Miezi tisa baadaye.

Umbali tuloutoka,ni neema zake Bwana,
Ndiyo maana nataka,shuhuda ana kwa ana,
Usiwahi kunicheka, labda tulipokezana,
Masikio uyatege,kigoda ukikalia.

Imekuwa unoita,miezi ile ya mwambo,
Fedha nazo kuzipata,limekuwa gumu jambo,
Uchumi umezorota, biashara kwenda kombo.
Hatima yake ni njaa, umaskini na ukame.

Mauko yalokithiri, ‘masonko’ kwa mahawinde,
Yameshiba makaburi,wafu wakawa washinde,
Haya yote siyo siri, wala siyo peremende,
Wakwetu walotuaga, tukabaki kinywa wazi.

Wanaetu waliimba,wimbo usio mzuri,
Wakaweza pata mimba, ambazo zimewathiri,
Wazazi na wakagomba, hawakuata kiburi,
Magonjwa wakapokea, ukimwi hata zinaa.

Nitaikosa nidhamu, sipotaja mtalaa,
Sitaki kuwa hakimu,jionee ‘navyokaa,
Kila mara wana simu, wakitazama balaa,
Akili wamekanganya,wakadhani ni wazima.

Dawa zinazolewesha,ndiyo yao silabasi,
‘meweza wakutanisha,na kuwafanya wambasi,
Bangi wakaimarisha, matokeo ni uasi,
Walimu tunayo kazi, sote tuvalie njuga.

Ni vema tujukumike,tulio washikadau,
siwaache wateseke,tusiweze wasahau,
Ushauri ziboreke, wavyele kwa kina hau,
‘stakabali wa taifa, hutegemea vijana.

Kwa hivyo miezi tisa, mesheheni changamoto,
Tuweze kusali hasa! Na kupanga zetu ndoto,
Aweze kupatakasa, mwakani kwa manukato,
*Mafundi zangu wa* *nguo,mpunguze futi yangu.*

(Malenga ni Elisha Otoyi)

Wanafunzi likizoni.

Ni mwalimu Khamicyzo, mtoa nasaha sasa /
Wanafunzi mu likizo, umakini wawapasa /
Msije pata tatizo, majutoni mkanasa /
Wanafunzi likizoni, mwalijua lengo lake ////
*
Msishinde vijiweni, na pulei sitesheni /
Bora mkae nyumbani, muitwe wa kizamani /
Kuliko ulimbukeni, mkamezwa na fasheni /
Wanafunzi likizoni, mwalijua lengo lake ////
*
Asubuhi ikifika, begi kwenda tuisheni /
Maji mwakataa teka, vipindi sikupiteni /
Kukosha vyombo mwang’aka, atakucheka fulani /
Wanafunzi likizoni, mwalijua lengo lake ////
*
Wazazi pia walezi, wenenu wapo ma kwenu /
Oneni ilivyo kazi, kulea visukununu /
Waweza pata uchizi, leeni hawa wenenu /
Wanafunzi likizoni, mwalijua lengo lake ////
*
Wazazi walalamike, mwawatesa likizoni /
Wataka wanufaike, uweponu majumbani /
Badalaye sekeseke, kwa mambo yaso thamani /
Wanafunzi likizoni, mwalijua lengo lake ////
*
Likizo yaenda mwisho, kipi mlichokivuna /
Maisha leo na kesho, mwaenda kuwa vijana /
Msije kuwa michosho, jamii ikawakana /
Vipi ya kwenu malengo, mlejeapo shuleni /

(Malenga ni Bin Omary)

Vikwazo vya maenezi ya Kiswahili katika enzi ya ukoloni.

Ingawa lugha ya Kiswahili ilienea sana, lakini kulibainika vilivile vikwazo vilivyo
tatiza maenezi yake, Japo Kiswahili kilikuwa kimeenea mataifa mengi Afrika
Mashariki lakini kuna vikwazo vingi vilivyoifanya lugha hii kutopiga hatua kwa
mataifa mengineo ya Afrika na lau sivikwazo hivyo Kiswahili kungekuwa lugha
ya mataifa mengi ya bara Afrika, miongoni mwa sababu hizo:
1- Dharau za Wazungu kwa Waafrika
Mfumo wa utawala wa Wazungu na Waingereza, ulileta pingamizi kubwa katika
maenezi ya Kiswahili. Waingereza waliwadharau sana Waafrika na mambo yao
yote kukiwemo lugha zao. Kiswahili kama mojawapo ya Lugha za Kiafrika
haingeweza kuepuka dharau hizo.
Kwa upande mwengine Wakoloni walichukulia kuwa lugha yao ya Kiengreza ni
adhimu na yenye manufaa kuliko lugha yeyote, na mwenye kutaka ustaarabu
lazima ajifunze Kiingereza, waliweza kukuza lumbikizo hizo kwa kupitia mashule
walioazisha na nafasi za kazi ambazo waliwapa kipawa mbele wanaojuwa Kiingereza, pia waliweka mawazo kwenye akili za watu kuwa Kiswahili hakitoshi
kunfanya mtu astaarabike.
Kwa sababu hizo za chuki Waaingereza walianzisha lugha rasmi za matumizi kwa
Mwafrika, hivyo basi Kiingereza kikapawa hadhi kubwa na ya juu kufanywa
lugha rasmi kisha Kiswahili. Hapo basi Kiingereza kikawa ndio lugha ya
Ustaarabu na yeyote aliyetaka kustaarabika alijifunza Kiingereza.
Kuna fikra mbaya zaidi iliyoenezwa na Wazungu hao, nao nikuwa Kiswahili
hakina misamiati yakuendesha shughuli za kielimu na taaluma isipokuwa
Kiingereza kwa maoni yao Waafrika ni watu washenzi na washamba.
Mawazo hayo yaaliwaathiri sana wenyeji na wengi wakaanza kuutoroka Uafrika
tamaduni na hata lugha, na wengi wakaanza kutafuta ustaarabu katika lugha za
kigeni. Kwa mfano Kenya na Uganda, kuna baadhi ya viongozi hadi leo waamini
kuwa kiingreza ni bora kuliko Kiswahili na lugha nyengine za Afrika.
2- Kiswahili ni lugha geni.
Kuna baadhi ya watu walidai kuwa Kiswahili ni lugha geni yaani ni Kiarabu,
nahivyo basi kilikuwa hakina nafasi hapa Africa Mashariki na yakati. Hivyo basi
wakaonelea ni heri wajifunze lugha za kienyeji badali ya Kiarabu, tume ya Philips
stoke ya 1924, nchini Kenya ilipendekeza matumizi ya lugha ya Kikamba, Kijaluo,
Kikikuyu, na Kiluhya, nchini Uganda walipendekeza Kiingereza na Luganda,
katika maeneo ya kifalme na hata maeneo yasiokuwa ya kimalme, nchini Zaire
Waluba, Wakongo na Walingala walikataa katakata kusanifishwa kwa Kiswahili
cha Kiungwana kwa sababu walidai kuwa ni lugha geni ya Afrika Mashariki na
basi haina nafasi Zaire ndiposa Kifaransa kikaendelezwa na Wabelgiji.
3- Dhana kwambaKiswahili kiliendeleza Uislamu.
Nao Wamishonari hawakukipenda Kiswahili kwa madai yakuwa Kiswahili
chaendelza Uislamu ilihali wao walitaka kuendeleza Ukiristo, hali hiyo
iliwapelekea kukusanifisha Kiswahili wakidai kuwa walikuwa wakiondoa Uarabu
na Uislamu katika Kiswahili, pia walidai wataka kukipa chombo cha kueneza dini
ya Ukiristi nidhamu, haya yote yalifanywa na Wameshinari wakishirikiana na Wazungu kwakutambua hakuna lugha nyengine yaweza tumiwa kwa mambo ya
Mungu isipokuwa Kiswahili.
Kwa mtazamo wa makini twaweza sema lau Wakoloni na Wamishonari
wangekuwa na lugha mbadala kuliko Kiswahili basi wamgetumia lugha hiyo na
wangeiacha lugha ya Kiswahili, lakini kwa kuwa ingekuwa gharama kufasiri
baadhi ya vitabu vyao kama Biblia katika lugha nyengine za Kiafrika basi
waliazimia kutumia Kiswahili, nchini Uganda na Kenya kuna tume ziliochaguliwa
kuchunguza matumizi ya Kiswahili kwakuwa lugha hii imekabiliana na Uislamu.
4- Biashara.
Kwa jumla biashara ni miongoni mwa viekezo vikuu vilivyoifanya lugha ya
Kiswahili kuenea Afrika Mashariki, ingawa hivyo biashara hii ilitumiwa na
Wakoloni kuifanya lugha ya Kiswahili kuchukiwa na kuonekana lugha mbaya.
Waingereza walieneza propaganda kuwa Kiswahili na wanaotumia Kiswahili
wamefungamana na biashara ya watumwa, nayo fikira ikaeneya kwa jamii kwani
biashara ya watumwa ilikuwa ni biashara mbaya na yeyote aliyetoka maeneo ya
bara alimchukia mwenye kufanya biashara hiyo nakumuona adui, kwahivyo
Kiswahili kikachukiwa na Waswahili wenyewe wakachukiwa kwa kuhusishwa na
biashara ambazo hazikuwa za kweli.
Kawaida biashara siku zote huhusishwa na porojo na ukora na ujanja mwingi, basi
ikawa lugha ya Kiswahili ni lugha ya wakora na wajanja wenye kufanya biashra za
watumwa, kwa sababu hizo lugha hii ikawa wengi katika wageni hasa wasiotoka
maeneo ya mwambao waichukia.

(Makala haya ni kwa hisani ya DR.K.M Kame)

Nifunzeni umalenga.

Nifundisheni kutunga, na kughani mashairi / Nisiwe wa kubananga, kila tungo ni sifuri / Kwa vina kuungaunga, mizani nazo bahari / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni //// *

Niishikapo kalamu, niandike kwa bidii / Niandike tungo tamu, za kuijenga jamii / Nitoe kubwa elimu, upatikane utii / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni ///

* Niwe na sauti nzuri, ya kukonga halaiki / Niwe mlumbi mzuri, bila hata ya maiki / Niziepuke dosari, nighanipo pigwe tiki / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni ////

* Nifundisheni nudhumu, kuanzia na chimbuko / Nitunge vyenye muhimu, nichunge yetu miiko / Nifumeni kwa taimu, niupate muamko / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni //// *

Nisipate hadaiko, kwa laiki na komenti / Kwa kuvitunga vituko, mithili yake matenti / Nigawieni zinduko, nifuzu niwe ajenti / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni

Ombi langu kwa wakunga, mnapaswa nitibie / Vyema muweze nijenga, katu msinikimbie / Nami niwe mwenye vanga, hadhira initambue / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni ////

Nimefika kaditama, mswada mewakilisha / Nangoja mshindo nyuma, ujumbe meufikisha / Khamicyzo nasimama, peni nayo imeisha / Nahitaji kuwa manju, wanafuu nifunzeni ////

(Malenga ni Bin Omary)

Matatizo yanayoikumba lugha ya Kiswahili.

Licha ya kuwa lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa bado kuna changamoto si haba katika kuikuza.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na yafuatayo.

Kwanza,lugha hii imepata upinzani mkubwa kutoka kwa lugha nyingine kama vile Kiingereza, Kifaransa,Kijerumani, Kiarabu n.k

Pili,kuna dhana kuwa Kiswahili ni lugha ya watu duni hivyo kutengwa katika matumizi katika nyanja mbalimbali.

Tatu,pana ukosefu wa sera maalum ya matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nchi kadhaa kama vile Kenya.

Nne,kuna ukosefu wa walimu wa wakutosha wakufunza lugha ya Kiswahili waliohitimu.

Aidha,kuna kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha za kigeni.

Walaji viporo.

Wale wapasha viporo, tabia hiyo acheni /
Mwaileta migogoro, hata haya hamuoni /
Na zote zake kasoro, mnatupia kinywani /
Viporo vina madhara, bure mwazichuma dhambi ////
*
Chakula umeshapika, kizuri tena cha moto /
Waanza kuyayatika, na kiporo kiso joto /
Sijui kipi wataka, zote hizi changamoto /
Viporo vina madhara, hata viliwe kwa ndimu ////
*
Waona unafaidi, ukila kwa kujificha /
Wafurahi maridadi, hukiogopi kuchacha /
Wakiona ni sitadi, ingali ulikiwacha /
Kiporo kina madhara, hata ukile gizani ////
*
Ulikiacha mwanzoni, ukenda pata cha moto /
Wakikumbukia nini, kiporo na hili joto /
Sendekeze fuadani, takuletea mazito /
Kiporo kina madhara, hata ukipashe moto ////
*
Kula hicho kilo moto, fureshi ulochagua /
Ukakiona fumbato, ndani ukenda kitia /
Yasikuhadae mato, kiporo kukumbushia /
Kiporo kina madhara, duniani na mbinguni ////
*
Uchumi unadorora, wahudumia viporo /
Nyumbani watia fora, huachi toa kasoro /
Wakacha maisha bora, menogewa na viporo /
Viporo vina madhara, hata ule kwa upole ////
*
Viporo vina madhara, akhera na duniani /
Vyaweza kupa kuhara, gonjwa la kinywa na chini /
Afyayo kudorora, ukabaki majutoni /
Viporo vina madhara, ukinaswa utajua ////
*
Hukilagi peke yako, wewe ulaye kiporo /
Jua yupo na mwenzako, nyote mwapigishwa doro /
Wewe watoa mshiko, yule juu ya godoro /
Viporo vina madhara, risechi yatuambia ////
*
Sicho cha halali kwako, wakila kwa kichochoro /
Huthamini afya yako, wauthamini mchoro /
Kutimiza haja zako, njaa gani ya kiporo /
Kiporo kina madhara, hata kifishwe uturi ////
*
Haimpendezi Mola, kurudia matapishi /
Waona raha kukila, waendelea kuishi /
Ipo siku atafula, kuujutia utashi /
Viporo vina madhara, havifai kurudiwa ////
*
Apime ayapimae, masafa niambaaye /
Kupinga anipingae, kiporo akisifiye /
Uzuriwe atugee, kiporo abugiaye /
Kiporo kina madhara, hata kiwe na chachandu ////

(Malenga ni Bin Omary)

Nitetee Mola Wangu.

Tenzi :: Nitetee Mola Wangu

1 Nitetee Mola wangu
Wewe kimbilio langu
Duniani sina changu

2 Hali yangu vangu vangu
Nikulacho ni kichungu
Nimejawa naukungu

3 Siku ya tatu sijala
Na bado ni masajala
Nakesha kwenye jalala

4 Kuyaokota makopo
Ningeupata mkopo
Au ja kazi ya popo

5 Maisha yangu ni duni
Sina kitu mfukoni
Uzito upo kitwani

6 Muda wote ni majozi
Nacheka yaja machozi
Vitamu kwangu ni njozi

7 Njoo wangu muokozi
Nsije fanya udokozi
Kifo kiwe yangu dozi

(Malenga ni Abuuadillah)

Ngojera.

NGUO

*BABA*
1.Songea hapa mwanangu,,nikwambie tu dhahiri
Nguo zako za kizungu,,zamuudhi na kahari
Zatia ladha uchungu,,mwili wako husitiri
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
2.Baba wajuwa nijoto,,kipindi cha jua kali
Ninaupata msoto,,Nikivaa bulibuli
Bora nivae kiputo,,kimini na suruwali
*NGUO NDEFU SIZIWEZI,,NAKUWA KAMA MZEE*

*BABA*
3.Hali ngii akilini,,mwanangu unalosema
Mafunzo yetu ya dini,,wazi wazi mwayagoma
Munafata ya mijini,,yakidini mwayatema
*NGUO ZA MAPATA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
4.Baba dini kitu gani,,mbona na umekazana
Kwani dini si imani,,moyoni kutulizana
Vipi kwa nguo jamani,,nawe una gubusana
*NGUO NDEFU SIWEZI,,NAKUWA KAMA MZEE*

*BABA*
5.Ametufunza mtume,,sitara kuzingatia
Wote wake na waume,,lazima kuyafatia
Kheri ukweli niseme,,atanilipa jalia
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
6.Wapo wanao zivaa,,baba si tuna wajua
Na bado Wana adaa,,Wana tanga na dunia
Tena ninawashangaa,,nadini wanaijua
*HERI NI YAKWANGU MIMI,,SITARA NISOIVAA*

*BABA*
7.Wala hauna ta heri,,unajijaza madhambi
Wazikosa na mahari,,za wale wakuja chumbi
Chakula kilo kizuri,,sikile chenye mavumbi
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
8.Baba Mimi ni mrembo,,na tena ninavutia
Nina uzuri wa umbo,,na hata wa sura pia
Wale watakao chimbo,,watakuja nichumbia
*NGUO NDEFU SIZIWEZI,,NAKUWA KAMA MZEE*

*BABA*
9.Kumbuka mimi babako,,utakuja nikumbuka
Dunia sasa iliko,,itele mengi mashaka
Leo Niko kesho siko,,duniani taondoka
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
10.Nguo ndefu niushamba,,wataamba mezeeka
Wanavaa walo shamba,,mjini zimetutoka
Nitapataje mchumba,,bila wowo kuoneka
*NGUO NDEFU SIZIWEZI,, NAKUWA KAMA MZEE*

*BABA*
11.Kuolewa si ngongingo,,wala wowowo mwanangu
Mana huo nimpango,,ulopangwa naye *MUNGU*
Nguo hizo nimtungo,,zilotungwa nawazungu
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
12.Aah baba Mimi siwezi,,kuyavaa mabwanga
Nitajaitwa shangazi,,angali bado mchanga
Bora zangu hizi hizi,,nikitembea naringa
*NGUO NDEFU SIZIWEZI,,NAKUWA KAMA MZEE*

*BABA*
13.Sikiza nalo kwambia,,mwanagu unielewe
Utatamba kwa dunia,,ukitaka uonewe
Ila kumbuka jalia,,aliyasema mwenyewe
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,ZAWAPA FAIDA GANI*

*MWANA*
14.Baba nimekuelewa,,yako nitazingatia
Nisije pata ngekewa,,kwa tamaa za dunia
Nikamuudhi molewa,,vimini kujivalia
*NGUO FUPI TENA BASI,,NARUDI VAA SITARA*

*🤝🏻PAMOJA🤝🏻*
15.Ndugu zetu twawambia,,zingatieni hakika
Zivaeni zilo ridhia,,nguo za kuheshimika
Zimridhishe nabia,,na *MOLA* Lo takasika
*NGUO ZA MAPAJA WAZI,,TUACHENI TUSI.

(MTUNZI: Malenga Msoso Salim)

Vyuo vikuu vya kibinafsi vilivyo bora nchini Kenya.

Kwa muda sasa taasisi za juu ya elimu nchini Kenya zimekumbwa na changamoto si haba kuhusiana na ubora wa mafunzo wazo.Kwenye upeo wa kimataifa vyuo vikuu vya umma vimeshamiri kulingana na takwimu zinatolewa kila uchao.Licha ya takwimu hizi baadhi ya vyuo vikuu vya kibinafsi pia zimeonekana zikitia fora.

Baadhi ya vyuo vikuu vya kibinafsi zilizo bora nchini Kenya ni kama vifuatavyo.

1.Chuo cha East African Baraton

Chuo hichi kilianzishwa mwaka wa 1978 kama shule ya kiadventista.Kipo mjini Eldoret na Nairobi.

2.Chuo cha Strathmore.

Chuo hiki kilianzishwa mwaka 2002.Kipo mjini Nairobi.

3.Catholic University of East Africa.

Hichi nacho kilianzishwa mwaka 1989.Kinapatikana mjini Eldoret, Nairobi na Kisumu.

4.United States International University of Africa.

Hiki chuo kilianza kufanya kazi nchini Kenya mwaka 1989.Kina tawi lake Nairobi.

5.Mount Kenya University.

Hiki chuo kilianzishwa mwaka 2008.Ni mojawapo kati ya vyuo vinavyojulikana sana nchini Kenya.Kina tawi Nakuru, Nairobi,Kitale.

Baba yangu yupo wapi.

***BABA YANGU YUPO WAPI?*** ** * #MTOTO
Yupo wapi baba yangu, mbona sijawahi mwona / Lanipa kizunguzungu, yeo itaitwa yana / Yamenizidi matungu, nomba niweke bayana / Baba yangu yupo wapi, mama naomba nijibu //// *

#MAMA
Kwani umewaza nini, hadi hivyo wauliza / Hapa ndo kwenu nyumbani, kipi kilichokukwaza / Ningependa nibaini, ewe mwanangu #Kazaza / Ewe mwanangu kipenzi, njoo hapa tuyajenge //// *

#MTOTO Hapo kwako ninakuja, ila usipotezee / Swali langu mie moja, nomba unielezee / Nijipatie faraja, ukweli hebu nigee / Baba yangu yupo wapi, nataka nimtambue //// *

#MAMA
Mwanangu kwanza tulia, kipi leo chakusibu / Kwanza uache kulia, cheki unajipa tabu / Wapaswa kuvumilia, utazua masaibu / Kwangu unakosa nini, kipi ambacho hupati //// *

#MTOTO
Ninakula ninashiba, sivyo maisha yalivyo / Napenda ‘mjue baba, kama vile ‘kujuavyo / Fuadi nina uhaba, najiona ovyoovyo / Baba yangu yupo wapi, ninataka mfahamu //// *

#MAMA
Ukikua utajua, kwanini hivi twaishi / Mwenyewe utagundua, ukweli na si uzushi / Kisha utayaamua, machungu ima fuleshi / Mwanangu kua uone, wakubwa tunavyoishi //// *

#MTOTO
Mama ninacho kifua, japo mdogo kiumri / Ukweli nataka jua, kujuza yako hiari / Siku nikija tusua, nijue wa kusitiri / Mama yangu nakupenda, hakika wewe shujaa //// *

#MAMA
Babako alikimbia, kisa mie sina kazi / Alisepa ukilia, yamemshinda malezi / Hawezi kuhudumia, maisha magumu shazi / Nduguze siwafahamu, hakutaka niwajue //// *

#MTOTO
Pole mama’ngu jasiri, unileae kwa tabu / Kwa jaala ya Jabari, twaishi hatuharibu / Sasa nimeshaabiri, umenifunza adibu / Ngoja nikateke maji, wewe nenda ukalale //// ** *

(Malenga ni Bin Omary)