Sifa za lugha tandawazi.

Kimsingi, kuna sifa bainifu moja katika lugha tandawazi ambayo ni ‘ufupishaji’. Ufupishaji
huu unatokea kutokana na ‘udondoshaji’, ‘unambaishaji’ na ‘umatamshi’. Sifa hizi ingawa
zinaweza kuangaliwa kama zinazojitegemea, ni vijitawi tu vya sifa moja kuu yaani ufupishaji.
Kama nitakavyoonesha hivi punde, lengo la sifa hizi tatu: ‘udondoshaji’, ‘unambaishaji’ na
‘umatamshi’ hulenga kufupisha neno, sentensi au kifungu cha sentensi ili mhusika aweze
kutuma maneno mengi iwezekanavyo kwa kutumia nafasi ndogo. Kwa maneno mengine
anafanya mawasiliano ‘marefu’ kwa kutumia maneno machache. Sifa hizi zimeelezwa kwa
undani na wataalamu kama vile Crystal (2001, 2004, 2008a, 2008b). Inawezekana kadri
utafiti katika eneo hili unavyozidi kuongezeka, ndivyo tutakavyogundua sifa bainifu nyingine
zaidi ya hii ya ufupishaji, na hata kupata mawazo mapya kutokana na tafiti hizo.
Sifa hii ya ufupishaji ni matokeo ya utandawazi. Utandawazi umefafanuliwa na watu
mbalimbali kwa mitazamo tofauti. Katika makala hii ninatumia neno ‘utandawazi’
nikikubaliana na Sullivan na Kymlick (2007: 1) waliofafanua kuwa:
Kuongezeka kwa maingiliano ya watu nje ya mipaka ya mataifa yao, hususan
katika nyanja za biashara na uwekezaji, lakini pia ni utoaji wa teknolojia, safari za
watu na mtawanyiko wa mitindo ya maisha ya kimagharibi inayosukumwa
ulimwenguni kupitia bidhaa kama vile sinema na filamu za Hollywood na vyakula
vya McDonald (Tafsiri ya mwandishi)
Katika maana hii ya Sullivan na Kymlick, suala la utolewaji wa teknolojia halijawa wazi
kama hayo mengine. Nchi nyingi zinazoongea Kiswahili kwa mfano, zimepokea zaidi bidhaa
zilizokwisha kuundwa kuliko zilivyopokea teknolojia. Kwa mfano, nchi hizi zimepokea simu
za kiganjani bila kupokea teknolojia ya utengenezaji simu hizo. Aidha, watumiaji wa simu
wamepokea simu hizo pamoja na namna fulani ya utamaduni katika matumizi ya simu.
Matumizi ya lugha ya mawasiliano katika simu hizi yamekuwa yakifanana kwa watumiaji wa
lugha ya Kiswahili mahali pengi wanapokuwa. Lugha hii tandawazi ina sifa kama
nilivyozieleza na inasukumwa mbele na utandawazi kama nilivyoueleza. Hata hivyo kuna sifa
ya ziada katika utandawazi popote ulimwenguni. Sifa hiyo ni watu kutaka kutumia zaidi huku
wakilipia kidogo. Sifa hii ndiyo tunayoiona katika matumizi ya simu: watumiaji wanataka
kuwa na maneno mengi kadri inavyowezekana, lakini wana nafasi ndogo katika simu zao, na wangelipenda kutokutumia fedha zaidi kama ikiwezekana. Ufupishaji wa mawasiliano
unaoletwa na lugha tandawazi unaweza kuonekana kuwa unamwelekeo huu.
Ikiwa tunakubaliana kuhusu sifa hii bainifu na vijitawi vyake, tutafakari sasa changamoto
zinazotolewa na lugha hii, katika nadharia za isimujamii. Nadharia tunayoijadili hapa ni ile
inayohusiana na kuchanganya msimbo na kubadili msimbo (code mixing na code switching).
Katika isimujamii, mbinu hii ya matumizi ya lugha hutokeza hali mbili ambazo zote uhusisha
maneno. Kwa mujibu wa King’ei (keshatajwa) kuchanganya msimbo hutokea pale ambapo
mzungumzaji huamua kuwa na misimbo au ‘ndimi’ zaidi ya moja katika usemi mmoja.
King’ei ametumia mifano ya misimbo ya Kiswahili na Kiingereza. Aidha ameelezea kuwa
mazingira ya uchanganyaji misimbo unaweza kuhusiaha lahaja za lugha moja, na hapo
amaonesha mifano ya uchanganyaji misimbo inayohusisha Kiswahili, Kiingereza na Sheng
(2010: 25). Katika mifano yote miwili, amefafanua uchanganyaji huo unaohusisha maneno tu.
Kubadili msimbo kunaelezwa kuwa ni “kuchanganya lugha mbili tofauti lakini katika kauli
tofauti badala ya kuwa katika usemi mmoja” (kama hapa juu). Na hata katika mfano huu,
maelezo yake yanahusisha maneno tu. Jambo hili ni tofauti katika lugha tandawazi; lugha
inayoletwa na matumizi ya simu za viganjani, barua pepe na maongezi katika tovuti. Utafiti
wa Crystal katika lugha hii ya simu za viganjani, umehusisha lugha ya Kiingereza tu. Ingawa
vitabu na makala zake zimesaidia sana kutoa mwanga katika makala hii, hazikujadili
changamoto zinazojitokeza kama lugha mbili au zaidi zikiwa pamoja. Mifano inayotolewa
toka kwa wazungumzaji wa Kiswahili na lugha nyingine ni ya kipekee ambayo hatuna budi
kuijadili kwa kina kama sehemu inayofuata inavyoanzisha mjadala huu.

(Makala haya ni kwa hisani ya Prof.Aldin Mutembei)

Mabadiliko na Uchanganyaji msimbo katika Isimujamii.

Kwa mujibu wa Wanaisimujamii, kuna miundo miwili ya lugha katika Isimujamii. Moja ni
muundo wa kubadili misimbo na wa pili ni muundo wa kuchanganya misimbo. Kwa mujibu
wa Weinreich (1953), aliyenukiliwa Naseh (1997: 202), ubadilishaji misimbo hutokea katika
mazingira ya mazungumzo pale “watu wenye zaidi ya lugha moja wanapobadili msimbo
kutoka lugha moja kwenda nyingine kwa mujibu wa taratibu za mabadiliko katika lugha.”
Naye Hymes (1974) anaeleza ubadilishaji msimbo kuwa ni matumizi ya lugha mbili au zaidi
zinazogusa sentensi zaidi ya moja, au hata mitindo tofauti ya lugha. Ufafanuzi wa Bokamba
(1989) unatupeleka mbele kidogo pale anapoelezea ubadilishaji msibo kuwa ni “uchanganyaji
wa maneno, makundi ya maneno au sentensi kutoka katika mifumo miwili tofauti ya kisarufi
na kwa kuvuka mipaka ya sentensi katika lugha” (Ayeomoni, 2006: 90). Mawazo ya
Ayeomoni hayatofautiana sana na yale ya akina Grosjean (1982) na Myers-Scotton
(1993a/1997) ambao nao waliangalia ubadilishaji msimbo kuwa ni matumizi ya msimbo
mmoja au lugha moja au zaidi katika mazungumzo au tukio uneni ambapo mabadiliko hayo
yanaweza kuwa ni neno moja, kikundi cha maneno, sentensi au zaidi ya sentensi moja. Kwa
ujumla tunaona kuwa ubadilishaji misimbo ni suala linalohusiana na maneno katika lugha.
Jambo kama hili tunaliona pia katika maana ya uchanganyaji misimbo.
Uchanganyaji misimbo unafafanuliwa na Muysken kuwa ni mazingira yote ambapo
kipengele kimoja cha kileksika na sehemu ya kisarufi kutoka lugha mbili tofauti
huchanganywa pamoja au hutokea kwa pamoja katika sentensi moja (2000: 1). Ubadilishaji
na uchanganyaji misimbo umeangaliwa na wanaisimu wengine kuwa ni mabadiliko
yanayotokea kwa darajia mbili. Moja ni baina ya sentensi na sentensi, na nyingine ni ndani ya
sentensi moja (Ho 2007). Kwa mujibu wa Poplack (1980: 586), mazingira ya ubadilishaji
msimbo huwapo pale vipengele vya lugha mbili zinazotumika katika mabadilishano hayo (L1 na L2) havikiuki kaida za kisintaksia za lugha mojawapo. Ingawa ukweli umekuwa ni huu
katika maandishi ya kiisimujamii, zipo tofauti kidogo katika kubadili msimbo au hata
kuchanganya misimbo kupitia simu za kiganjani hasa pale kunapotokea matumizi ya namba.
Kama ilivyo kwa kubadilisha misimbo, kuchanganya misimbo kunagusa tu maneno katika
lugha zinazoshughulikiwa na sio namba. Ujio wa lugha tandawazi inayotumika kwa simu za
viganjani, barua pepe na maongezi katika tovuti, umeleta mabadiliko katika lugha ambapo
miundo ya uchanganyaji na ile ya mabadiliko huingiza pia namba. Kabla hatujaanza kuijadili
lugha tandawazi kwa undani, tuangalie sifa bainifu za lugha hii.

(Makala haya ni kwa hisani ya Prof.Aldin Mutembei)

Mabadiliko na Uchanganyaji msimbo katika Isimujamii.

Kwa mujibu wa Wanaisimujamii, kuna miundo miwili ya lugha katika Isimujamii. Moja ni
muundo wa kubadili misimbo na wa pili ni muundo wa kuchanganya misimbo. Kwa mujibu
wa Weinreich (1953), aliyenukiliwa Naseh (1997: 202), ubadilishaji misimbo hutokea katika
mazingira ya mazungumzo pale “watu wenye zaidi ya lugha moja wanapobadili msimbo
kutoka lugha moja kwenda nyingine kwa mujibu wa taratibu za mabadiliko katika lugha.”
Naye Hymes (1974) anaeleza ubadilishaji msimbo kuwa ni matumizi ya lugha mbili au zaidi
zinazogusa sentensi zaidi ya moja, au hata mitindo tofauti ya lugha. Ufafanuzi wa Bokamba
(1989) unatupeleka mbele kidogo pale anapoelezea ubadilishaji msibo kuwa ni “uchanganyaji
wa maneno, makundi ya maneno au sentensi kutoka katika mifumo miwili tofauti ya kisarufi
na kwa kuvuka mipaka ya sentensi katika lugha” (Ayeomoni, 2006: 90). Mawazo ya
Ayeomoni hayatofautiana sana na yale ya akina Grosjean (1982) na Myers-Scotton
(1993a/1997) ambao nao waliangalia ubadilishaji msimbo kuwa ni matumizi ya msimbo
mmoja au lugha moja au zaidi katika mazungumzo au tukio uneni ambapo mabadiliko hayo
yanaweza kuwa ni neno moja, kikundi cha maneno, sentensi au zaidi ya sentensi moja. Kwa
ujumla tunaona kuwa ubadilishaji misimbo ni suala linalohusiana na maneno katika lugha.
Jambo kama hili tunaliona pia katika maana ya uchanganyaji misimbo.
Uchanganyaji misimbo unafafanuliwa na Muysken kuwa ni mazingira yote ambapo
kipengele kimoja cha kileksika na sehemu ya kisarufi kutoka lugha mbili tofauti
huchanganywa pamoja au hutokea kwa pamoja katika sentensi moja (2000: 1). Ubadilishaji
na uchanganyaji misimbo umeangaliwa na wanaisimu wengine kuwa ni mabadiliko
yanayotokea kwa darajia mbili. Moja ni baina ya sentensi na sentensi, na nyingine ni ndani ya
sentensi moja (Ho 2007). Kwa mujibu wa Poplack (1980: 586), mazingira ya ubadilishaji
msimbo huwapo pale vipengele vya lugha mbili zinazotumika katika mabadilishano hayo (L1 na L2) havikiuki kaida za kisintaksia za lugha mojawapo. Ingawa ukweli umekuwa ni huu
katika maandishi ya kiisimujamii, zipo tofauti kidogo katika kubadili msimbo au hata
kuchanganya misimbo kupitia simu za kiganjani hasa pale kunapotokea matumizi ya namba.
Kama ilivyo kwa kubadilisha misimbo, kuchanganya misimbo kunagusa tu maneno katika
lugha zinazoshughulikiwa na sio namba. Ujio wa lugha tandawazi inayotumika kwa simu za
viganjani, barua pepe na maongezi katika tovuti, umeleta mabadiliko katika lugha ambapo
miundo ya uchanganyaji na ile ya mabadiliko huingiza pia namba. Kabla hatujaanza kuijadili
lugha tandawazi kwa undani, tuangalie sifa bainifu za lugha hii.

(Makala haya ni kwa hisani ya Prof.Aldin Mutembei)

Dhana Ya Wahusika.

Dhana ya wahusika katika kazi za fasihi imewahi kufasiliwa na watafiti kadhaa. Kama
ilivyokwishaelezwa kuwa wahusika katika kazi za fasihi ni viumbe wanaopatikana katika hadithi
yoyote ile. Viumbe hawa huwa sehemu ya kazi nzima. Pili, wahusika ni binaadamu
wanaopatikana katika kazi ya kifasihi, na ambao wana sifa za kimaadili, kitabia, kiitikadi,
kifalsafa ambazo hutambulishwa na wanayoyasema na wanayoyatenda. Wahusika huweza
kutambulishwa pia na maelezo ya mhusika au msimulizi, msingi wa hisia, hali ya kimaadili,
mazungumzo na matendo ya wahusika ndio kiini cha motisha au uhamasishaji wa wahusika
(Wamitila, 2002).
TUKI (1998:169), wamefasili wahusika kuwa ni watu, miti au viumbe vinavyowakilisha watu
katika kazi za fasihi. Wahusika hutumiwa katika kazi za fasihi ili kuwakilisha hali halisi ya
maisha ya watu katika jamii inayohusika. Katika mgogoro unaozungumziwa katika kazi ya fasihi
hutumiwa kuwakilisha mawazo mbalimbali ya pande mbili au zaidi za mgogoro huo.
Maelezo hayo ya Wamitila na TUKI yalikuwa na umuhimu mkubwa katika kusukuma mbele
kazi hii. Hii ni kutokana na kwamba, Wamitila amedokeza maswala muhimu sana katika kutoa
maana ya wahusika katika kazi za fasihi. Sifa kama zile za kimaadili, kitabia, kiitikadi, kifalsafa
ambazo huwa zinawatambulisha wahusika hao zilitupa mwanga na muongozo mzuri katika
utafiti wetu huu uliolenga kuchunguza namna wahusika wanavyolandana na majina yao katika
riwaya teuliwa.
Rono (2013) akimnukuu Msokile (1992:42-43), anaeleza kwamba, wahusika husawiriwa kisanaa
na mwandishi ili waweze kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha katika jamii. Mwandishi
huwasawiri wahusika kwa wasomaji wake kwa kutumia sifa pambanuzi walizonazo, jinsi
walivyo, mambo gani hawayapendi na yapi wanayapenda katika maisha yao na kadhalika.
Wahusika hao hutumia misemo, nahau, tamathali za usemi na methali katika mazungumzo yao
ili kujenga tabia na hali ya kisanaa Rono (ameshatajwa), anaendelea kueleza kuwa, wahusika wa kazi za sanaa huwa na tabia
zinazotofautiana kati yao kwa sababu mbalimbali. Kwanza kabisa inategemea mwandishi ana
lengo gani analotaka kuonyesha katika kazi yake ya sanaa. Pili, aina ya kazi ya sanaa inaweza
kuathiri aina ya wahusika jinsi walivyosawiriwa, kuaminika kwao, wanavyohusiana wao kwa
wao, uwakilishi wao na majina yao. Wahusika katika hadithi ni mhimili mkubwa katika fasihi
andishi na hata simulizi.
Aidha, Msokile (1992), akiwanukuu Penina Muhando na Ndyanao Balisdya wanasema kwamba
wahusika wanaweza kuumbwa kinafsia, kiakili na kimwili. Kutokana na ujenzi wa aina hii,
mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au anaweza kuonyesha mabadiliko yake kila
anapokutana na mazingira tofauti. Ataonyesha mabadiliko katika uhalisia wake kwa kuzingatia
nguvu zinazomzunguka kama vile za utamaduni, siasa, uchumi na kadhalika.
Kwa mujibu wa Wamitila (2008:369), wahusika ni nyenzo kuu katika fasihi kwa sababu
wahusika ndiyo dira ya matukio na matendo yanayopatikana katika kazi ya kifasihi inayohusika.
Mtazamo wa dhana ya wahusika hutofautiana kutegemea mkabala anaouchukua mhakiki na
nadharia ya fasihi inayohusika.
Mhusika ni mtendaji katika kazi ya kifasihi na huwa kielelezo cha viumbe wanaopatikana
ulimwenguni, ingawa si lazima sifa zote za mhusika zifungamane moja kwa moja na za
wanadamu. Hii ndio maana neno “mhusika” linatumika bali si ‘mtu’ au ‘Kiumbe’. Mwelekeo wa
kuwahusisha wahusika wa kifasihi na binadamu wanaopatikana katika hali halisi huathiri kwa
kiasi fulani matarajio ya usawiri wa uhusika. Upo mwelekeo mkubwa wa kuwachunguza
wahusika wa kifasihi kwa kuwafungamanisha na binadamu halisi na hata, labda kutokana na
athari za mielekeo ya kimaadili, tukitarajia kuwa wahusika, hasa wale wakuu watakuwa na
maadili fulani.

Hata hivyo, tunakubaliana na Kundera (2007) kuwa, wahusika wa kifasihi hawahitaji kupendwa
kutokana na maadili yao bali wanachotakiwa kufanywa ni kueleweka. Matendo yanayopatikana
katika kazi ya kifasihi huhusishwa na wahusika. Matendo hayo ni nguzo kuu ya dhamira na
maudhui yanavyoendelezwa katika kazi inayohusika. Mawazo hayo ya Kundera yalitupa
mwanga mkubwa wakati wa kuwachungua wahusika na namna wanavyolandana na majina yao
na namna walivyobebeshwa dhamira na waandishi wa riwaya teuliwa.
Kulingana na Njogu na Chimerah (1999:45), wahusika ni viumbe wa sanaa wanaobuniwa
kutokana na mazingira ya msanii. Mazingira haya yaweza kuwa ya kijiografia, kihistoria,
kijamii, kitamaduni au ya kisiasa. Wahusika hujadiliwa kwa namna wanavyoingiliana na
dhamira na hili hujitokeza kutokana na maneno, tabia na matendo yao, yaani kulingana na hulka
yao. Wahusika wa aina yoyote wawe watu au viumbe hurejelea na huakisi sifa na tabia za
binadamu katika jamii husika.

Njia za kubainisha wahusika.

Uchunguzi wa historia na maendeleo ya fasihi unadhihirishwa kuwa, wahusika wa kifasihi
hubadilika kadri wakati unavyoendelea. Wahusika wanaopatikana katika kazi za kifasihi za
miaka ya zamani wanatofautiana kwa kiasi kikubwa na wahusika wanaopatikana katika kazi za
fasihi za miaka ya baadaye.
Njogu na Chimerah (1999:40-44), wanarejelea wahusika wanaozungumziwa Mlacha na
Madumulla (1991).
Wamitila (2008: 382-392), amegawanya wahusika katika makundi manne. Mhusika wa jadi,
mhusika wa kimuundo au kimtindo, mhusika wa kihalisi na mhusika wa kisasa.

Mhusika wa kijadi.
Dhana ya kijadi inakwenda na suala la wakati na hasa wakati wa zamani. Mhusika wa aina hii
basi ni anayeweza kuelezwa kama mhusika wa zamani. Mtindo huu wa kusawiri wahusika
umetumiwa na baadhi ya waandishi mbali mbali wa kazi za fasihi. Kwa mfano, katika tamthiliya
ya Kivuli Kinaishi (1990), mhusika Bi Kizee ni mfano wa mhusika wa kijadi. Aidha, katika
tamhiliya ya Mfalme Juha (1971) wahusika Mfalme na Juha ni mfano wa wahusika wa kijadi
kwa sababu hawa wamekuwa ni wahusika wa kimapokeo katika kazi mbali mbali za kisimulizi.
Mhusika wa Kimuundo na Kimtindo
Mhusika wa kimuundo na kimtindo huainishwa kuhusiana na wahusika wanaorejelewa. Mawazo
ya wana muundo ni ya kimsingi katika kuwainisha wahusika wa aina hii. Kulingana na Wamitila
(2008), wahusika wa aina hii wameainishwa kama ifuatavyo:
Mhusika wa Kiuamilifu
Huyu ni mhusika ambaye anabainishwa kwa kuwa na sifa za aina moja ambazo kimsingi
zinapangiwa kumfanya mhusika huyo kuwa chombo cha mwandishi ili kutimiza lengo fulani.
Pia anaweza kubainishwa kwa kuangalia nafasi yake ya kiutendaji. Mfano nzuri ni Karama
katika riwaya ya Kusadikika (1981) , yeye atumiwa na msanii kufanikisha lengo lake akiwa
kama mzalendo na mkombozi wa jamii.

Mhusika wa kiishara.
Mhusika wa kiishara anatumiwa kiishara, yaani ni sehemu ya uashiriaji katika kazi ya kifashi.
Kwa mfano Rono (2013), anamtumia Mhusika Amani katika Kidagaa Kimemwozea (2012),
kama ni ishara ya mabadiliko katika jamii ambayo haiwezi kuuliwa na harakati za utawala
mbaya wa kuyazuia mabadiliko yenyewe. Ndiye aliyeongoza katika uchunguzi wa nyendo za
Nasaba bora wakiwa na Majisifu kisha wakagundua matendo yake maovu. Aidha, kisa cha fahali
kumeza nguo katika riwaya hiyo ya Kidagaa Kimemwozea ni ishara ya nasaba bora aliyokuwa akitafuna ardhi na mali za raia wake bila huruma na kuwaacha maskini. Usimulizi wa mto
Kiberenge na maji yake kutonywewa na wakazi wa maeneo yake ni ishara kuwa, wakati hao
huafikiana na maswala fulani bila utafiti au uchunguzi wowote.
Wahusika wa Kinjozi
Wahusika wa kinjozi ni wahusika wanaohusishwa na fantasia. Hupatikana katika ulimwengu wa
ajabu. Kwa mfano, Mhusika Pama katka riwaya ya Siri za Maisha ni mfano wa Mhusika wa
kinjozi kutokana na matendo yake ya kiajabu.

Mhusika wa kihalisi.
Msingi mkuu katika uainishaji wa wahusika wa aina hii ni kanuni ya maisha halisi, kwa
kutegemea kanuni ya ushabihi kweli. Mhusika wa kihalisia ana sifa nyingi zinazohusishwa na
binadamu katika maisha ya kila siku. Kulingana na Wamitila (2008), tapo hili lina wahusika wa
aina tatu, mhusika wa kimapinduzi, mhusika wa kisaikolojia na mhusika wa kidhanaishi.
Wahusika hawa wamefanyiwa uchambuzi kama ifuatavyo:
Mhusika wa Mapinduzi
Mshusika wa kimapinduzi ana sifa zote zinazohusishwa na mtu anayeweza kupatikana katika
maisha halisi. Mhusika huyu anasukumwa na kuchochewa na nia ya kutaka kubadilisha jamii
yake. Wahusika Mdoe na Sikamona katika riwaya ya Zawadi ya Ushindi ni mifano mizuri,
wanasukumwa na nia ya kutaka kuyabadilisha maisha katika jamii yao ambayo inaongozwa na
viongozi walafi na wananchi wengine wenye tamaa ya kupata mali kwa njia zisizo za halali.
Mhusika wa Kisaikolojia
Mhusika wa kisaikolojia anaonyeshwa kwa undani zaidi na labda hata misukumo ya kisaikolojia
ya matendo yake kuonyeshwa kwa njia bayana. Mama Ntilie katika riwaya ya Watoto wa Mama
Ntilie ni mhusika wa kisaikolojia kulingana na yale anayopitia kutoka kwa mumewe Lomolomo
na pia kufukuzwa kwa watoto wake shule kunapelekea kutumia akili yake zaidi ili apambane na
hali hiyo na kumiliki nafsi yake isiathirike kisaikolojia.

Mhusika wa kidhahanishi.
Mhusika wa kidhanaishi anaakisi sifa kadhaa zinazohusishwa na falsafa ya udhanaishi ambayo
msingi wake ni kudadisi ukweli, furaha na hali ya kuweko maishani. Mfano nzuri wa kazi za
kifasihi zilizoandikwa na Kezilahabi kama vile Nagona na Mzingile zinasadifu sana matumizi ya
wahusika wa kidhanaishi. Katikariwaya ya Nagona , wahusika Paa na Mimi wanawakilisha
kundi hili.
Wafula na Njogu (2007), wanasema kwamba mhusika anaweza kuangaliwa kama mtu binafsi na
maisha yake. Waliorodhesha wahusika kama jaribosi au nguli, kivuli na wengineo. Nguli
aghalabu huwa mhusika mkuu mbaye husafiri kwa sababu fulani. Mara nyingi safari hii huanzia
utotoni hadi anapofikia utu uzima. Wakati mwingine hii inaweza kuwa safari ya kikweli ambapo
nguli anajizatiti kukisaka kitu au kujisaka mwenyewe. Mkinzani wa nguli hupambana kuiharibu
mipango ya nguli kwa kujaribu kumwangamiza. Aghalabu mhusika huyu huwa mzinzi, mlafi na
wakati mwingine huwa tajiri kama vile Mzoka katika riwaya ya Miradi Bubu ya Wazalendo.
Aidha katika riwaya ya Adili na Nduguze, mhusika Adili anasafiri kwa ajili ya kufanya biashara.
Katika safari hizo tunaoneshwa ndugu zake Mwivu na Hasidi wanavyoamua kumtupa baharini
kutokana na wivu na choyo.
Mwisho tunaona namna anavyookolewa na mtoto wa Mfalme wa Kijini, Huria. Mjadala huu
kuhusu matapo ya wahusika ulikuwa na manufaa sana kwa mtafiti, kwa sababu, mtafiti alitumia
mawazo hayo, ili kubaini aina za wahusika waliotumika katika riwaya teuliwa.

Mbinu za kusawiri wahusika.

Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mwandishi anaweza kutumia njia kadhaa na tofauti katika
kuwasawiri wahusika wake. Msanii ana uhuru sio tu wa kuwatumia wahusika wa aina fulani, bali
wa kuiteua namna ya kuwawasilisha wenyewe. Kama wasomi na wahakiki wa fasihi,
tunategemea sifa kadhaa kuwaelewa wahusika hao: maumbile yao, mienendo na tabia zao, lugha
zao, vionjo vyao, uhusiano wao na wahusika wengine, hisia zao kwao na wengine, mazingira na
mandhari yao, kiwango chao cha elimu, jamii yao nakadhalika.

Mbinu zinazotumika kusawiri wahusika ni kama vile; mbinu ya kimaelezi, mbinu ya kidrama,
mbinu ya uzungumzi nafsi wa ndani, mbinu ya majazi au matumizi ya majina, mbinu ya
kuwatumia wahusika wengine na mbinu ya ulinganuzi na usambamba.
Wamitila ameainisha na kuchambua mbinu zifuatazo ambazo hutumika katika kuwasawiri
wahusika. Mbinu hizo zimetolewa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Mbinu ya kimaelezi.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002:23-24), anayetumia mbinu hii huzieleza sifa za mhusika na
mara nyengine hutoa picha ya maneno inayomwelezea mhusika anayehusika. Kwa kutumia
mbinu hii, mwandishi anakuwa na nafasi ya kubainisha mapenzi au chuki yake dhidi ya
wahusika fulani. Hii ni njia rahisi ya kuwasawiri wahusika na hasa kwa kuwa mwandishi
anaweza kutoa maelezo machache yanayoifumbata tabia au wasifu wa mhusika ambao
ungechukua muda mrefu kutokana na matendo yake mwenyewe. Hata hivyo, hii ni mbinu
ambayo ina udhaifu pia.
Mbinu hii ya kimaelezi haimpi msomaji nafasi ya kushiriki katika kuitathmini tabia ya mhusia
fulani. Analazimika kuukubali msimamo na kuridhika na maelezo ya mwandishi. Mfano
unaofuata unaonesha namna ya mbinu hii inavyotumika; kutoka katika riwaya ya Vuta n`kuvute
ya Shafi A Shafi:
“Yasmini alikuwa na kijuso kidogo cha mdawiri mfano wa tungule na macho makubwa ambayo
kila wakati yalionekanwa kama yanalengwalengwa na machozi. Alikuwa na pua ndogo,
nyembamba na chini ya pua hiyo ilipangana midomo miwili mizuri iliyokuwa haitulii kwa tabia
yake ya kuchekacheka, huku akionyesha safu mbili ya meno yake mazuri. Alikuwa na kichaka
cha nywele nyeusi zilizokoza ambazo zilianguka kwa utulivu juu ya mabega yake. Alikuwa si
mrefu lakini hakuwa mfupi wa kuchusha, na matege aliyokuwa nayo yalizidi kuutia haiba
mwendo wake wakati anapotembea” (1999:1).

Haya ni maelezo ya mwandishi kumhusu mhusika huyu ambayo yanatokea katika sehemu ya
mwanzo. Ingawa hasemi wazi wazi, uteuzi wake wa maneno unatuelekeza kuamini kuwa ana
mtazamo fulani kumhusu mhusika na ambao huenda ukatuelekeza kwenye njia fulani.

Mbinu ya kidrama.
Wamitila (2002), mbinu hii ya ki-muhakati (ki-mimesia), kama ilivyo katika tamthilia,
huonyesha wasifu wa mhusika wake. Pia mbinu hii inamwezesha msomaji au mhakiki kumjua na
kumweleza mhusika bila ya kuathiriwa na mtazamo wa mwandishi au msimulizi kumhusu.

Mbinu ya uzungumzaji nafsi wa ndani.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mbinu hii hulinganuliwa na nyengine inayojulikana kama
mkondo wa king’amuzi/kirazini. Mawaazo yanayopatikana katika mbinu hii huwa na
mshikamano wa muwala, mawazo hayo yamepangika kama unavyoweza kutokea katika
ung’amuzi nafsi wa kawaida, yaani pale endapo mhusika anapoongea peke yake.
Kwa upande mwengine, mkondo wa king’amuzi ni mbinu inayotumiwa kuonyesha mawazo
hayo au hisia za wahusika bila ya kuyahariri mawazo hayo au kuyapanga kwa namna yoyote ile
iwayo. Hii ni mbinu inayotumiwa sana katika uandishi wa unaokita kwenye tapo la usasaleo.
Mbinu ya uzungumzi nafsi wa ndani hujulikana kama “mjadala wa ndani” au “mjadala mdogo”.
Mjadala unaonekana hapa unazihusisha sauti mbili zinazohusika kwenye majibizano. Sifa
muhimu ni kuwa lazima maswali au majibu yanayopatikana yaibuke katika sauti ambazo
zinawakalisha mikabala, imani au sifa tofauti.

Mbinu ya kuwatumia wahusika wengine.
Wamitila (2002:26), badala ya kuyatumia majina ya wahusika, mwandishi anaweza kusawiri
mhusika kupitia kwa kuelezwa na wahusika wengine. Wahusika wanaweza kuelezwa na
wahusika wengine, yaani tunawajua kutokana na maneno ya wahusika wenzao. Hapa pana
tathmini ya mhusika ambayo ni ya ndani (kwa wahusika wengine), kuliko ya nje kama ya
masimulizi (mbinu ya kimaelezi).
Hata hivyo lazima tukumbuke maneno anayoyatamka mhusika A kumhusu mhusika B yanaweza
kuangaliwa kwa njia mbili. Kwanza, yanaweza kutusaidia kumwelewa B kwa kutufichulia
mambo ambayo hatuwezi kuyajua bila ya kuelezwa. Pili, inawezekana kauli anazozitamka A
kumhusu B zikatuonesha alivyo mhusika A kuliko alivyo B.

Mbinu ya ulinganuzi na usambamba.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mwandishi anaweza kuitumia mbinu za usambamba na
ulinganuzi katika kuwasawiri na kuwakuza wahusika wake. Ulinganuzi ni nini? Huu ni
ulinganishi kwa kinyume. Kuweko kwa mhusika ambaye ni kinyume cha mhusika fulani huweza
kuwa ni mojawapo ya uhusika.
Mwandishi anaweza pia kuwaweka wahusika au kuwaonyesha kwa namna ambazo ni sambamba
na kwa njia hii humfanya msomaji au mhakiki aziwazie tofauti au mfanano wa sifa zao. Ni
muhimu kukumbuka kuwa ulinganuzi sio tu mbinu ya uhusika bali hutumiwa katika usimulizi
wa matukio na ukuzaji wa dhamira na maudhui.
Wakati huo huo mwandishi anaweza kuwasawiri wahusika kwa namna ambavyo tabia zao
zinaonesha kupingana kwa aina fulani. Yaani tukimwangalia mhusika kwa makini, tunahisi
kuwa kuna kupingana kwa sifa fulani katika uhusika wake. Hapa tunasema kuwa za ki-nzani.

Mbinu ya majazi au matumizi ya majina.

Wamitila (2002), waandishi wa kazi za kifasihi huweza kuyatumia majina ya wahusika ambayo
huakisi mandhari zao, wasifu wao, itikadi zao, vionjo vyao na kadhalika. Uchunguzi wa majina
ya wahusika lazima uhusishwe na msuko, mbinu za utunzi, ucheshi, dhamira na maudhui na
itikadi au motifu katika kaziinayohusika.
Tunapozungumzia kulandana kwa wahusika na majina yao katika kazi faulani ya fasihi, ni kule
kuwiana kwa matendo ya wahusika na majina yao, sifa zao na majina yao, lugha yao na majina
yao, kujiamini kwao na jinsi majina yao yalivyo, elimu yao na majina yao, maana ya majina yao
na jinsi yanavyofanana na wao wenyewe ambapo msanii wa kazi ya fasihi huzitumia sifa hizi,
katika kusadifu hali fulani iliyozoeleka katika jamii.
Maelezo hayo yalikuwa na mchango mkubwa kwa mtafiti katika kusukuma mbele utafiti huu.
Hii inatokana kuwa Wamitila ameweza kuonesha na kufafanua vipengele vya msingi ambavyo
vilitumiwa na mtafiti katika kuchambua lengo la utafiti na hatimae kuweza kufikia lengo la
utafiti huu.
Aidha, kamusi ya BAKIZA (2010:208), wamefasili neno kulandana kuwa, linatokana na nomino
landa lenye maana ya kitendo cha kufanana na mtu ama kushabihiana. Landana pia ni kitendo
cha mtu kuwa na sura inayofanana na mwenzake; shabihiana.
Ingawa maelezo ya BAKIZA juu ya neno kulandana hayakuelezwa kwa mkabala wa kifasihi,
hata hivyo, maelezo hayo yalitoa mwanga kwa mtafiti, kuhusu maana halisi ya neno kulandana,
ambapo aliitumia dhana hiyo katika uchambuzi wa data zake.
Wamitila (2002:64), sadifa katika fasihi; kwake yeye, sadifa ni uzuri au ubaya. Sadifa ni utukiaji
wa matukio kwa wakati mmoja na aghalabu kwa namna ya kushangaza inayoashiria bahati.
Umuhimu wa dhana hii unatokana na kujitokeza kwake kwingi katika kazi kadhaa za fasihi ya Kiswahili. Kwa kuanzia ni muhimu kutaja kuwa sadifa hutumiwa kama mbinu au kipengele cha
msuko au kimtindo. Katika baadhi ya tanzu, sadifa ni kipengele muhimu katika muundo wake.
Tuisomapo hadithi ya Jamaadar ya Mui huwa Mwema, yanayaona matumizi ya sadifa kuhusiana
na Kotini na wahusika wengine. Vivyo hivyo katika riwaya za M.S.Abdulla. Katika riwaya za
M.S.Abdulla huwa sadifa jinsi matukio ya wahalifu yanavyokunjuka na hatimaye kufichuka.
Sadifa katika kazi hizi ni kipengele cha lazima.
Maelezo haya ya Wamitila tunaona kuwa yana mnasaba na mshabihiano mkubwa katika mada
yetu ya kuchunguza dhana zilizobebwa na wahusika na zinavyolandana na majina yao, hivyo ni
dhahiri kwamba kupitia maelezo haya tuliyatumia kama dira ya kufikia lengo la utafiti wetu.
Njogu na Chimerah (1999), wameeleza kuhusu suala la sadifa kwa wahusika katika riwaya ya
Siku Njema, ambapo wahusika Bi Rahma kasadifu vyema, Rashid Omar kasadifu na anakufa
lakini kifo chake si cha kifasihi, Zawadi anasadifu kuolewa na Kongowe, mtoto wa miaka kumi
na sita, ilihali yeye ana miaka ishirini na mitatu na akiwa na elimu ya juu. Pia wahusika wengine
waliohakikiwa ni Alice MacDonald, Vumilia Abdalla, Amina na Juma Mukosi.
Ufafanuzi wa huu uliofanywa na Njogu na Chimerah unaonekana kuwiana vyema na mada yetu
hii ya kuchunguza dhana zilizobebwa na wahusika na zinavyolandana na majina yao, hivyo kwa
kuzingatia mbinu hii pia mtafiti alipata msaada mkubwa uliomwezesha kufikia malengo ya
utafiti wake.

(Makala haya yaliandaliwa na Mwalimu Omukabe wa Omukabe wa Chuo Kikuu cha Kenyatta

Idara ya Kiswahili)