika tawi hili la isimu ni kuwa mchakato wa uzungumzaji
huanzia katika akili ya mtu. Hivyo mwanaisimu ubongo hujaribu kutafitina kueleza
ni nini hasa kinatokea katika ubongo ambacho kinamwezesha mwanadamu
kuzungumza. Pia hutafiti na kueleza matatizo katika lugha yanayotokana na
matatizo katika ubongo wa mwanadamu.
Isimujamii – Isimu Jamii (social linguistcs) – ni tawi la isimu (elimu ya lugha)
linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake.
Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali
za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii
inayoitumia. King’ei (2010), anaeleza kuwa, kwanza lugha ni zao la jamii, na ni
kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika. Pili, lugha hutumiwa na
jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha
kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo isimu jamii hueleza na kufafanua
mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha.
Isimu -anthropolojia– tawi hili la isimu hukijita katika kutafiti na kueleza historia
ya na miundo ya lugha ambazo bado hazijaandikwa.
Isimu- kompyuta – huchunguza matumizi ya kompyuta katika kuchakata na
kuzalisha lugha ya mwanadamu. Ni tawi ambalo kwa hakika si la muda mrefu na
linatokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia hasa baada ya uvumbuzi wa
kifaa kama kompyuta.Isimu-tumizi– huchambua na kueleza matumizi ya nadharia mbali mbali za lugha na maelezo ya kufundishia lugha.(Mr.Simile.O. Utangulizi wa lugha na isimu,Mzumbe University,2012/2013)

Matawi Ya Isimu.

Isimu-ubongo– ni tawi la isimu linalochunguza mahusiano kati ya lugha na
michakato ya kiakili (ubongo), uzalishaji wa matamshi katika ujifunzaji wa lugha.
Msingi mkubwa katika tawi hili la isimu ni kuwa mchakato wa uzungumzaji
huanzia katika akili ya mtu. Hivyo mwanaisimu ubongo hujaribu kutafitina kueleza
ni nini hasa kinatokea katika ubongo ambacho kinamwezesha mwanadamu
kuzungumza. Pia hutafiti na kueleza matatizo katika lugha yanayotokana na
matatizo katika ubongo wa mwanadamu.
Isimujamii – Isimu Jamii (social linguistcs) – ni tawi la isimu (elimu ya lugha)
linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake.
Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali
za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii
inayoitumia. King’ei (2010), anaeleza kuwa, kwanza lugha ni zao la jamii, na ni
kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika. Pili, lugha hutumiwa na
jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha
kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo isimu jamii hueleza na kufafanua
mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha.
Isimu -anthropolojia– tawi hili la isimu hukijita katika kutafiti na kueleza historia
ya na miundo ya lugha ambazo bado hazijaandikwa.
Isimu- kompyuta – huchunguza matumizi ya kompyuta katika kuchakata na
kuzalisha lugha ya mwanadamu. Ni tawi ambalo kwa hakika si la muda mrefu na
linatokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia hasa baada ya uvumbuzi wa
kifaa kama kompyuta.

Isimu-tumizi– huchambua na kueleza matumizi ya nadharia mbali mbali za lugha na maelezo ya kufundishia lugha.

(Mr.Simile.O. Utangulizi wa lugha na isimu,Mzumbe University,2012/2013)

Dhana Ya Fonolojia.

Fonolojia ni nini?
Kwa mujibu wa Mugulu (1999) akimrejelea Fudge (1973) anasema kwamba fonolojia ni kiwango
kimojawapo cha lugha fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha.
Vipashio vya kifonolojiani fonimu na alofoni zake.
Dosari ya fasili hii ni kwamba haijafafanua kiwango kipi cha lugha ambacho kinahusika na fonolojia kwani lugha
inaviwango mbalimbali.
Massamba (2010) anasema kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na mfumo wa sauti (asilia) za lugha.
Hii inamaana kwamba, kila lugha mahususi inamfumo wake wa sauti ambamo maneno hujengwa. Ki ukweli
fonolojia hujihusisha na namna sauti zinavyotumika katika maneno ya lugha mahususi katika kuleta maana.
Massamba na wenzake (2004) wanafafanua kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha na uchunguzi,
uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za
binadamu.
Massamba (2010), pamoja naMassamba na wenzake (2004), wanaonekana kufanana katika fasili zao juu ya
fonolojia isipokuwa, Massamba na wenzake (2004), wameonesha kuwa fonolojia si tawi linalojihusisha na mfumo
wa sauti tu, bali huzichunguza, huzichambua pamoja na kuziainisha sauti hizo.
TUKI (1990) wanasema kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti
zinazotumiwa katika lugha fulani.
Vilevile dosari ya fasili hii ni kwamba, imeegemea upande mmoja tu yaani uchambuzi wa mfumo wa sauti za lugha
fulani na kusahau kuwa taaluma hii ya fonolojia haijikiti tu katika uchambuzi bali huzingatia uchambuzi, uchunguzi
pamoja na uainishaji wa sauti hizo kama asemavyo Massamba na wenzake (2004). “fonolojia ni tawi la isimu
ambalo hujishughusha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika
mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.”Akmajian na wenzake (2001), nao wanadokeza msimamo kama wa massamba wanapodai
kwamba fonolojia inaweza kuchunguzwa kwa mitazamo miwili tofauti. kwanza, fonolojia kama
tawi dogo la isimu linalochunguza mfumo na ruwaza za sauti za lugh mahususi ya binadamu; pili
fonolojia kama sehemu ya nadharia ya jumla ya lugha ya binadamu inayohusika na tabia za jumla
za mfumo wa sauti za lugha asili za binadamu. Katika mhadhara huu, hata hivyo tutakuwa
wafuasi wa mtazamo unaoona kuwa fonolojia ni tawi la isimu linaloshughulikia mfumo wa sauti
za lugha mahususi, hivyo tuna kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza,
fonolojia ya Kiha, fonolojia ya Kihehe, na fonolojia ya Kibena. Kipashio cha msingi cha
fonolojia ni fonimu.(Makala haya yaliandaliwa na ANTIDIUS JOVINARY NSIGA)

Dhana Ya Fonimu.

Fonimu
Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi,
fonimu ina maana, kwa kuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi katika
neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo
wa sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache ikilinganishwa na foni. Idadi
ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu
ishirini na nane (28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na
tatu (33) na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza kubadilishwa
nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa alofoni.
Alofoni ni kishio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa na
kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano:
• Fedha na feza
• Sasa na thatha
• Heri na kheri
Kwa kifupi, alofoni ni matamshi tofautitofauti ya fonimu [sauti] moja.
Mitazamo juu ya Dhana ya Fonimu.
Juhudi za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo
mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo
hujulikana zaidi.
(i) Fonimu ni tukio la kisaikolojia
Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni
Noam Chomsky. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhana iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha.Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa
bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake Chomsky anayaita maarifa haya kuwa ni
umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa
miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha
(kutamka) fonimu hizo, yaani utendi (performance). Chomsky anabainisha kuwa kuna
uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali
ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo
vya matamshi (alasauti za lugha), athari za mazingira, ulevi na maradhi. Hivyo kutoka na hali hii,
fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia tu.
(ii) Fonetiki ni tukio la kifonetiki
Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel James. Ambaye anaiona fonimu kuwa
ni {umbo} halisi linalojibainisha kwa sifa zake bainifu. Anadai kuwa fonimu huwakilisha
umbo halisi la kifonetiki na inapotokea kukawa na fungu la sauti katika fonimu moja, sauti
hizo huwa na sifa muhimu za kifonetiki zinazofanana. Hivyo, fonimu ya Kiswahili ni kitita
cha sauti za msingi pamoja na alofoni zake.
(iii) Fonimu ni Fonolojia.
Huu ni mtazamo wa kidhanifu, ambapo huaminika kuwa fonimu ni kipashio cha kimfumo, yaani
fonimu huwa na maana pale tuinapokuwa katika mfumo mahususi. Mwanzilishi wa mtazamo huu
ni Nikolai Trubetzkoy. Yeye huamini kuwa fonimu ni dhana ya kiuamilifu na uamilifu huu
hujitokeza tu fonimu husika inapokuwa katika mfumo wa sauti wa lugha husika. Kwa mujibu wa
mtazamo huu, fonimu ni kipashio kinachobainisha maana ya neno. Mtazamo huu hutumia jozi
sahihi kudhihirisha dai lake. Mathalani, maneno baba na bata yana maana tofauti kwa sababu ya
tofauti ya fonimu /b/ na /t/. Mtazamo huu hujulikana kuwa ni wa kifonolojia. Na kwa hakika,
mawazo haya ndiyo yaliyoshika mzizi zaidi katika taaluma ya fonolojia na ndiyo inayofunzwa
hivi sasa katika sehemu nyingi ulimwenguni.(Makala haya yaliandaliwa na ANTIDIUS JOVINARY NSIGA)

Sajili Ya Simu.

Hii ni lugha inayotumiwa katika mazungumzo ya simu.
Sifa za lugha ya simu
Mazungumzo ya simu ni mafupi, hutumia sentensi fupi zenye muundo rahisi.
Hoja hutajwa moja kwa moja bila maneno mengi kwani ili kudhibiti gharama ya simu
Huwa na kukatizana kwa maneno kati ya wazugumzaji.
Huwa ni mazungumzo baina ya watu wawili pekee; anayepiga na anayepokea.
Hutumia istilahi maalum za lugha ya simu kama neno ‘hello’
Huchanganya ndimi (kutumia maneno yasiyo ya lugha nyinginezo) ili kuwasilisha ujumbe kwa upesi.
Ni lugha ya kujibizana.

Isimujamii.

Isimujamii– ni tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.

Istilahi za isimujamii
Isimu – ni mtalaa ambao huchunguza, huchanganua na pia kuchambua na kufafanua lugha kama mfumo wa mawasiliano baina ya wanadamu.
Lugha – ni chombo cha mawasiliano baina ya watu. Lugha huzingatia mpangilio maalum wa sauti, maneno na sentensi.
Sajili – ni mukhtadha/rejista mbalimbali au mitindo maalum ya lugha katika mazingira/hali mbalimbali.
Mifano ya sajili ni kama vile lugha ya hospitalini, shuleni, sajili ya dini, biashara, kisiasa, michezo,
Fonolojia – ni tawi la sayansi ya isimu linaloshughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti. Fonolojia hutumika kuunda alfabeti katika lugha fulani. Aghalabu kila lugha hutumia mfumo fulani wa sauti mahususi katika lugha hiyo pekee.
Fonetiki – huchunguza sauti zinazotamkwa na binadamu bila kuzingatia lugha yoyote.
Mofolojia – (au sarufi maumbo) ni tawi la isimu linalochunguza maneno ya lugha fulani, aina za maneno katika lugha, hasa upangaji wa mofimu mbalimbali zitumikazo kwa ajili ya kuunda maneno hayo. Kwa mfano, lugha ya Kiswahili hutumia mbinu kadhaa kuunda maneno kulingana na mpangilio wa mofimu. Kwa mfano, neno ‘lima’ linaweza kutumika kuunda maneno mengine katika Kiswahili k.m mkulima, kilimo, nimelima, limika n.k Katika kubadilisha mofimu hizi, tunaweza kubadilisha neno moja kutoka aina moja(kitenzi) hadi nyingine (nomino) n.k
Sintaksia– (au sarufi miundo) ni tawi la isimu au taaluma ya sarufi inayoshughulikia jinsi vikundi vya maneno na sentensi mbalimbali zinajengwa katika lugha. Sintaksia huangazia kanuni au sheria za lugha. Kila lugha huwa na sheria zake za kuambatanisha maneno kama vile jinsi ya kufuatanisha vitenzi, nomino na vielezi. Kwa mfano: Mtoto yako shiba ni sentensi isiyokuwa na sintaksi. Sentensi sawa ingekuwa: Mtoto wako ameshiba.
Semantiki – ni tawi la isimu linalochunguza maana halisia (mantiki) ya maneno, kifungu au sentensi katika lugha. Sentensi isiyokuwa na mantiki ni sentensi inayotoa maana ambayo haiwezekani katika uhalisia. Sentensi inaweza kuwa sawa kisintaksia lakini iwe na makosa ya kimantiki. Kwa mfano: Kiatu cha mbwa kimefutwa kazi kwa sababu kumi ni kubwa kama hewa.

Aina za lugha katika isimujamii
Lafudhi– Ni upekee wa mtu katika matamshi (accent) unaoathiriwa na lugha ya mama, mazingira yake ya kijiografia au kiwango ujuzi wake wa lugha.
Lahaja – ni vijilugha vinavyoibuka kwa lugha moja kuu kutokana na tofauti za kijiografia baina ya wazungumzaji wa lugha hiyo.
Kwa mfano lugha ya Kiswahili ina lahaja kadhaa kama vile Kimtang’ata, Kilamu, Kimvita, n.k. Tofauti baina ya lufudhi ni kama msamiati, muundo wa sentensi au matamshi.
Lugha rasmi – ni lugha inayotumika katika shughuli za kiofisi ama ya wakati wa mawasiliano rasmi katika taifa fulani. Kwa mfano, lugha rasmi nchini Kenya ni Kiingereza.

Lugha rasimi – ni mtindo wa lugha uliotumiwa na mtu/watu fulani mashuhuri (zamani) na ambao huonekana kuwa mtindo bora wa lugha unaofaa kuigwa na wengine. Kwa mfano lugha ya Shakespeare.
Lugha ya taifa – ni lugha inayoteuliwa na taifa fulani kama chombo cha mawasiliano baina ya wananchi, kwa maana inazungumzwa na wananchi wengi katika taifa hilo. Lugha ya taifa, nchini Kenya ni Kiswahili; Uganda ni Kiganda.

Lugha sanifu – Ni lugha iliyokarabatiwa na sheria zake (k.v muundo wa sentensi, msamiati, sarufi, n.k) kubainishwa na kuandikwa, na kwa hivyo huzingatia sarufi maalum na upatanisho sahihi wa sentensi.
Kwa mfano: Kiswahili sanifu – ni lugha isiyokuwa na makosa ya kisarufi.
Lingua Franka – Ni lugha inayoteuliwa miongoni watu wenye asili tofauti wasiozungumza lugha moja ili iwe lugha ya
kuwaunganisha katika shughuli rasmi au za kibiashara.
Pijini– ni lugha inayozaliwa kutokana na mchanganyo wa lugha zaidi ya moja.
Kwa mfano. Sheng’ (lugha ya vijana mitaani nchini ni lugha iliyoibuka kutoka kwa Kiswahili na Kiingereza.
Krioli – Ni pijini iliyokomaa na kukubalika.
Lugha mame – hii ni lugha isiyokua na ambayo hubaki kati umbo lake la awali.
Kwa mfano lugha ya Kilatini haibadiliki na hivyo hutumika katika kubuni majina ya kisayansi, n.k.
Lugha azali – ni lugha inayozaa lugha nyinginezo.
Misimu – ni lugha yenye maneno ya kisiri ambayo hutumiwa na kikundi fulani cha watu katika jamii, inayoeleweka tu baina yao. Misimu huibuka na kutoweka baada ya muda.

Dhana ya Waswahili.

Katika kipindi ambacho kilipita, niliweza kufafanua mchango wa Kiswahili katika bara la Afrika. Katika maelezo hayo, niliweza kueleza Mswahili ni nani. Nitarejelea sehemu hiyo ya kumweleza Mswahili na Uswahili wake.Mwandishi wa _Periplus_ anasema kuwa Waswahili ni:-
a). *Wajuzi* *wa* *meli* : tabia inayojitokeza hapa ni kwamba, watu hawa wana tabia za kipwani na kibahari. Hapo awali, waliokuwa na ujuzi wa kutumia bahari walikuwa Waswahili pekee na walikuwa wanaitumia bahari kujikimu kimaisha. Kulipatikana makabila mengine lakini wengi walishughulika na mambo ya ukulima.
b). *Sura* *Jamali* ( _nzuri_ ): waliokuwa na sura zilizokuwa zafanana na Waarabu hawakuwa wengine isipokuwa Waswahili, na Waarabu walisifika na kuwa na sura nzuri za kuvutia, walipooana na Waswahili, sura hizo jsmali zikaingia kwa Waswahili.
c). *Uhusiano* *wa* *ndoa* : Waswahili ndio wenyeji pekee wa upwa wa Afrika Mashariki ambao walioana na Waarabu kabla ya kufika kwa dini ya ukristo katika sehemu za Afrika Mashariki, hakuna jamii nyingine ya Pwani ilikuwa na uhusiano wa ndoa na Waarabu kuliko Waswahili. Kwa hivyo, ni wazi kuwa mwandishi wa _Periplus_ alikuwa akiwazungumzia katika andiko lake Waswahili.*MAONI* *YA* *WANAHISTORIA* *KUHUSUBWASWAHILI*
a). *Waswahili* *ni* *chotara* : kuna wanaodai kuwa Waswahili walitokana na ndoa baina ya Wabantu na Waarabu. Hawa na wale Wabantu waliokuwa wakiishi kwenye Mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki. Wengine wakadai kuwa, Waswahili ni uzao wa Washirazi na Wabantu. Katika maoni yao, Kiswahili hakikuwepo tangu awali bali kilibuniwa wakati wa Waarabu, Washirazi na Wabantu wa Mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki walipoanza kuishi na kuoana. Hoja wanayoitoa ni kuwa, Kiswahili kina maneno ya Kuarabu na Kishirazi mengi sana.
b). *Wangozi* *ndio* *Waswahili* : katika nyakati za karibuni, maoni mbalimbali yametolewa kuhusu Waswahili ns Uswahili. Kuna waliodai kuwa Uswahili ulitokana na Wabantu na wageniwalioishi Mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki. Kati ya wenye maoni hayo ni Chiraghddin S, na Mnyampala. Maoni yao ni kuwa, Waswahili walikuweko tangu azali hata kabla ya Waarabu na Washirazi kufika Mwambao wa Pwani japo Waajemi walichangia kuwepo kwa msamiati wa Kiajemi hasa ya Kiarabu kwenye Kiswahili. Wanahistoria hawa wanaamini kwamba chimbuko la Waswahili liko kati ya Kismayu na mto Juba maeneo ya Somalia pahali pajulikanapo kama Shungwaya. Kuanzia wakati huo, Waswahili walisambaa kusini na kufanya maskani zao mahali mbalimbali, mfano Barawa, Lamu, Malindi, Mombasa, Kilwa, Mtwara, Kisiwa cha Unguja, Pemba na Ngazija pamoja na maeneo ya Komoro. Watu hawa wana lugha ya asilia iliyojulikana kama Kingozi. Lugha hii ilikuwa Kibantu cha asili yake. Kingozi ndiyo lugha iliyoweka msingi mlimojengwa lugha ya Kiswahili na mchanganyiko wa maneno mengi ya lugha za kigeni.
c). *Nadharia* *ya* *Jamadari* : Jamadari adai kuwa wageni wengi waliomiminika maeneo ya Mwambao, walijumuika na wenyeji wa Afrika Mashariki hata kabla ya kuzaliwa kwa Nabii Issa bin Maryam. Malengo ya Waarabu kufika maeneo ya Mwambao yalikuwa ya kibiashara. Bwana Jamadari adai kabila saba za Kiarabu:- Shaban, Sab-aan, Hamyar, Kahtwan, Kasman, Kaslaan na Min-aan kutoka Yemen. Kabila hizi ziliwahi kufika kupitia Uhabeshi, Somalia pahali walipokutana na Wangozi ambao walioana na kupatikana kabila lililojulikana kama Azzania. Waazzania walisambaa kuanzia Kismayu kuelekea sehemu za kusini. Mwarabu Ibn Batuta ndiye aliyewaita hawa Waazzania Waswahili.
d). *Maoni* *ya* *Profesor* *Ahmad* *Shekh* *Nabahani* : waandishi wengi waliandika juu ya Waswahili na Uswahili na wanamapisi ya mapokezi walioeleza kwamba kabila kuitwa Wangozi ni kuwa matumizi makubwa yao walikitumia ngozi. Walitumia ngozi katika mambo kama vile; kutekea maji(viriba vya maji), viriba vya kuvukutia moto kwa wahunzi au wafua vyuma, kitapa cha kuchotea maji, viatu, kanda, nyuo za panga, visu na hata kamba za kupimia ardhi n.k. Wangozi si kwamba walitumia ngozi kuwa walikuwa wawindajiau wafugaji ndipo wakaitwa Wangozi, bali walipewa jina la Wangozi kwa sababu ya kutumia ngozi pakubwa. Waswahili wanasema, ” Mti wenye matunda ndio upigwao kwa mawe.” Mijadala juu ya Waswahili ni ile kuwa Mswahili alijulikana kuwa ni Mngozi, kwao kuna mushkili kwamba jina hili linawaelekea watu wanaoishi msituni, wawindaji au wakulima kwa sababu ndio wenye kuwafuga wanyama, na Waswahili ni watu wa pwani au mwambao. Jina la Wangozi halistahili kuitwa watu hao waliotoa fikra au maoni hayo, pia hapa ushahadi Waswahili kutokuwa na jina hilo. Mwandishi lazima kabla hajaanza fikra zozote lazima afanye utafiti kwa wajuzi wale ambao ni wa kabila lile ambalo anataka kuandika habari zake.

Nafasi ya Kiswahili Barani Afrika.

*NAFASI* *YA* *KISWAHILI* *KATIKA* *BARA* *LA* *AFRIKA* !
Swali ambalo tunafaa kulijua tunapoangazia suala hili ni, je! Mswahili ni nani?, Kiswahili kilitoka wapi?.
Hilo ni suala la kiisimu ambalo pengine nitaligusia kidogo. Kuna maono mbalimbali kuhusu huyu anayeitwa mswahili. Mwandishi wa _periplus_ katika katika usemi wake anadai kuwa:
a). Waswahili ni wajuzi wa meli- yaani ni watu wenye tabia za kibahari na tamaduni za kipwani.
b). Wana sura jamali- yasemekana kuwa waliokuwa na sura zifananazo na Waarabu walikuwa waswahili.
c). Uhusiano wa ndoa- waliooana na Waarabu katika upwa wa pwani ndio waswahili.

Kwa mujibu wa _Wanahistoria_ , kulikuwa na maoni mbalimbali. Maoni hayo ni;
a). Waswahili ni chotara- ndoa kati ya Wabantu na Waarabu.
b). Wangozi ndio Waswahili- wanahistoria wanadai kuwa, Kiswahili kilikuwepo tangu jadi. Wanadai kuwachimbuko la Kiswahili lipo kati ya Kismayu na Mto Juba maeneo ya Somalia, Shungwaya. Kuanzia wakati huo, Waswahili walusambaa kusini na kufanya maskani zao mahali mbalimbali k.v. Lamu, Malindi, Mombasa, Kilwa, Mtwara, Pemba, Komoro na maeneo mengineyo ya mwambao wa upwa wa Afrika. Watu hawa wana lugha asilia iliyojulikana kama Kingozi. Hivyo basi, Kingozi ndicho Kiswahili kwa mujibu wa maoni haya.
c). Nadharia ya Jamadari- Jamadari adai kuwa wageni waliomiminika mwambao walijumuika na wenyeji wa Afrika Mashariki hata kabla ya kuzaliwa kwa Nabii Issa bin Maryam. Lengo kuu lilikuwa biashara. Jamadari adai kuwa kabila saba za Kiarabu zilizokuwemo ziliitwa Wazzania Waswahili naye Muarabu Ibn Batutwa.
d). Maoni ya Professor Ahmad Shekh Nabahani- kulingana na mwanazuoni huyu, Wangozi walitumia ngozi pakubwa katika shughuli nyingi na hawa ndio wanaodaiwa kuwa Waswahili.

Kiswahili kina hadhi na nafasi kubwa barani Afrika:
– Ukombozi kutoka ukoloni: lugha hii ilitumiwa na Waafrika wengi, aghalabu Afrika Madhariki kupigana dhidi ya ubepari wa mkoloni. Katika karne ya kumi na tisa, wakoloni walikuwa wameingia Afrika na kutawala mataifa mbalimbali. Mnamo mwaka wa (1990) karne ya ishirini, Kiswahili kilisemekana kuwa lugha ya saba katika lugha za ulimwengu, na niblugha inayotumika na watu wasiopungua milioni 110 . Kiswahili kilichangia pakubwa kuihamasisha Afrika kupigania ukombozi.
Kiswahili kimetapakaa katika eneo kubwa kuliko eneo lake la asili.

-Kiswahili ndio lugha yenye asili ya Afrika iliyoenea sehemu kubwa ya Afrika na hata kuvuka mipaka ya bara hili. Lugha hii inazungumzwa Uarabuni na imewaathiri Waafrika na wasiokuwa Waafrika.

– Biashara: Kiswahili kimechangia pakubwa katika shughuli za kibiashara Afrika na hata nje ya Afrika. Kuna msemo wa Kiswahili kuwa ‘Biashara ndio uti wa mgongo’. Katika enzi za utawala wa Sayyid Said bin Sultwaan, miji ya pwani ilinoga kibiashara. Kiswahili kama lugha kilitumika kueneza biashara. Kupitia kwa biashara, Kiswahili kimeweza kuenea barani Afrika. Lugha hii ilirahisisha mawasiliano na kurahisisha shughuli za kibiashara.
Dini ya Ukristo na Uislamu: dini ya Uislamu ilipokuja na kuingia miongoni mwa Waswahili, tayari Kiswahili kilikuwa chatumiwa maeneo ya pwani. Uislamu ulienezwa kwa kutumia Kiswahili. Wamishonari nao walifuata mkondo huo na kueneza dini kwa ligha ya Kiswahili. Hivyo basi, lugha hii ashirafu ina nafasi muhimu katika dini ya Kiislamu na Kikristo Afrika nzima.
Utamaduni: Kiswahili ina nafasi katika kukuza na kuendeleza tamaduni za Afrika. Kuna uhusiano mkubwa kati ya lugha na tamaduni. Tamaduni zinadhihirisha kaida na kanuni muhimu, na kaida hizi zinaputishwa kwa kutumia lugha. Kuna methali za Kiswahili zinazodhihirisha hili k.v. ‘Usiache mbachao kwa msala upitao.’ na ‘Mwacha mila ni mtumwa.’ Kiswahili basi kimechangia pakubwa katika ukuzaji wa tamaduni na sanaa za Waswahili Afrika yote. Sanaa hizi ni k.v. ngoma za Waswahili n.k.
Utunzi: Kuna kazi nyingi bunilizi zilizoandikwa kwa Kiswahili. Aghalabu, watunzi wa kazi za sanaa katika Kiswahili ni Waafrika. Licha ya watunzi hawa kubuni kazi zao, wameweza kutafsiri kazi za lugha nyingine zije Kiswahili. Kazi hizi zikiwemo riwaya, novela, hadithi fupi, makala bunifu, madhairi na nyimbo zinaisawiri jamii. Hivyo basi, Kiswahili ni lugha ambayo imechangia pakubwa katika kuakisi matukio ya kijamii kupitia kwa kazi za fasihi.
Vyama: kuna vyama mbalimbali ambavyo vimewaleta wanalugha pamoja. Vyama hivi vinachangia katika umoja wa Afrika. Vyama hivi mbalimbali vinapiga msasa lugha na kuchangia katika uundaji wa Kamusi na nakala nyinginezo za Kiswahili. Kamusi hizi na nakala hizi nyinginezo zinaipa Kiswahili hadhi bora Afrika na hata katika mataifa mengine ulimwenguni. Vyama hivyo ni pamoja na TUKI, CHAWAKAMA, CHAKITA, CHAKAMA n.k.
Elimu: Kiswahili ina nafasi yake katika elimu kwenye nchi mbalimbali za Afrika. Nchi ya Tanzania inatumia Kiswahili kuendeleza masomo takribani yote. Nchini Kenya, Kiswahili ni somo la lazima kuanzia chekechea hadi shule ya upili, vilevile, kozi mbalimbali zinamhitaji mwanafunzi awe amepasi vizuri katika somo hili la Kiswahili. Hivyo basi, Kiswahili kina nafasi murwa katika asasi ya elimu.
Uanahabari: Kiswahili kimepewa hadhi katika utangazaji wa habari. Habari hizi ni muhimu katika kuijuza jamii yanayojiri. Katika bara lote la Afrika, kuna stesheni maalum zinazopeperusha jumbe zake kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Dhana Ya Fonetiki.

Fonetiki ni taaluma inayojishughulisha na jinsi sauti yo yote inavyotolewa au inavyopatikana. Hii ni sayansi huru ambayo inatumia nadharia za sayansi halisi kama vile fizikia, uhandisi, baiolojia, nk. na kufaidi matokeo ya kiutafiti ya taaluma hizi. Mathalani, ili mwanafonetiki aelewe jinsi ala za sauti zinavyofanya kazi wakati wa utolewaji wa sauti, atafaidika na maelezo ya kibaiolojia kuhusu namna mfumo wa mwili wa mwanadamu unavyofanya kazi.

Mgulu, (2001:48) anadai: ‘ … fonetiki ni moja tu, lakini fonolojia zipo nyingi kama lugha zenyewe zilivyo nyingi. Kwa mfano, hatuna fonetiki ya Kiingereza au fonetiki ya Kiswhili. Fonetiki ni fonetiki tu. Kwa upande mwingine, tuna fonolojia za lugha mbalimbali ambazo hutofautiana. Tunazo, kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kifaransa, fonolojia ya Kinyamwezi, fonolojia ya Kindendeule, nk.

Tunapozungumzia upatikanaji wa sauti za lugha za binadamu, tunafafanua jinsi sauti za lugha husika zinavyotamkwa katika bomba la sauti la mwanadamu. (Tazama Jedwali 3.5). Tunazibainisha ala, hususani alasogezi na alapahala husika katika kuitamka sauti husika. Alasogezi ni ile ala ambayo inaweza kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. Alapahala au Ala-tuli ni ile ala ambayo haiwezi kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. (Tazama Kielelezo 3.1). Ni alasogezi ambayo hujisogeza kwenye alapahala husika wakati wa utamkwaji wa sauti husika (Nchimbi, 1979).

3.2.2 Utamkwaji wa Sauti-Fonimu za Kiswahili
Ieleweke kwamba hewa itokayo kwenye chemba ya mapafu ambayo sisi sote twaitumia kwa kupumua ili tuishi, ndiyo hiyo hiyo itumikayo katika utamkwaji wa sauti za lugha za binadamu. Hewa hiyo itapitishwa kwenye chemba zilizomo katika bomba la sauti kwa mujibu wa sauti inayotarajiwa kutamkwa hadi nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo au chemba ya pua

Hewa hiyo ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate ku

Lakini hewa hiyo, isipopitia chemba ya pua, ikapitia chemba ya midomo tu hadi nje, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-sing’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. (Tazama Kielelezo 3.4).

Tutaanza kufafanua utamkwaji wa sauti-fonimu-irabu za Kiswahili, ukifuatiwa na ufafanuzi wa utamkwaji wa sauti-fonimu-konsoni za Kiswahili. Ufafanuzi utafanywa kwa kuzingatia vigezo vin’ne, navyo ni:
(a) utamkwaji ki-alapahala,
(b) utamkwaji ki-sampuli,
(c) utamkwaji ki-ughuna,
(d) utamkwaji ki-ung’ong’o na,
(e) msimamo wa midomo hususani kuhusu utamkwaji wa fonimu-irabu.

3.2.3 Utamkwaji wa Fonimu-Irabu-Mama za Lugha za Binadamu
Irabu-mama katika lugha zote za binadamu ni /i a u/ ambazo utamkwaji wake katika bomba la sauti unajitokeza kwenye alapahala ya burutio-gumu/kaakaa-gumu ikishirikiana na alasogezi ya ulimi-kati ki-alasogezi-pahala kama ilivyo kwenye Kielelezo 3.5.

Katika Kielelezo 3.5 alasogezi-pahala za irabu, irabu-mama /I/ inajidhihirisha kuwa ni ya juu-mbele wakati irabu-mama /U/ ni ya juu-nyuma. Irabu-mama /A/ ni ya chini-kati.

Vigezo vya kufafanulia matamshi ya irabu ni kama ifuwatavyo:

(i) Kwa Mujibu wa Alapahala:ni burutio-gumu; ama sehemu ya mbele, ama sehemu ya kati, ama sehemu ya nyuma ya burutio-gumu.

(ii) Kwa Mujibu wa Alasogezi: ni ulimi; ama sehemu ya mbele (ulimi-mbele), ama sehemu ya kati (ulimi-kati), ama sehemu ya nyuma ya ulimi (ulimi-nyuma).

(iii) Kwa Mujibu wa Midomo: ni ama midomo-tandazi au midomo-futuzi.

(iv) Kwa Mujibu wa Mpenyo: ni ama mpenyo-mwembamba, ama mpenyo-mwembamba-kiasi, ama mpenyo-mpana.

(v) Kwa Mujibu wa Kidaka-Tonge: ni ama irabu-ng’ong’o ama irabu-sing’ong’o

(vi) Kwa Mujibu wa Nyuzi za Sauti/Glota: ni ama irabu-ghuna ama irabu-sighuna.

3.2.4 Utamkwaji wa Fonimu-Irabu //i e a o u/
Fonimu-irabu za kiswahili sanifu ni /i e a o u/. Fonimu-irabu-mbele za kiswahili sanifu ni /a e i/ na fonimu-irabu-nyuma ni /a o u/. Fonimu-irabu na nusu-irabu-mbele /a e i j/.

Wakati wa utamkwaji wa fonimu-irabu-mbele / a e i /, alasogezi ya ulimi-kati hujikweza kuelekea kwenye alapahala ya burutio-gumu-mbele. Mpenyo unaofanyizwa kati ya alasogezi ya ulimi-kati na alapahala yake ya burutio-gumu-mbele ni mpana wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [a], ni mpana kidogo wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [e] na ni mwembamba wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [i].

Mpenyo huu wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [i] unapofanyizwa kuwa mwembamba zaidi , basi matamshi ya sauti-endelezi ya nusu-irabu [j] hudhihirika, yaani [a e i j]. Aidha, midomo hubakia tandazi (Nchimbi,1979). Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o.

Utamkwaji wa Fonimu-Irabu na Nusu-Irabu-Nyuma /a o u w/:Wakati wa utamkwaji wa fonimu-irabu-nyuma / a o u /, alasogezi ya ulimi-kati hujikweza kuelekea kwenye alapahala ya burutio-gumu-nyuma. Mpenyo unaofanyizwa kati ya alasogezi ya ulimi-kati na alapahala yake ya burutio-gumu-mbele ni mpana wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [a], ni mpana kidogo wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [o] na ni mwembamba wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [u].Aidha, alasogezi ya mdomo-chini na alapahala ya mdomo-juu hujifutua, na kwa hiyo, kufanyiza mpenyo aina ya mviringo.

Mpenyo huu wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [u] unapofanyizwa kuwa mwembamba zaidi, basi matamshi ya sauti-endelezi ya nusu-irabu [w] hudhihirika, yaani [a o u w], na midomo hubakia futuzi. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o.

(Haya ni makala yaliyoandikwa na Mwita Peter)

Matumizi Ya Lugha.

Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Katika mada hii utajifunza mambo ya msingi ya kuzingatia unapotumia lugha. Utaelewa dhana mbalimbali zinazohusishwa na matumizi ya lugha kama vile rejesta, misimu, utatata katika lugha, lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi.
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika.

DHIMA YA MATUMIZI YA LUGHA
Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mila na desturi za jamii inayohusika.

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA MATUMIZI YA LUGHA.
1. Mada inayozungumziwa
Mada za mazungumzo zipo nyingi. Kuna mada za kijamii, kwa mafano ndoa, unyago, mapenzi, kifo, matanga, burudani, muziki n.k. Kuna mada za kibiashara kwa mfano bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara, faida n.k. Kwa hiyo, ili mazungumzo yaweze kwenda vizuri, wazungumzaji wanatakiwa kuzingatia mada husika.
2. Muktadha wa mazungumzo
Mazungumzo yanaweza kuathiriwa na miktadha tofauti. Kwa mfano kuna miktadha ya kidini, kiganga, huzuni, sherehe, kisiasa, kielimu, kibiashara n.k. Mazungumzo yanaweza kufanyika mjini, kijijini, ugenini, shuleni, dukani, hotelini n.k
3. Malengo ya mazungumzo hayo
Malengo ya mazungumzo nayo yanaathiri matumizi ya lugha. Kwa mfano, lengo linaweza kutoa taarifa, kuhoji, kukejeli, kutia moyo n.k. Sasa jinsi lugha itakavyotumika katika kutoa taarifa ni tofauti na itakavyotumika katika kutia moyo au kukejeli.
4. Uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji
Matumizi ya lugha huweza kuathiriwa pia na mahusiano ya wazungumzaji. Kuna mazungumzo baina ya watoto, wanafunzi, wazee, viongozi, marafiki n.k. Upo uhusiano wa daktari na mgonjwa, mwalimu na mwanafunzi, mnunuzi na muuzaji. Kwa hiyo mazingira baina ya pande hizi mbili yatategemea uhusiano wao, kwa hiyo kaida za uhusiano huu utapaswa kuzingatiwa.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia mambo haya manne, itawafanya wazungumzaji wawe makini katika uteuzi wa maneno, miundo, mifano na kina cha ufafanuzi wa maelezo au habari inayozungumzwa

AINA ZA REJESTA
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika
Rejesta za Mitaani Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke)n.k. Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka wa wazungumzaji wenyewe.
Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali) Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale. Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
– Maofisini au mahali popote pa kazi – Mahakamani – Hotelini – Hospitalini – Msikitini – Kanisanin.k
(a) Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
Nani wali kuku?
B: Mimi
Chai moja wapi?
B: Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”: ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
(b) Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitizausahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano:
Wakili wa Utetezi: Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Kenya?
Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Kenya na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi: Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishna Msaidizi:Sijui.
Kimsingi hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashtaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa maelezo.

iii. Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
– Vijana wenye rika moja, – Wazee wenyewe, – Wanawake wenyewe, – Wanaume wenyewe, – Mwalimu na mwanafunzi, – Meneja na wafanyakazi wake, – Mtu na mpenzi wake, n.k.
(c)Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.
MFANO:
‘Basi, Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana’ ‘Basi nilizamia infoo kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga’ ‘Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa noma kila mzamiaji’ Alikuwa mnoko kishenzi’ ‘Akatema mkwara mbuzi, nikajibu kwa mkwaradume….akabloo mimi ndani’.

MAANA YA MANENO
Wikiendi – Mwisho wa wiki. Kibaridi –tulivu. Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa. Zinga la Mnuso –sherehe kubwa. Saiti –sehemu. Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni. Noma – Hatari. Mnoko kishenzi – kinaa sana Mkwala mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.

DHIMA ZA REJESTA

Katika kipengele cha utambulisho wa kijamii tunaangalia namna aina ya lugha ya mazungumzo inavyoweza kujidhihirisha miongoni mwa watumiaji wake au kuwatambulisha na kuwatofautisha wanajamii husika. Pia katika utambaulisho wa kijamii tunaangalia vile ambavyo mtu hutambulika katika jamii kulingana na namna anavyoongea kulingana na hadhi, tabaka, na jinsi ambavyo mtu huyo anavyoweza kusababisha mshikamano au mwachano katika mazungumzo. Kwa mfano jamii itamtambua mwanajamii kuwa ni msomi kulingana na mtindo wa lugha ya mazungumzo anaoutumia, au ni mtu wa mtaani kulingana na lugha anayotumia.
Rejesta, ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hii ni kutokana na kwamba, madhumuni makuu ya mawasiliano katika biashara ni kuwavutia wateja na kuwafanya kuamini kuwa bidhaa ama huduma wanazouziwa ni za kiwango cha juu na ni thamani bora kwa pesa zao. Hivyo lugha ya biashara (rejesta), kwa kawaida ni lugha ya kutangaza uzuri wa bidhaa au huduma, huwa na sentensi au vifungu vifupi, mfano “Okoa mapesa chungu mbovu” pia huwa na lugha ya kupumbaza na kuaminisha, mfano “Kunywa XYZ kufumba na kufumbua afya yako itakurudia”.
Pia rejesta inasaidia sana kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji katika masuala mbalimbali ya kibiashara na hata katika huduma mbalimbali za kijamii. Mfano hospitalini “mbili mara tatu”, hotelini “kuku wali tafadhali”, sokoni “kata nusu” na maeneo mengine.
Baadhi ya rejesta hutumika kupunguza idadi ya maneno hivyo kufanya mazungumzo yawe mafupi na yanayoeleweka kwa urahisi mfano rejesta za hotelini kama vile:- Muuzaji: wapi ng’ombe? Mteja: hapa Muuzaji: wapi chai chapati? Mteja: hapa.
Pia katika kutolea elimu ya dini kanisani na msikitini rejesta ina nafasi kubwa katika kujenga maadili.
Vilevile rejesta ina nafasi ya kupamba mazungumzo, wazungumzaji wengi wanapozungumza hapa na pale hupenda kutumia maneno tofautitofauti ili kufanya mazungumzo yawe ya kuvutia. Mfano mazungumzo miongoni mwa vijana:
Kijana 1: Niaje? Nakuona umechili Kijana 2: mzuka jembe. Kama kawa… kama dawa!

MISIMU
Misimu ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. misimu inayodumu huweza kuingia katika methali, nahau au misemo ya lugha ya jamii hiyo.
Chanzo cha misimu
Misimu huzuka kulingana na mabadiliko ya kihistoria yanayoikumba jamii husika katika nyakati mbalimbali.
Misimu huzuka kutokana na haja ya watu kuelezea hisia zoa juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika vipindi fulani kwa mfano, njaa, mafuriko, vita n.k.

AINA ZA MISIMU
Misimu ya pekee Hii ni misimu ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja, na hujulikana miongoni mwao pekee.
Misimu ya kitarafa Misimu hii hujulikana na watu wengi katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni kata, wilaya au tarafa.
Misimu zagao Ni misimu iliyoenea nchi nzima au pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu hii husikika redioni, magazetini na hata kwenye vitabu. Msimu uliokita mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati rasmi.

SIFA ZA MISIMU
Huzuka na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya jamii.
Ni lugha isiyo sanifu.
Ina chuki.
Ni lugha ya mafumbo.
Ina maana nyingi.

DHIMA YA MISIMU
Hutumika kupamba lugha.
Hutumika kukuza lugha.
Hutumika kutunza historia ya jamii fulani.
Hutumika kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji.
Hufurahisha na kuchekesha.

TUNGO TATA
Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo tungo tata ni tungo ambayo inaweza kuwa na maana zaidi ya moja.
MFANO:
Patience amemwandikia Lilian barua Sentensi huweza kuwa na maana kuwa Patience ameandika barua kwenda kwa Lilian au Patience ameandika barua kwa niaba ya Lilian
Umefanikiwa kununua mbuzi? Sentensi hii huweza kumaanisha ununuzi wa mbuzi mnyama au mbuzi kifaa cha kukunia nazi.
Alimkuta amelala kwenye nyumba ya wageni Sentensi hii huweza kumaanisha, nyumba ya mtu lakini inatumika kwa ajili ya wageni kwa malipo au ni nyumba inayomilikiwa na watu ambao ni wageni katika eneo lile.
Attu ametumwa na Aritamba Sentensi hii inaweza kueleweka kumaanisha, Aritamba amemtuma Attu au Attu na Aritamba wametumwa wote kwa pamoja.

SABABU ZA UTATA
Utata katika tungo hutokea kwa sababu zifuatazo:
Neno kuwa na maana zaidi ya moja, kwa mfano neno mbuzi, kata n.k.
Kutozingatia taratibu za uandishi, Mfano; Tulimkuta Nyammy na rafiki yake, MazalavsTulimkuta Nyammy na rafiki yake Mazala. Katika sentensi hizi alama (,) ndio huleta tofauti, sentensi ya kwanza inamaana kulikuwa na watu wawili Nyammy na rafiki yake aitwaye Mazala na sentensi ya pili isiyo na alama (,) inamaanisha kulikuwa na watu wawili Nyammy na mtu mwingine ambaye ni rafiki yake Mazala
Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha wa matumizi ya maneno hayo.
Utamkaji wa maneno Wakati mwingine utata unaweza kujitokeza katika matamshi tu, ili hali katika maandishi utata hauonekani. Kwa mfano; Mimina wewe, katika maandishi linaweza kuandikwa mimi na wewe, na hivyo kuondoa utata.
Mjengo wa maneno Utata huu huzuka katika vitenzi kama pigia. Chanzo cha utata katika kitenzi hiki ni kiambishi –i-. Kiambishi hiki kinaweza kumaanisha: kwa ajili ya…, kwa sababu ya.., kwa kutumia chombo fulani.., au mahali fulani.

MFANO
Alimpigia ukorofi wake (kwa sababu ya)
Alimpigia kiatu (kifaa)
Alimpigia ndani (mahali)
Lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
Lugha ya mazungumzo
Lugha ya mazugumzo ni maongezi ya watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima kubwa ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii ya mazungumzo ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira yake, hivyo kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli zote za kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.

FAIDA YA LUGHA YA MAZUNGUMZO
Mzungumzaji anaweza kukaa ana kwa ana na msikilizaji, hivyo hukuza uhusiano.
Mzungumzaji anaweza kutumia ishara za mwili katika kusisitiza maelezo yake.
Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kuuliza au kuulizwa maswali.
Mzungumzaji anaweza kuonesha hisia zake kwa kulia, kupaza sauti, kupunguza sauti, kuonyesha furaha huzuni au hasira.
Mzungumzaji anaweza kuuliza maswali, kuona hisia za mzungumzaji kwa kusikiliza lugha zinazotolewa na kuangalia ishara za mwili zinazotumika.
Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kufuta usemi wake, kuongezea jambo au kutoa maelezo ya ziada.
Mzungumzaji anaweza kubadilisha lugha yake kulingana na mazingira aliyomo.
Mzungumzaji anao uhuru wa kutumia lugha ya mitaani, misimu kulingana na muktadha.

MATATIZO YA LUGHA YA MAZUNGUMZO
Maelezo lazima yahifadhiwe kichwani, hivyo kama mtu hana kumbukumbu, taarifa zilizotolewa hupotea na kusahaulika.
Mtumiaji wa lugha ya mazungumzo anaweza kurudiarudia vipengele fulani na hivyo kuichosha hadhira.
Ujumbe unaweza usieleweka kama unatolewa kwenye kelele nyingi.

LUGHA YA MAANDISHI
Hii ni lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi. Lugha ya maandishi huzihusiha pande mbili, mwandishi na msomaji. Lugha ya maandishi sharti iwe fasaha ili msomaji anaposoma maandishi hayo, apate kuelewa kila kitu, yaani asibaki akijiuliza maswali.
Lugha ya maandhi huambatana na alama za uakifishaaji, hii husaidia maandishi kusomeka vizuri na kueleweka kwa urahisi.

UBORA WA LUGHA YA MAANDISHI
Lugha ya maandishi huwawezesha watu walio mbali kuwasiliana.
Lugha ya maandishi hustawisha sarufi ya lugha na misingi yake, kwa sababu mwandishi anahakikisha kwamba anazingatia vizuri kanuni za kisarufi ili msomaji wake aweze kumwelewa.
Ili kuhakikisha maelezo yake yanaeleweka mwandishi analazimika kuandika kwa uwazi na kwa kuzingatia kanuni na miiko yote ya uandishi.

UDHAIFU WA LUGHA YA MAANDISHI
Lugha hii hutumiwa na wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
Lugha ya maandishi haina msisimko uletwao na lafudhi na matamshi.
Msomaji hukosa vidokezo vingi ambavyo katika lugha ya mazungumzo huchangia katika mawasiliano.
Lugha ya maandshi inamnyima mwandishi nafasi ya kupima welewa wa msomaji kwa kuwa hamwoni.

DHIMA YA LUGHA YA MAZUNGUMZO NA LUGHA YA MAANDISHI
Lugha ya mazungumzo na lugha ya maandshi zote zina umuhimu wa pekee katika maisha ya kila siku kwa sababu ndizo zinzaowezesha watu kuwasiliana kwa namna mbalimbali.
Umuhimu wa lugha ya maandshi pia hutokana na dhima yake kwa watu. Maandishi yanaweza kuhifadhiwa na kusambazwa kwa watu wengi hata walio mbali. Maandishi yanahifadhi kumbukumbu

Kwa hali hii,watu wanaweza kusoma yaliyofanyika karne nyingi zilizopita.