Mutahi Kagwe atakiwa kujiuzulu.

Jumamosi,tarehe 29, waziri wa afya ajipata matatani baada ya kutajwa katika kashfa ya shirika la usambazaji dawa la KEMSA.Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo alisema kwenye mahojiano na seneti kuwa Kagwe na karibu mkuu wa utawala wa wizara ya afya,Bi.Susan Mwachache walihusika katika sakata hiyo.Afisa huyo alisema Kagwe ndiye alimlazimisha kutoa tenda kupitia kwa ujumbe wa simu.Alisema waliopatiwa tenda ya kusambaza vifaa vya kujikinga dhidi ya Korona walifuja pesa hizo.

Ikumbukwe kwamba wabunge wanaoegemea upande wa naibu wa rais William Ruto wakiongozwa na mbunge wa Kikuyu,Kimani Ichungwa,wanashikiza Kagwe ajiuzulu mara moja ili kupisha uchunguzi.Mbunge mwingine ni Ayub Savula ambaye alisema Kagwe anafaa kutoka ofisini ili uchunguzi ufanyike wa ubadhirifu wa fedha za Korona.Isitoshe,Seth Panyakoo pia ametaka Rais Kenyatta kumpiga Kagwe kalamu baada ya kuhusishwa katika sakata hiyo.

Magoha asema shule zaweza kufunguliwa hivi Karibuni.

Waziri wa Elimu nchini Kenya amewaambia wazazi wajitayarishe vilivyo kwani shule zaweza kufunguliwa wakati wowote kuanzia sasa.Magoha alisema maambukizi ya virusi tandavu vya Korona vinaonekana kupungua siku chache zilizopita hivyo wanatazamia wiki tatu zijazo kuona kama asimilia itafikia tano.Ikumbukwe shirika la Afya duniani limesema kwamba hatua madhubuti zinafaa kuchukuliwa kuepuka kufungua biashara na jamii kiujumla kiholela.

Magoha aliyezungumza katika taasisi ya elimu ya Wote katika kaunti ya Makueni aliwashutumu vikali wakuu wa taasisi hizo kwa kukosa kupanga mikakati ya haraka ya ufunguzi wa taasisi za juu ya elimu.Ikumbukwe wizara ya elimu iliwasihi wakuu wa vyuo kupanga mikakati kurejelewa kwa mafunzo iwapo maambukizi yatapungua.

Chelsea yamsajili Kai Havertz.

Mashabiki wa klabu ya Chelsea inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza wana kila sababu ya kutabasamu baada ya usajili wa kiungo matata.Kai Havertez ambaye alikuwa mchezaji wa Bayern Leverkusen amedhibitishwa kusajili na ‘the blues”.

Inadaiwa kuwa amekubali mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo.Habari hizi zinatokana na kauli ya Fabrizio Romano kwenye mtandao wa kijamii alipoulizwa na shabiki mmoja kama usajili huo umekamilika.

Usajili huu unakuja siku chache tu baada ya klabu hiyo kuwasajili wachezaji Hakim Ziyech,Timo Werner,Thiago Silva na Malang’ Sarr.

Umuhimu wa Kiswahili.

Kitaifa: Katika kiwango cha kitaifa lugha ya Kiswahili kina majukumu yafuatayo:
 Ni chombo cha mawasiliano katika kiwango cha kitaifa, Kikanda na kimataifa
kama ilivyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika (UA).
 Ni kitambulisho muhimu cha utaifa na uzalendo wetu.
 Ni kitambulisho cha watu wa Afrika Mashariki. Kiswahili ni lugha ya taifa na
vilevile lugha rasmi nchini Kenya na Tanzania.
 Hutumika katika uandishi na uchapishaji. Vitabu vingi vimeaandikwa au
kutafsiriwa kwa Kiswahili, kwa mfano Biblia Takatifu, Daftari la Isimujamii.
 Ni kigezo cha kuchujia wanaojiunga na vitengo mbalimbali nchini. Kufuzu
Kiswahili au Kiingereza na Hisabati kwa gredi fulani ni moja kati ya masharti ya
kujiunga na taasisi mbalimbali nchini.
 Huhifadhi utamaduni na historia ya jamii ya Waswahili.
 Kiswahili kinawaunganisha watu wa kutoka makabila tofautitofauti (45) humu
nchini na Tanzania (makabila 120) na Afrika Mashariki na Kati kwa jumla.
 Ni chombo cha kutolea elimu ambayo ni mhimili wa Ruwaza ya 2030.
 Aidha, ni lugha rasmi, sambamba na Kiingereza, nchini Kenya na Tanzania.
 Hutumika katika sherehe za kitaifa. Viongozi hutumia Kiswahili kutoa hotuba za
kitaifa ili ujumbe uweze kuwafikia wananchi wengi. Wakenya wapatao asilimia
sitini (60%) hawajui wala kuelewa vyema lugha ya Kiingereza. Hii ndiyo sababu
kila baada ya Rais kutoa hotuba yake kwa Kiingereza katika shughuli za kitaifa,
huangazia tena mambo muhimu kwa Kiswahili.
 Ni lugha ya Kiafrika ambayo asili yake ni Afrika Mashariki wala si lugha kutoka
ugenini kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kireno, Kiarabu, Kichina.
 Hutumiwa katika utawala na uongozi. Hutumiwa kuwahamasisha watu.
Kimataifa: Majukumu ya lugha ya Kiswahili ni mengi katika kiwango hiki pia.
 Kiswahili kilikabidhiwa majukumu mengine mapya ya kuwa moja ya lugha za
kuendeshea shughuli za Umoja wa Afrika (UA).
 Ni chombo cha kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki na Kati. (Kinadumisha
utamaduni wa Kiafrika na ni kitambulisho cha watu wa Afrika Mashariki).
 Hutumika kufanya utafiti, kuchungua na kusambaza matokeo. Vyuo vingi duniani
hutumia Kiswahili kufanyia utafiti. Kwa mfano, vyuo vikuu vya Ohio (Marekani),
Mumbai (India), Copenhagen (Denmark), Guttenburg na vingine vingi.

Hutumiwa katika elimu, biashara, sheria/mahakama, dini, utalii, sera, na siasa.
Wana Afrika Mashariki na Kati hutumia Kiswahili kama lugha sambazi.
 Hutumika katika teknolojia ya mawasiliano, yaani, teknohama. Kimeungana na
lugha zingine kuu duniani kama nguzo za utandawazi.
 Hutumiwa kuandika na kutafsiri maandishi na kazi nyingine nyingi za kisanaa.
 Hutumika kama chombo cha ajira. Kwa mfano, katika mashirika ya utangazaji ya
kimataifa kama vile BBC (Shirika la Utangazaji la Uingereza), Deutsche Welle
(Ujerumani) VOA (Voice of America –Sauti ya Amerika), Redio Beijing (Jamhuri
ya Watu wa Uchina), Redio Moscow (Urusi), Iran na kadhalika.
Kuna watu ambao ingawa si Waswahili, hawana lugha nyingine ila Kiswahili. Watu
hawa ni Waarabu wa upwa wa Afrika Mashariki na makabila mengine kama vile Iraqw/
Hadzapi, Wadahalo, Wadigo, Wapokomo, na kadhalika. Aidha, kuna wale ambao
wangali na lugha zao asilia lakini wana ujuzi mkubwa katika Kiswahili kuliko lugha zao.
Ikumbukwe kuwa Kiswahili ndicho lugha yenye asili ya Kiafrika iliyoenea sehemu
kubwa ya Afrika na hata kuvuka mipaka ya bara hili. Kwa sababu ya umuhimu wake,
hamna lugha yoyote ya Kiafrika inayokaribia hadhi ya Kiswahili na kutangazwa katika
idhaa za utangazaji za dunia au kusomeshwa katika vyuo vikuu mbalimbali duniani.(Vitalis Oyoo.2019.Daftari la Isimujamii kwa shule za upili na vyuo)

Lugha ya Kiswahili kama msingi wa elimu.

Kiswahili kinatambulika kama lugha ya Afrika Mashariki. Kwa miaka mingi sasa
imekuwa ikipata hadhi ya lugha ya Kimataifa, licha ya kwmba imekuwa ndio njia
kuu ya mawasiliano baina ya watu wa makabila tofauti. Sifa hizi zote ni ushahidi wa
haraka tu kwamba Kiswahili ni lugha ambayo imeweza kujenga misingi maalum ya
maarifa ya wazungumzaji wake. Hii inatokana na kuwa hizi ni sifa zinazodhihirisha
kuwa Kiswahili kinaweza kuzielezea dhana tofauti za watu wa aina mbalimbali na
zikaeleweka kwa wazungumzaji wengine na hivyo watu kuelewana. Aidha kinaweza
kuchukua dhana za kigeni na kuzielezea kwa wazungumzaji na dhana za
wazungumzaji zikaelezewa kwa wageni na kueleweka na hivyo kuchangia katika
hadhi hiyo ya kimataifa.
Katika upana wake, Kiswahili ndio lugha ambayo tunaitumia katika kila aina ya
shughuli ambayo itatujumuisha sote. Ni pale tu uhusiano unapokuwa wa kikabila,
kikazi (katika maeneo machache) na kielimu (hasa baada ya shule ya msingi)
ambapo Kiswahili hunyimwa nafasi ya kutumika ipasavyo. Athari za kutotumia
Kiswahili katika makundi ya kikabila zinafahamika mojawapo ikiwa ni kuwanyima
taarifa, hekimana maarifa wale ambao sio wazungumzaji wa lugha ya kabila hilo
Hivyo, ni taarifa na mawasiliano kwa wachache na wateule na wasioijua lugha hiyo
hutengwa. Katika maeneo ya kikazi misingi ni hiyohiyo na kwa hali hiyo katika
elimu athari zake za msingi ni hizohizo. Totauti na usiri wa kikabila na kikazi, elimu
ni haki ya wote na huwa wazi kwa kila mwenye kuhitaji kuipata na ambaye yupo
tayri kuipata. Kwa hali hiyo, suala la usiri halistahili kuwepo na ndio maana, kama
tutakavyojadili hapa, ni muhimu elimu itolewe kwa lugha ya Kiswahili, ambayo ndiyo lugha ya wazi kwa wote na ambacho ndicho chombo kinachoweza kutumika
kuufikisha ujumbe, maarifa, ujuzi kwa walengwa ambao ndio hao wazungmzaji.
Lugha ya Kiswahili, ambayo huzungumzwa na idadi kubwa ya watu, ni lugha
ambayo imeshangaza watalamu wengi kuona kuwa haipewi nafasi ya kutumika ili
kuwapatia wazungumzaji wake elimu bora. Wataalamu hao (Khamisi 1980,
Abdullaziz 1980, Mulokozi 1989, Massamba: 1989, Rubagumya (1991)
wameliangana suala la lugha na elimu na kupata data ambazo zimedhihirisha kuwa
sera zetu kuhusu lugha na kuhusu elimu zilikuwa zina mapengo mengi. Hata hivyo
hali sio kwa upande wa Kiswahili tu, bali hili ni suala ambalo limezikumba au
limewahi kuzikumba lugha nyingi duniani na hasa pale watumiaji wake wanapokuwa
na lugha ya kigeni ambayo wanaiheshimu kuwa ni lugha inayohusu elimu. Kama
alivyoelezea Amuzu (1993:105).
Tatizo la lugha ni tatizo ambalo lipo na
ambalolitaendelea kuzaa mijadala mipya
kwa kipindi kirefu.
Maendeleo ya kihistoria na kijamii katika nchi za Afrika Mashariki yamedhihirisha
kuwa utambulisho wa kijamii na mahusiano baina ya watu ambayo yalikuzwa
kutokana na matumizi ya Kiswahili katika upana wake yameendelea kukua na
kuwekewa misisitizo ya ina mbalimbali sehemu na nyakati tofauti. Kwa mfano
wakati Tanzania Kiswahili kimetiliwa mkazo kama somo na lugha ya kufundishia
katika shule za msingi, Kenya Kiswahili kinawekewa mikakati madhubuti katika
kiwango cha Chuo Kikuu. Wakati huohuo, Tanzania ambayo ndiyo yenye idadi
kubwa ya watu ambao lugha yao kuu ni Kiswahili, wanatumia lugha ya Kiingereza kufundishia elimu ya juu. Wanafunzi wengi hawajui lugha ya Kiingereza kwa
kiwango kinacholingana na elimu wanayostahili kuipata.
Tanzania inaandaa wanafunzi wake kwa lugha wanayoielewa hadi wanapomaliza
elimu ya msingi na mra baada ya hapo kuanza tena kuwapa maarifa hayo kwa lugha
wasioielewa. Mchanganyiko huu wnyewe ni kichocheo kikubwa cha kuwachuja na
kuwatenga wale ambao waliweza kuelewa hapo awali. Kwa maana hiyo wanafunzi
bora katika shule za msingi wanajikuta katika hali ngumu zaidi hasa wanapoingia
kidato cha kwanza na kuanza kutumia lugha ya Kiingereza Tatizo kubwa zaidi ni
pale ambapo hata hao walimu ambao kutoa elimu hiyo kwa Kiingereza nao wanalo
tatizo hilohilo la msingi la kutoimudu lugha hiyo.Hii inamaanisha kuwa elimu
inayotolewa sio kamili na huwafikia wanafunzi ambao nao huipokea nusu au chini
ya hapo.

Utandawazishaji wa Kiswahili kupitia simu.

Mojawapo ya matokeo ya utandawazi ni kuwapo kwa simu za kiganjani1 na matumizi yake.
Siku hizi nchini Tanzania mawasiliano ya simu yamekuwako kwa wingi kuliko ilivyokuwa
tangu wakati wa uhuru hadi katikati ya miaka ya tisini. Mahali ambapo hakukuwa na
mawasiliano kabisa, kama sehemu nyingi za vijiji vya Tanzania, siku hizi kuna mawasiliano
kwa njia ya simu hizi za kiganjani na lugha inayotumika katika mawasiliano haya ni
Kiswahili. Lugha ya Kiswahili inayotumika katika simu hizi ni ya kiutandawazi na pengine si
rahisi kuiona nje ya wigo huu wa kiutandawazi ambao pia unajumuisha mawasiliano kwa
barua pepe, na maongezi katika tovuti. Katika lugha hii ya kiutandawazi, watu huwasiliana
kwa kutumiana matini fupi fupi zenye mchanganyiko wa maneno na namba, na hivyo kuunda
lugha tofauti na iliyozoeleka katika jamii nyingine.Mbali na lugha hii katika simu, barua pepe, na Tovuti, Kiswahili kimeshuhudia pia
matumizi ya Sheng hasa miongoni mwa vijana. Lugha hii ipo kwa wingi nchini Kenya
ambapo wataalamu wa isimu na lugha wamekwisha kuiandikia Kamusi (Mbaabu 2003), na
hata makala (Mokaya 2006; Momanyi 2009). Lugha hii pia inatumika hasa katika programu-
pendwa za vijana katika stesheni za radio na TV katika Afrika mashariki. Ingawa lugha kamaSheng imefanyiwa utafiti na imeandikwa, lugha hii ya kiutandawazi inayojichomoza sasa
kupitia katika barua pepe, simu za kiganjani na maongezi katika Tovuti, bado haijavuta – kwa
kiasi kikubwa, shauku ya wataalamu na wapenzi wa lugha hata kuifanyia utafiti. Makala
chache kuhusu suala hili zimeongelea lugha hii katika mawanda tofauti. Kwa mfano, Butts na
Cockburn (2001) wameandika wakitathmini utumaji wa matini (texting) kama mbinu ya
mawasiliano. Waligundua kwamba, utumaji wa matini fupi fupi ni desturi inayokuwa haraka
hasa miongoni mwa vijana. Na kuwa kati ya Januari na Disemba 2000 matini fupi fupi (SMS)
zilizotumwa ziliongezeka kwa haraka kutoka matini bilioni nne na kufikia bilioni kumi na
tano kwa mwezi. Waliona kuwa matini kama hizo zitakuwa zimeongezeka na kuwa bilioni
200 kwa mwaka ifikapo Disemba 2001. Mtaalamu aliyeandika kuhusu aina ya ujumbe na
uundwaji wa lugha mpya ni Crystal (2008a; 2008b). Katika makala yake, aliyoiita Texting
(hapa ninaiita ‘Umatinishaji’), anasema kuwa umatinishaji ni jambo jipya kabisa ambalo sasa
linaelekea kupata lugha yake. Anaelezea kuwa katika umatinishaji, lugha mpya aliyoiita
textspeak inakua kwa haraka hasa miongoni mwa vijana. Makala yake hii ni ya msingi sana
katika mjadala wetu. Hata hivyo, makala ya Crystal iliongelea umatinishaji katika lugha moja
tu ya Kiingereza, na wala haikuonesha athari ya lugha hii “textspeak” au lugha tandawazi
katika nadharia za isimujamii.
Suala kubwa tunalolijadili katika makala hii ni changamoto zinazoletwa na lugha hii katika
Isimujamii, hasa kuchanganya msimbo (lugha) na kubadili misimbo (lugha) (code mixing and
code switching) au kama asemavyo King’ei “kuchanganya ndimi na kubadilisha ndimi”
(2010: 24). Tangu maandishi ya akina Blom na Gumperz (1972), suala hili la kuchanganya
msimbo na kubadili msimbo, limeshughulikiwa sana na wanaisimujamii. Waliolieleza kwa
kina ni pamoja na Labov (1973), Trudgill (2000), Meyerhoff (2006), na Nilep (2006) na hasa
zaidi utafiti na machapisho mbalimbali ya Myers-Scotton (1990, 1993a/1997, 1993b, 1993c,
2002). Hata hivyo, kwa wote hao ukimtoa Crystal (keshatajwa) hakuna aliyeshughulikia kwa
upana lugha ya simu za kiganjani; lugha ambayo hapa tumeiita ‘lugha tandawazi’.
Kwahiyo mwelekeo wa makala hii ni utafiti wa matumizi ya lugha hii tandawazi kwa
kuangalia simu za viganjani na athari yake katika nadharia za isimujamii. Madhumuni yetu ni
kuangalia matumizi ya lugha ya Kiswahili katika simu za viganjani. Kwa vyovyote vile,
matumizi ya Kiswahili cha leo katika simu yanafungua nafasi kwa matumizi ya lugha-pendwa
yanayosababishwa na utandawazi. Je Kiswahili cha kesho, tunaweza kubashiri
kitakavyokuwa na hivyo kukiandaa ili jamii ikipokee na kuendelea kukitumia? Ingawa
Crystal hadhani kuwa lugha hii ya simu itaathiri lugha ya kawaida ya Kiingereza,
inawezekana matokeo yakawa tofauti kwa lugha ya Kiswahili. Tukiangalia nyuma na kuitalii
historia ya makuzi ya lugha ya Kiswahili, tunaona kuwa Waswahili wa miaka iliyopita
walifanya kazi kubwa kukiandaa Kiswahili cha leo. Misingi iliyojengwa miaka ya nyuma
ndiyo iliyosimamisha nguzo za Kiswahili cha leo. Changamoto kubwa katika kukua kwa kasi
kwa lugha inaletwa na sayansi na matumizi ya teknolojia: vipengele viwili vinavyosukumwa
mbele na utandawazi. Kwahiyo, ili kujiandaa na ukuaji huo wa kasi, na ili tuweze kujua mwelekeo wa lugha na kuutawala, hatuna budi kuihakiki ‘lugha tandawazi’ kama hivi
vinavyoibuliwa leo na simu za kiganjani hasa miongoni mwa vijana. Tutafanya hivyo kwa
kuangalia mawasiliano miongoni mwa jamii za Tanzania tukijadili nafasi ya Kiswahili katika
mawasiliano hayo. Aidha tutaibua changamoto katika vipengele vya isimujamii ambapo
katika lugha tandawazi, tunaona upya unaotutaka tuziangalie tena tafsiri na maana ya kubadili
au kuchanganya msimbo.

Utandawazi na mawanda ya matumizi ya simu.

Utandawazi na Mawanda ya matumizi ya simu
Jamii nyingi za Kitanzania kama zilivyo nyingi katika Afrika, bado zinaishi vijijini ambako
hakuna umeme. Aidha katika vijiji kama hivyo, hakukuwa na mawasiliano ya ‘simu za
mezani’. Kwahiyo, ilikuwa haiyumkiniki kuwa na mawasiliano kwa njia rahisi bila kuwepo
kwa miundombinu hasa umeme na simu. Upatikanaji wa simu za viganjani, na kukua kwa
matumizi yake kumeleta mabadiliko makubwa na kurahisisha mawasiliano. Matumizi ya
simu hizi mijini na vijijini ni mojawapo ya matokeo chanya ya utandawazi.
Simu hizi za viganjani zinatumika kwa wingi miongoni mwa wanajamii bila kujali umri,
jinsia, elimu au mahali mtu atokako. Wanajamii hawa huwasiliana kwa hutumia ‘lugha
tandawazi’, yaani lugha ya maandishi iliyochanganywa na namba huku ikifupishwa na
pengine kuchanganywa zaidi ya lugha mbili tofauti. Kutokana na ukweli huu swali letu la
kwanza ni je lugha tandawazi inayotumika katika mawasiliano ya simu inatumiwa na nani
hasa katika jamii? Je inatumiwa na wote (kama walivyotajwa hapa juu) au matumizi yake
yanajipambanua kutokana na umri, jinsia, elimu au mahali pa watumiaji? Swali jingine ni je,
tunaweza kuwa na sheria za lugha hii katika mawasiliano? Je mawasiliano haya yanaingia
katika mundo wa isimujamii uliokwisha kuwapo au yanaanzisha muundo mpya? Maswali
yote haya yanahitaji utafiti wa kina wa uwandani ili kuweza kujibiwa kiuyakinifu; makala hii
ni ya kiuchokozi kuanzisha mjadala kama huo.
Utafiti wa awali wa watumiaji wa lugha tandawazi kwa jiji la Dar es Salaam (Mutembei
2010), ulihusisha vijana wenye umri wa kati ya miaka 14 na 18 toka shule za Jangwani,
Azania, Tambaza, Makongo, Jitegemee na Mbezi. Mawasiliano ya vijana hao wa shule
yalilinganishwa na mawasiliano ya wafanyakazi wenye umri kati ya miaka 40 na 55 ambao
walichaguliwa toka Ofisi mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ardhi,
Chuo Kikuu kishiriki cha Chang’ombe na Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba – Muhimbili.
Sehemu zote mbili, ile ya shuleni na ile ya Vyuoni zilifanana kwa kuwa zote ni sehemu za
utoaji elimu. Wote walichukuliwa kuwa ni watu wenye uelewa na wanajitahidi kwenda na
wakati wakiathiriwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Katika utafiti huo, tuligundua kuwa wengi wa watumaji wa lugha tandawazi ni vijana
kutoka shule za sekondari. Katika jumla ya vijana 60 ambao walikubali kutupatia
mawasiliano mbalimbali waliyoyafanya na vijana wenzao, ni kijana 1 tu ambaye hakuwa na
wingi wa mchanganyiko wa namba, maneno, ufupishaji na mchanganyiko wa lugha mbili hasa za namba. Na kati ya wafanyakazi 60 ambao walikubali mawasiliano yao yaangaliwe
kama data ya utafiti, ni 4 tu ambao walikuwa wamechanganya namba, maneno na ufupishaji,
lakini hata hawa hawakuchanganya lugha mbili.
Bila shaka utafiti kama huo ukiweza kufanyika ukihusisha watu wengi zaidi na wa kada
mbalimbali unaweza kutupa majibu sio tu kuhusiana na vipengele vya isimujamii, bali hata
athari za lugha tandawazi hasa kwa mustakabali wa lugha ya Kiswahili. Ni kweli kwamba
kuenea kwa simu mahali pengi na kuongezeka kwa matumizi yake kumerahisisha sana
mawasiliano. Aidha ni kweli kuwa matumizi hayo yanakuza Kiswahili – lugha inayotumika
katika mawasiliano hayo. Tukiukubali ukweli huu, hatuna budi pia kuuangalia ukweli
mwingine unaojitokeza. Matumizi ya lugha tandawazi kwa njia ya simu na barua pepe
yanaweza kuwa na athari kubwa katika lugha ya Kiswahili nje ya miktadha ya mawasiliano
haya ya simu na barua pepe. Kabla hatujaangalia athari za lugha tandawazi nje ya wigo wa
simu na barua pepe, napendekeza tukubaliane kuhusu muundo wa mabadiliko ya kiisimujamii
katika lugha.
(Makala haya ni kwa hisani ya Prof.Aldin Mutembei)