Msipachike wa shuleni.

Mimba zimezua hofu,kotekote tu nchini
Mewaponza wadhaifu,kutorudi mashuleni
Wamepata usumbufu,kwao kukaa nyumbani
Himili si ulemavu,wapewe nafasi shule

Wenye hamu nakashifu,wote tena hadharani
Kupachika ni halifu,utaozea jelani
Nyi mnao upungufu,mwapachika wa shuleni
Wana wangali wadogo,sheria ifanye kazi

Nyinyi mna hitilafu,chuzi mwamwaga mwilini
Naomba mniarifu,mbona wengi mnazini
Mnao uharibifu,wana wako balaani
Tusimameni Kidete,tukashifu hayawani

Waumini wadilifu,kokote kenya nchini
Tumuombeni latifu,tusikome asilani
Aondoe hitilafu,wana pate afueni
Injili tuenezeni,wana wapate wosia

Mola wetu mtukufu,wasichana hatarini
Acha ‘mi nikuarifu,uwatoe matatani
Wondolee babaifu,waeze toka tabani
Mola wetu saidia,wanao wawe pazuri

Nanyi waja waongofu,roho zenu matatani
Mbona hamuwaarifu,mafundisho kuwapeni
Mwajitia takatifu, usokitu kitwani
Tuwape mema malezi,nasaha pia muhimu

(Malenga ni Agadias Ikoha)

Ndoto imejitabiri.

Ndoto imejitabiri
mahaba yamenikola,mwenzenu sifurukuti,
sikwa kunywa wala kula,na ucheshi wake sweety
roho safi hana ila,si wa wingi ati ati,
Ndoto imejitabiri,yamiaka na mikaka,

mahaba nikikohozi,na ua lenye thamani,
ajuae mana penzi,hisia huzithamini,
kumkosa mi siwezi,hata nikapewa nini,
Imetimu yangu ndoto,yamiaka na mikaka

pazidipo hali ngumu,ndo mazuri hutokea,
utajua yupi humu,alo mwema na mbea,
dhiki ya chungu nitamu,pesa huba ndo dunia
ndoto imejitabiri,yamiaka na mikaka,

Alo penda mempenda,na ndoani kamueka
Alo nitenda mekwenda,kaniachia baraka,
za mwengine kumpenda,kwa furaha na kucheka,
Ndoto imejitabiri,ya miaka na mikaka,

Lipa mabaya kwa mema,ndilo mama kanambia,
si wazuri wanadama,bure watakuchukia,
moyo nao sio chuma,sipende yakusikia,
imetimu yangu ndoto,ya miaka na mikaka,

Japo na ishi kutapa, nakushukuru karima,
hadi kufikia hapa,kuna mengi meyasoma,
siweke roho ya pupa,maisha yatakukwama,
imejitabiri ndoto,ya miaka na mikaka,

Nafunga wangu uneni,beti saba zatoshea,
simba narudi porini,pale baba metokea,
nlipo kosa samahani,tungoni sijabobea,
Imetimu yangu ndoto,kwa mapenzi yake mola

(Malenga ni Simba Mtoto)

Naomba suluhisho.

NAOMBA SULUHISHO
Mawazo jama mawazo, natambua chanzo chake
Huletwa na matatizo, kila mja ana yake
Mengine ni ya mizozo, furahayo yakupoke
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Mawazo huwa mazito, akili kuizuzua
Huleta kivangaito, lakufanya kutojua
Tumbo likawaka moto, na moyo ukaungua
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Hutia wengi vidonda, na kuchomeka moyoni
Kufanya wengi kukonda, waishie kaburini
Hasa yale ya kupenda, wengi wapo taabani
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Na mawazo ya maisha, ni wengi yamewatesa
Madhila yasiyoisha, yasopigika misasa
Kisha njaa huwatisha, tatizo hawana pesa
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Kuna yale ya kuatwa, matozi yabubujike
Na yakuumishe kitwa, mwendanio umzike
Mtima utaburutwa, ulie usononeke
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Mengine ni ya elimu, haswa kwa watahiniwa
Mitihani ni migumu, maishani wangojewa
Hutaki kujilaumu, cheti chako ukipewa
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Wengi sana hujiuwa, tamaa ikikatika
Sumu kule ikanywewa, uhai wakajipoka
Na vitanzi vikatiwa, mawazoni kupatoka
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo

Na mawazo huchakaza, na uso ukanyauka
Makunyanzi kuyajaza,surayo ikapauka
Huwezi kuyapuuza, mana moyo wachomeka
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Niishije.

NIISHIJE
Naja kwenu kwa heshima, salamu zipokeeni
Sitowapita daima, bila kuwapungieni
Nauliza kwa tadhima, mnijuze ihiwani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Nawaomba nijuzeni, m’menishinda jamani
Nikitenda ihisani, mwanilipa nukusani
Wema hamuuthamini, chokochoko ni za nini
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Nikikaanga omena, kapata mada jirani
Sasa nami nyama sina, wataka nipike nini
Hajanipa Subuhana, wanichunguzia nini
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Nikipata cha jioni, wauliza kala nini
Nikienda msalani, chooche ki rangi gani
Kwani wanitakiani, kujuwa ya kwangu ndani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Nikipika za majani, mchicha sukumawiki
Mboga zake ni majani, aliwapeza samaki
Yule hana na hanani, kwake nyumbani sifiki
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Yakwenu yamewashinda, ya kwangu mwayatakani
Vijiweni mwaniponda, sina kitu mfukoni
Wanafiki m’mewanda, umbea uso kifani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Maswali mwaulizana, yule ataoa lini
Amepita usichana, ataolewa na nani
Hata sura yeye hana, mwamkufuru Manani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Ukishika zako njia, ana maringo fulani
Huenda amefulia, kajifungia nyumbani
Pema ukiangukia, anaabudu shetwani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Kinalika shughulini, wajanicheka jirani
Kidhera ni cha zamani, ana majacha guuni
Kishati chake fulani, kilitoka mfukoni
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Nawaaga kwaherini, nawaachia maswali
Mwenzenu niambieni, ‘sinyamaze kulihali
Menzamwenye ndo nyumbani, jina langu Danieli
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

(Daniel Wambua ndiye malenga wa shairi hili)

Umeshinda.

UMENISHINDA
Moyo unanipa tabu, husikii ‘ngakwambiya
Sijui utajitibu, matungu yangafikiya
Nawaza kukuadhibu, moyo ‘ningakufikiya
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Mshawishi wako mato, sifiti akutongeya
Likikupata fukuto, kamwe hatokaribiya
Yakikufika majuto, yeye atakimbiya
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Mato hayana paziya, yapepesa huku kule
Kwa haraka yakimbiya, uendako yapo mbele
Mabaya hukwegesheya, yateke ‘kipata ndwele
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Nakurai nisikiya, kwani huwezi tuliya
Pondo sitokutiliya, motoni ‘kitumbukiya
Yakikudirika haya, matozi utajiliya
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Mato haya hukumbonya, na weye ukapendezwa
Kisha ukajibambanya, hapo akili hubezwa
Wakanyi wangakukanya, nao hapo wangapuzwa
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Ulimi ukajongeya, matamu kukuteteya
Mahaba kukutakiya, chumvi utakutiliya
Tena utakusifiya, hisia kukutekeya
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Kiziwi hunisikii, sauti ‘ngakupaziya
Yani katu hunitii, upendako wajendeya
Tatizo hufikirii, litakalokutokeya
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika

Dunia itakufunda, nakwatiya ulimwengu
Mwanzoni nilikupenda, ‘kasaliti pendo langu
Moyo we’ umenishinda, nipunguziya matungu
Yamekushinda ya damu, mengineyo wajitwika.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Tusikufuru Muumba.

TUSIKUFURU MUUMBA

Mungu ndiye nguvu yetu, mchunga wa sisi sote,
Kubagua hathubutu, ila atupenda sote,
Kaumba vitu na watu, twafanana sisi sote,
Tusikufuru muumba, kwa kufisha mahuluku.

Liwafikie muliko, mswahili nawasihi,
Yasitufike mauko, kwa mambo yaso sahihi,
Siasa ya masumbuko, itatung’oa wajihi,
Tusikufuru muumba, kwa kufisha mahuluku.

Ninawasihi vigogo, bwana Ruto na Raila,
Hata na wale wadogo, kwenye siasa za hila,
Tusivunjike magego, hini ndiyo yangu sala,
Tusikufuru muumba, kwa kufisha mahuluku.

Amani kigezo chetu, si lazima kulipia,
Ubinadamu ndo wetu, anavyopenda Jalia,
Huu ndio wito wetu, viongozi na raia,
Tusikufuru muumba, kwa kufisha mahuluku.

(Malenga ni Toney Francis Ondelo).

Pera limeiva .

*PERA LIMEIVA.*
Ni vipi nitasombera,mti ule wa jirani,
Kulichuma nalo pera,ambalo nalitamani,
Pera kubwa ja mpira,lanivutia usoni,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Natamani kulichuma,lazidi kunivutiya,
Ni nani nitamtuma,aweze kunileteya,
Mbona nijishike tama?Pera nikiliwaziya,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Kila siku naliona,lanifanya kufikiri,
Nami melipenda sana,kulila niko tayari,
Wallahi nitakazana,nilichume kwa kiburi,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Kwa jirani kuna kuta,vipi nitalifikia,
Natamani kulipata,ningali mwenye tamaa,
Nikipata sitajuta,bali nitafurahia,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Kwa muda najilaumu,mbona sina mikakati,
Tajikaza ilhamu,sitaki tena kuketi,
Kwa hivyo tanilazimu,nisipoteze wakati,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Jirani naye mkali,hataki kunisikia,
Vyovyote kwa kila hali,nitazidi kumwambia,
Heri ajue ukweli,kuliko kumuibia,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Jambo lipi nitafanya,na pera laniduwaza,
Mwenyewe amenionya,sitaki kumchokoza,
Na tayari ashamanya,sababu nimemweleza,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Tamati sasa natua,itabidi kutulia,
Kwa sasa nimeamua,kuweza kumsikia,
Bure nitajililia,mwishowe nitaumia,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

(Malenga Kitongojini)

Kumbuka mwanadamu.

KUMBUKA MWANADAMU
Hakika ya mwanadamu, utambaye ardhini
Ulosahau Rahimu, wajitapa duniani
Rabana humheshimu, wajigamba kwa mapeni
Miliki hata bahari, makaziyo mwanandani

Kusali huna wakati, Mola wako humtaki
Shetwani kakuthibiti, kwake gizani hutoki
Umebebwa hatihati, mwanadamu huzinduki
Uliumbwa mwanadamu, umsujudie Allah

Umejawa na kiburi, hukumbuki jehanamu
Waabudu utajiri, pesa kwako ndo muhimu
Wamkufuru Kahari, kiama hukifahamu
Ewe mja nakusihi, mtubie Mola wako

Ujana umekuteka, ardhini una ndweo
Anasa ziso mipaka, midundo ya mamboleo
Wapata unachotaka, ila huna mwelekeo
Kuna kifo mwanadamu, na hutoishi dahari

Mbona tusijiandae, kwa maisha ya keshoni
Anasa tuzikatae, tukapenyezwe peponi
Umepata upendae, wasahau kaburini
Tuishipo duniani, tukumbuke kaburini

Rohoyo itolewapo, uchungu uso kifani
Uwapendao hawapo, na hawatakuauni
Muda wako ufikapo, ukatiwe kaburini
Adhabu ya mle ndani, mwenzangu hutoiweza

Kuna nyoka anauma, mfano wake hakuna
Kila swala ‘takuuma, si usiku si mchana
Giza litakuandama, usaidizi hakuna
Adhabu hino jamani, kuiepuka ni swala

Kuna rungu kubwa sana, malaika wasubiri
Dhambi zako ewe mwana, azinakili Nakiri
Hutoikumbuka jana, ujibupo Munikari
Maswali haya wenzangu, ni mazito tena sana

Hivi nani Mola wako, utashindwa kulijibu
Na ni ipi dini yako, utamani uwe bubu
Subiri hukumu yako, litakuliza muhibu
Hino dunia si yetu, tujiandae ahera.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Sichoke.

USICHOKE
Mie jogoo la shamba, siwezi wika mjini
Nisichanike misamba, bora nibaki nyumbani
Kule mwana sitotamba, matungu yawe moyoni
Ewe akili fikiri, fikiri maisha yangu

Ewe akili fikiri, fikiri maisha yangu
Kesho yangu itabiri, yawate ya walimwengu
Usijeinywa shubiri, dunia ikawa tungu
Miguu nawe tembea, safari bado ni ndefu

Miguu nawe tembea, safari bado ni ndefu
Kamwe usijezembea, wakakuona dhaifu
Mwenzio nakuombea, atakujibu Raufu
Weye chapa zako lapa, karambukia maisha

Weye chapa zako lapa, karambukia maisha
Ila usiwe na pupa, hadhiyo ukajishusha
Ukibwagwa na wa hapa, wakule watakuvusha
Jikaze mwana jikaze, maisha si lelemama

Jikaze mwana jikaze, maisha si lelemama
Kujiuwa usiwaze, hata utakapokwama
Mawazo mawi yapuze, pambania mwisho mwema
Fahamu lolote jema, halikosi maumivu

Fahamu lolote jema, halikosi maumivu
Ushauri wake mama, mwana nisiwe mvivu
Punje ile ya mtama, yahitaji ukomavu
Leo zikubali dhiki, kesho utafarijika

Leo zikubali dhiki, kesho utafarijika
Zingatia itifaki, nawe huko utatoka
Zidi kusaka riziki, na kamwe usijechoka
Hawawezi kuiziba, pengine kucheleweshwa

Hawawezi kuiziba, pengine kucheleweshwa
Kumbuka haba na haba, mwishoni huunganishwa
Zikakijaza kibaba, na sifa kikabebeshwa
Mgaa gaa na upwa, hawezi kula mkavu

(Malenga ni Daniel Wambua).

Sichoke.

USICHOKE
Mie jogoo la shamba, siwezi wika mjini
Nisichanike misamba, bora nibaki nyumbani
Kule mwana sitotamba, matungu yawe moyoni
Ewe akili fikiri, fikiri maisha yangu

Ewe akili fikiri, fikiri maisha yangu
Kesho yangu itabiri, yawate ya walimwengu
Usijeinywa shubiri, dunia ikawa tungu
Miguu nawe tembea, safari bado ni ndefu

Miguu nawe tembea, safari bado ni ndefu
Kamwe usijezembea, wakakuona dhaifu
Mwenzio nakuombea, atakujibu Raufu
Weye chapa zako lapa, karambukia maisha

Weye chapa zako lapa, karambukia maisha
Ila usiwe na pupa, hadhiyo ukajishusha
Ukibwagwa na wa hapa, wakule watakuvusha
Jikaze mwana jikaze, maisha si lelemama

Jikaze mwana jikaze, maisha si lelemama
Kujiuwa usiwaze, hata utakapokwama
Mawazo mawi yapuze, pambania mwisho mwema
Fahamu lolote jema, halikosi maumivu

Fahamu lolote jema, halikosi maumivu
Ushauri wake mama, mwana nisiwe mvivu
Punje ile ya mtama, yahitaji ukomavu
Leo zikubali dhiki, kesho utafarijika

Leo zikubali dhiki, kesho utafarijika
Zingatia itifaki, nawe huko utatoka
Zidi kusaka riziki, na kamwe usijechoka
Hawawezi kuiziba, pengine kucheleweshwa

Hawawezi kuiziba, pengine kucheleweshwa
Kumbuka haba na haba, mwishoni huunganishwa
Zikakijaza kibaba, na sifa kikabebeshwa
Mgaa gaa na upwa, hawezi kula mkavu

(Malenga ni Daniel Wambua).