Malimwengu.

MALIMWENGU

Jamani jama wandani, moyoni ninaumia,
Naloa damu kwa ndani, lazma mle tagandia,
Hata huku wajihini, kunyanzi yanivamia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Najiita hayawani, kwa udhia wa dunia,
Masumbuko manyumbani, uzee unaingia,
Matusi ya hadharani, matumbo yanaumia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Hata ninapojaribu, mathalani kuridhia,
Hayupo wa kunitibu, kukichapo ninalia,
Majanga yananisibu, wapi n’takimbilia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Nimejaribu jirani, yote haya kumwambia,
Kumbe sivyo nivyodhani, jirani anazamia,
Ashaikula yamini, rohoye kujikatia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Hata nao marafiki, mijini wamehamia,
Wote walioashiki, siwezi kuwafikia,
Wengineo mafasiki, maisha wanojutia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Nilijaribu kusoma, kazi kuikimbilia,
Vitabuni nilizama, aushi kupigania,
Haya yanoniandama, sikujua tapitia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Rahimu mwenye huruma, jikaze hima Jalia,
Mpaji wa yalomema, nipe nije furahia,
Vicheko vije kukoma, nami nije shangilia,
Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

(Malenga ni Francis Ondelo)

Penzi wangu ucjali.

Maisha hapa chuoni, ni magumu mno sana
Nafunga yangu machoni, ili kesho kuiona
Sembe sukuma mezani, kutia tukizi sana
Penzi wangu usijali nilikwacha nijikimu

Nguo moja nimekita, sio eti ninapenda
Hata nywele sijikata, juu juu zinapanda
Nyayo kwako nimekata, taniua nishakonda
Penzi wangu usijali, nilikwacha nijikimu

Kazi yake muhazili, sitaweka hata chapa
Kwa rehema za Jalali, hitatupwa kwebye pipa
Kwa hakika sina hali, ni maisha nanichapa
Penzi wangu usijali, nilikwacha nijikimu

Za kukwenda kwenye mesi, hata kumi mimi sina
Mkopaji kwenda mesi, limekuwa langu jina
Ninajuta hiyo kasi, likwendavyo hilo jina
Penzi wangu usijali, nilikwacha nijikimu

*Kevin* *Akong’o*
Akongokevin6@gmail.com

Yanga bingwa pinduzi.

***YANGA BINGWA MAPINDUZI***
**
*
Paka havuki bahari, kwenda kuifunga Yanga /
Katu hii siyo siri, kule Zenji wamelonga /
Icheki yao dosari, ni baada ya kipyenga /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Imedhihiri #sadfa, kisiwa cha Zanzibari /
Yanga kuipata sifa, ndani hii januari /
Simba kapata kifafa, kalambwa kombe shuburi /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Viza kwenda kisiwani, Paka koko wamekosa /
Wakashindwa ushindani, goli tukenda wanasa /
Wananchi burudani, Simba tumempapasa /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Ni kombe la Mapinduzi, siye tumeshalitwaa /
Mtani hawezi kazi, mcheki ameduwaa /
Amewamba bumbuwazi, muda ulimuhadaa /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Kombe latua Jangwani, tumemfunga mtani /
Pale uwanja Amani, tumewapa tamrini /
Mato yao yapo chini, waona hawaamini /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Yanga daima ni mbele, kurudi nyuma ni mwiko /
Tumewachoma mishale, ilowafanya mideko /
Msimbazi ni kelele, ngebe nazo hadaiko /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Aibu yao wenyewe, tumewagongea Zenji /
Wamebaki na kiwewe, tumewaachia chenji /
Hakuna sandakalawe, tumewapigia tanji /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Siyo pila biriani, sasa pila mashendea /
Na njaa haliiwini, bali mewaongezea /
Hawa Simba matopeni, kushindwa wamezoea /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani ////
*
Kaditama kipembuzi, #Khamicyzo ninakaa /
Weka wako uchambuzi, kufungwa Simba adaa /
Halikwepo pingamizi, sie kwetu si ajaa /
Tumetwaa Mapinduzi, kwa kumfunga mtani

(Malenga ni Bin Omary)

Nampenda.

NAMPENDA😍😍😍

Nimezama mapenzini
Na sitamani kutoka
Nimempenda Fulani
Na yeye ameridhika
Hata mi mnipe nini
Mimi kwake nimefika
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Kumuacha abadani
Nathubutu kutamka
Nyonga mkalia ini
Huyu wangu muhibaka
Amenikaa moyoni
Katu hawezi kutoka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Amenijaa kichwani
Siachi kumkumbuka
Hata nikiwa ndotoni
Sautiye yasikika
Namuomba RAHMANI
Marengo kutimizika
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Nampa vitu laini
Meno yasije kun’goka
Biriani ya maini
Ale pindi akitaka
Nae kaniganda yani
Hawezi kuchoropoka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Anipenda si utani
hatamani kuchepuka
Mimi kwake ndie shani
Nanga’ra nanawirika
Pindi akinita hani
Naitika rabaika
Nampenda kweli kweli
Kumuacha abadani

Pole ya yule Fulani
Kwangu alieondoka
Hakwona yangu thamani
Ndio akachoropoka
Nimempata hayuni
Na Mimi ametosheka
Nampenda kweli kweli
Kumuacha abadani

Kuachana abadani
Labda mola akitaka
Nasi twamwomba manani
Upendo kuimarika
Sote tufike ndoani
Kwa uwezo wa rabbuka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

Kalamu nashusha chini
Nimechoka kuandika
Anipende daimani
Katu nisije achika
Mahasidi wa pembeni
Waishie kuumbuka
Nampenda kwelikweli
Kumuacha abadani

(MTUNZI: Bintrasool)

Hana Taraka.

HANA TARAKA.

Na tena mkitengana, hawara hana taraka,
Wala hatongozwi tena, hawara ukimtaka,
Tena mnapokutana, ya nyuma kuyakumbuka,
Hana taraka hawara, ukweli nimebaini..

Nilikuwa ninabisha, kukataa jambo hili,
Yanayo mengi maisha, mengine sio ya kweli,
Hili nimethibitisha, kwa macho yangu mawili,
Hana taraka hawara, ni kweli sio utani.

Usije kudanganyika, Aseme wameachana,
Mambo yatavurugika, siku watapokutana,
Yalio sahaulika, yote watakumbushana,
Hana taraka hawara, Chunguza utabaini..

Wasema umempata, na umfute machozi,
Alomliza hufwata, tena bila ya ajizi,
Akitakacho hupata, na kupeana mapenzi,
Hana taraka hawara, hilo weka akilini..

(Malenga ni Ibn Kimweri.

Jitokeze nikuone.

JITOKEZE NIKUONE

Yuko wapi nauliza, mwenye mapenzi ya dhati?
Kipusa wa kupendeza, mtego kwa ‘tanashati?
Asiyependa kuliza, na akipenda hasiti?
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.

Aliye na umbo nzuri, aibuaye hisia?
Mtamu kama sukari, ‘kimbusu najifia?
Nihisi mie ushwari, na akinikisi pia?
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.

Fundi wa kusasambua, tena bila kusumbua?
Na kiuno kunengua, tena bila kutegua?
Katu sitomzingua, ‘tampenda atambue,
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.

(MTUNZI:Kongowea)

Mapenzi yanaumiza.

MAPENZI YANAUMIZA

Bora uchomwe na mwiba
Ukitoa utapona
Sio utoswe na huba
Kwa yule mlopendana
Ukamwita mahabuba
Leo haunae mbona
Mapenzi yanaumiza
Maumivu yasokwisha

Chakula hautoshiba
Hamu ya kula hauna
Utachukia mahaba
Hutaki kupenda tena
Moyo wauma si haba
Tena Unauma Sana
Mapenzi yanaumiza
Maumivu yasokwisha

Machozi yanakukaba
Kutoka yashindikana
Wajuta majuto Saba
Kwanini ulimuona
Umeipata dhoruba
Mapenzi kweli hakuna
Mapenzi yanaumiza
Maumivu yasokwisha

Ulimwambia na baba
Kuwa umepata bwana
Sio bwana wa miraba
Bwana ametulizana
Leo mepata jaziba
Penzi la kudanganyana
Mapenzi yanaumiza
Maumivu yasokwisha

Hapa ninaweka kaba
Nimechoka kusonona
Ninamuachia RABBA
Sitaki mi kulumbana
ALLAH tanipa hijaba
Moyo wangu tulizana
Mapenzi yanaumiza
Maumivu yasokwisha

(MTUNZI: Bintrasool)

Kila la heri mwereni.

KILA LA HERI MWERENI
Salamu zangu nawapa, kaka yenu muadhamu
Niwambie pasi pupa, jambo lililo muhimu
Mtihani si mfupa, kwenu usiwe mgumu
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Muda sasa umefika, wa kuyavuna mapando
Kwa walimu sina shaka, waliwalisha uhondo
Mwisho atakaye cheka, hucheka kwacho kishindo
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Alopanda pametosha, mwambieni aamke
Atavuna pamekwisha, jina la shule lishuke
Walimu wakifundisha, kaeni ange mshike
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Ng’ombe msham’maliza, mkia usiwashinde
Mwishoni mkateleza, nawasihi chondechonde
Kamwe msije kucheza, Malaika wawashinde
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Katu msitetereke, bidii kuipunguza
Muda bado msichoke, mkajawa mapuuza
Nawaomba mdamke, vitabu kuvitukuza
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Someni kana ya kwamba, kesho hamsoni tena
Vilo chini kuvichimba, akilini kuvishona
Ngurumeni kama simba, wenye njaa zilo nona
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Kuweni sana karibu, huno muda na walimu
Maswali yakiwaswibu, kuwaona ni muhimu
Dokita watawatibu, keshoni mtahitimu
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Usiwapenye uzembe, mkaanza kujisifu
Kwa mola sana muombe, awalindeni Raufu
Siku chache msiyumbe, shikeni njia nyoofu
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Hadhi ya shule kudumu, ni nyie washika dau
Jaeni nyingi hamumu, wajawazito falau
Nawaachia hatamu, ishikeni angalau
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Izidisheni nidhamu, kwa walimu wenu pia
Katu wasiwalaumu, nukusi kuwatilia
Naiangusha kalamu, hapa kumi nakwamia
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

(Malenga ni Daniel Wambua)