Dhana Ya Wahusika.

Dhana ya wahusika katika kazi za fasihi imewahi kufasiliwa na watafiti kadhaa. Kama
ilivyokwishaelezwa kuwa wahusika katika kazi za fasihi ni viumbe wanaopatikana katika hadithi
yoyote ile. Viumbe hawa huwa sehemu ya kazi nzima. Pili, wahusika ni binaadamu
wanaopatikana katika kazi ya kifasihi, na ambao wana sifa za kimaadili, kitabia, kiitikadi,
kifalsafa ambazo hutambulishwa na wanayoyasema na wanayoyatenda. Wahusika huweza
kutambulishwa pia na maelezo ya mhusika au msimulizi, msingi wa hisia, hali ya kimaadili,
mazungumzo na matendo ya wahusika ndio kiini cha motisha au uhamasishaji wa wahusika
(Wamitila, 2002).
TUKI (1998:169), wamefasili wahusika kuwa ni watu, miti au viumbe vinavyowakilisha watu
katika kazi za fasihi. Wahusika hutumiwa katika kazi za fasihi ili kuwakilisha hali halisi ya
maisha ya watu katika jamii inayohusika. Katika mgogoro unaozungumziwa katika kazi ya fasihi
hutumiwa kuwakilisha mawazo mbalimbali ya pande mbili au zaidi za mgogoro huo.
Maelezo hayo ya Wamitila na TUKI yalikuwa na umuhimu mkubwa katika kusukuma mbele
kazi hii. Hii ni kutokana na kwamba, Wamitila amedokeza maswala muhimu sana katika kutoa
maana ya wahusika katika kazi za fasihi. Sifa kama zile za kimaadili, kitabia, kiitikadi, kifalsafa
ambazo huwa zinawatambulisha wahusika hao zilitupa mwanga na muongozo mzuri katika
utafiti wetu huu uliolenga kuchunguza namna wahusika wanavyolandana na majina yao katika
riwaya teuliwa.
Rono (2013) akimnukuu Msokile (1992:42-43), anaeleza kwamba, wahusika husawiriwa kisanaa
na mwandishi ili waweze kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha katika jamii. Mwandishi
huwasawiri wahusika kwa wasomaji wake kwa kutumia sifa pambanuzi walizonazo, jinsi
walivyo, mambo gani hawayapendi na yapi wanayapenda katika maisha yao na kadhalika.
Wahusika hao hutumia misemo, nahau, tamathali za usemi na methali katika mazungumzo yao
ili kujenga tabia na hali ya kisanaa Rono (ameshatajwa), anaendelea kueleza kuwa, wahusika wa kazi za sanaa huwa na tabia
zinazotofautiana kati yao kwa sababu mbalimbali. Kwanza kabisa inategemea mwandishi ana
lengo gani analotaka kuonyesha katika kazi yake ya sanaa. Pili, aina ya kazi ya sanaa inaweza
kuathiri aina ya wahusika jinsi walivyosawiriwa, kuaminika kwao, wanavyohusiana wao kwa
wao, uwakilishi wao na majina yao. Wahusika katika hadithi ni mhimili mkubwa katika fasihi
andishi na hata simulizi.
Aidha, Msokile (1992), akiwanukuu Penina Muhando na Ndyanao Balisdya wanasema kwamba
wahusika wanaweza kuumbwa kinafsia, kiakili na kimwili. Kutokana na ujenzi wa aina hii,
mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au anaweza kuonyesha mabadiliko yake kila
anapokutana na mazingira tofauti. Ataonyesha mabadiliko katika uhalisia wake kwa kuzingatia
nguvu zinazomzunguka kama vile za utamaduni, siasa, uchumi na kadhalika.
Kwa mujibu wa Wamitila (2008:369), wahusika ni nyenzo kuu katika fasihi kwa sababu
wahusika ndiyo dira ya matukio na matendo yanayopatikana katika kazi ya kifasihi inayohusika.
Mtazamo wa dhana ya wahusika hutofautiana kutegemea mkabala anaouchukua mhakiki na
nadharia ya fasihi inayohusika.
Mhusika ni mtendaji katika kazi ya kifasihi na huwa kielelezo cha viumbe wanaopatikana
ulimwenguni, ingawa si lazima sifa zote za mhusika zifungamane moja kwa moja na za
wanadamu. Hii ndio maana neno “mhusika” linatumika bali si ‘mtu’ au ‘Kiumbe’. Mwelekeo wa
kuwahusisha wahusika wa kifasihi na binadamu wanaopatikana katika hali halisi huathiri kwa
kiasi fulani matarajio ya usawiri wa uhusika. Upo mwelekeo mkubwa wa kuwachunguza
wahusika wa kifasihi kwa kuwafungamanisha na binadamu halisi na hata, labda kutokana na
athari za mielekeo ya kimaadili, tukitarajia kuwa wahusika, hasa wale wakuu watakuwa na
maadili fulani.

Hata hivyo, tunakubaliana na Kundera (2007) kuwa, wahusika wa kifasihi hawahitaji kupendwa
kutokana na maadili yao bali wanachotakiwa kufanywa ni kueleweka. Matendo yanayopatikana
katika kazi ya kifasihi huhusishwa na wahusika. Matendo hayo ni nguzo kuu ya dhamira na
maudhui yanavyoendelezwa katika kazi inayohusika. Mawazo hayo ya Kundera yalitupa
mwanga mkubwa wakati wa kuwachungua wahusika na namna wanavyolandana na majina yao
na namna walivyobebeshwa dhamira na waandishi wa riwaya teuliwa.
Kulingana na Njogu na Chimerah (1999:45), wahusika ni viumbe wa sanaa wanaobuniwa
kutokana na mazingira ya msanii. Mazingira haya yaweza kuwa ya kijiografia, kihistoria,
kijamii, kitamaduni au ya kisiasa. Wahusika hujadiliwa kwa namna wanavyoingiliana na
dhamira na hili hujitokeza kutokana na maneno, tabia na matendo yao, yaani kulingana na hulka
yao. Wahusika wa aina yoyote wawe watu au viumbe hurejelea na huakisi sifa na tabia za
binadamu katika jamii husika.

Njia za kubainisha wahusika.

Uchunguzi wa historia na maendeleo ya fasihi unadhihirishwa kuwa, wahusika wa kifasihi
hubadilika kadri wakati unavyoendelea. Wahusika wanaopatikana katika kazi za kifasihi za
miaka ya zamani wanatofautiana kwa kiasi kikubwa na wahusika wanaopatikana katika kazi za
fasihi za miaka ya baadaye.
Njogu na Chimerah (1999:40-44), wanarejelea wahusika wanaozungumziwa Mlacha na
Madumulla (1991).
Wamitila (2008: 382-392), amegawanya wahusika katika makundi manne. Mhusika wa jadi,
mhusika wa kimuundo au kimtindo, mhusika wa kihalisi na mhusika wa kisasa.

Mhusika wa kijadi.
Dhana ya kijadi inakwenda na suala la wakati na hasa wakati wa zamani. Mhusika wa aina hii
basi ni anayeweza kuelezwa kama mhusika wa zamani. Mtindo huu wa kusawiri wahusika
umetumiwa na baadhi ya waandishi mbali mbali wa kazi za fasihi. Kwa mfano, katika tamthiliya
ya Kivuli Kinaishi (1990), mhusika Bi Kizee ni mfano wa mhusika wa kijadi. Aidha, katika
tamhiliya ya Mfalme Juha (1971) wahusika Mfalme na Juha ni mfano wa wahusika wa kijadi
kwa sababu hawa wamekuwa ni wahusika wa kimapokeo katika kazi mbali mbali za kisimulizi.
Mhusika wa Kimuundo na Kimtindo
Mhusika wa kimuundo na kimtindo huainishwa kuhusiana na wahusika wanaorejelewa. Mawazo
ya wana muundo ni ya kimsingi katika kuwainisha wahusika wa aina hii. Kulingana na Wamitila
(2008), wahusika wa aina hii wameainishwa kama ifuatavyo:
Mhusika wa Kiuamilifu
Huyu ni mhusika ambaye anabainishwa kwa kuwa na sifa za aina moja ambazo kimsingi
zinapangiwa kumfanya mhusika huyo kuwa chombo cha mwandishi ili kutimiza lengo fulani.
Pia anaweza kubainishwa kwa kuangalia nafasi yake ya kiutendaji. Mfano nzuri ni Karama
katika riwaya ya Kusadikika (1981) , yeye atumiwa na msanii kufanikisha lengo lake akiwa
kama mzalendo na mkombozi wa jamii.

Mhusika wa kiishara.
Mhusika wa kiishara anatumiwa kiishara, yaani ni sehemu ya uashiriaji katika kazi ya kifashi.
Kwa mfano Rono (2013), anamtumia Mhusika Amani katika Kidagaa Kimemwozea (2012),
kama ni ishara ya mabadiliko katika jamii ambayo haiwezi kuuliwa na harakati za utawala
mbaya wa kuyazuia mabadiliko yenyewe. Ndiye aliyeongoza katika uchunguzi wa nyendo za
Nasaba bora wakiwa na Majisifu kisha wakagundua matendo yake maovu. Aidha, kisa cha fahali
kumeza nguo katika riwaya hiyo ya Kidagaa Kimemwozea ni ishara ya nasaba bora aliyokuwa akitafuna ardhi na mali za raia wake bila huruma na kuwaacha maskini. Usimulizi wa mto
Kiberenge na maji yake kutonywewa na wakazi wa maeneo yake ni ishara kuwa, wakati hao
huafikiana na maswala fulani bila utafiti au uchunguzi wowote.
Wahusika wa Kinjozi
Wahusika wa kinjozi ni wahusika wanaohusishwa na fantasia. Hupatikana katika ulimwengu wa
ajabu. Kwa mfano, Mhusika Pama katka riwaya ya Siri za Maisha ni mfano wa Mhusika wa
kinjozi kutokana na matendo yake ya kiajabu.

Mhusika wa kihalisi.
Msingi mkuu katika uainishaji wa wahusika wa aina hii ni kanuni ya maisha halisi, kwa
kutegemea kanuni ya ushabihi kweli. Mhusika wa kihalisia ana sifa nyingi zinazohusishwa na
binadamu katika maisha ya kila siku. Kulingana na Wamitila (2008), tapo hili lina wahusika wa
aina tatu, mhusika wa kimapinduzi, mhusika wa kisaikolojia na mhusika wa kidhanaishi.
Wahusika hawa wamefanyiwa uchambuzi kama ifuatavyo:
Mhusika wa Mapinduzi
Mshusika wa kimapinduzi ana sifa zote zinazohusishwa na mtu anayeweza kupatikana katika
maisha halisi. Mhusika huyu anasukumwa na kuchochewa na nia ya kutaka kubadilisha jamii
yake. Wahusika Mdoe na Sikamona katika riwaya ya Zawadi ya Ushindi ni mifano mizuri,
wanasukumwa na nia ya kutaka kuyabadilisha maisha katika jamii yao ambayo inaongozwa na
viongozi walafi na wananchi wengine wenye tamaa ya kupata mali kwa njia zisizo za halali.
Mhusika wa Kisaikolojia
Mhusika wa kisaikolojia anaonyeshwa kwa undani zaidi na labda hata misukumo ya kisaikolojia
ya matendo yake kuonyeshwa kwa njia bayana. Mama Ntilie katika riwaya ya Watoto wa Mama
Ntilie ni mhusika wa kisaikolojia kulingana na yale anayopitia kutoka kwa mumewe Lomolomo
na pia kufukuzwa kwa watoto wake shule kunapelekea kutumia akili yake zaidi ili apambane na
hali hiyo na kumiliki nafsi yake isiathirike kisaikolojia.

Mhusika wa kidhahanishi.
Mhusika wa kidhanaishi anaakisi sifa kadhaa zinazohusishwa na falsafa ya udhanaishi ambayo
msingi wake ni kudadisi ukweli, furaha na hali ya kuweko maishani. Mfano nzuri wa kazi za
kifasihi zilizoandikwa na Kezilahabi kama vile Nagona na Mzingile zinasadifu sana matumizi ya
wahusika wa kidhanaishi. Katikariwaya ya Nagona , wahusika Paa na Mimi wanawakilisha
kundi hili.
Wafula na Njogu (2007), wanasema kwamba mhusika anaweza kuangaliwa kama mtu binafsi na
maisha yake. Waliorodhesha wahusika kama jaribosi au nguli, kivuli na wengineo. Nguli
aghalabu huwa mhusika mkuu mbaye husafiri kwa sababu fulani. Mara nyingi safari hii huanzia
utotoni hadi anapofikia utu uzima. Wakati mwingine hii inaweza kuwa safari ya kikweli ambapo
nguli anajizatiti kukisaka kitu au kujisaka mwenyewe. Mkinzani wa nguli hupambana kuiharibu
mipango ya nguli kwa kujaribu kumwangamiza. Aghalabu mhusika huyu huwa mzinzi, mlafi na
wakati mwingine huwa tajiri kama vile Mzoka katika riwaya ya Miradi Bubu ya Wazalendo.
Aidha katika riwaya ya Adili na Nduguze, mhusika Adili anasafiri kwa ajili ya kufanya biashara.
Katika safari hizo tunaoneshwa ndugu zake Mwivu na Hasidi wanavyoamua kumtupa baharini
kutokana na wivu na choyo.
Mwisho tunaona namna anavyookolewa na mtoto wa Mfalme wa Kijini, Huria. Mjadala huu
kuhusu matapo ya wahusika ulikuwa na manufaa sana kwa mtafiti, kwa sababu, mtafiti alitumia
mawazo hayo, ili kubaini aina za wahusika waliotumika katika riwaya teuliwa.

Mbinu za kusawiri wahusika.

Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mwandishi anaweza kutumia njia kadhaa na tofauti katika
kuwasawiri wahusika wake. Msanii ana uhuru sio tu wa kuwatumia wahusika wa aina fulani, bali
wa kuiteua namna ya kuwawasilisha wenyewe. Kama wasomi na wahakiki wa fasihi,
tunategemea sifa kadhaa kuwaelewa wahusika hao: maumbile yao, mienendo na tabia zao, lugha
zao, vionjo vyao, uhusiano wao na wahusika wengine, hisia zao kwao na wengine, mazingira na
mandhari yao, kiwango chao cha elimu, jamii yao nakadhalika.

Mbinu zinazotumika kusawiri wahusika ni kama vile; mbinu ya kimaelezi, mbinu ya kidrama,
mbinu ya uzungumzi nafsi wa ndani, mbinu ya majazi au matumizi ya majina, mbinu ya
kuwatumia wahusika wengine na mbinu ya ulinganuzi na usambamba.
Wamitila ameainisha na kuchambua mbinu zifuatazo ambazo hutumika katika kuwasawiri
wahusika. Mbinu hizo zimetolewa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Mbinu ya kimaelezi.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002:23-24), anayetumia mbinu hii huzieleza sifa za mhusika na
mara nyengine hutoa picha ya maneno inayomwelezea mhusika anayehusika. Kwa kutumia
mbinu hii, mwandishi anakuwa na nafasi ya kubainisha mapenzi au chuki yake dhidi ya
wahusika fulani. Hii ni njia rahisi ya kuwasawiri wahusika na hasa kwa kuwa mwandishi
anaweza kutoa maelezo machache yanayoifumbata tabia au wasifu wa mhusika ambao
ungechukua muda mrefu kutokana na matendo yake mwenyewe. Hata hivyo, hii ni mbinu
ambayo ina udhaifu pia.
Mbinu hii ya kimaelezi haimpi msomaji nafasi ya kushiriki katika kuitathmini tabia ya mhusia
fulani. Analazimika kuukubali msimamo na kuridhika na maelezo ya mwandishi. Mfano
unaofuata unaonesha namna ya mbinu hii inavyotumika; kutoka katika riwaya ya Vuta n`kuvute
ya Shafi A Shafi:
“Yasmini alikuwa na kijuso kidogo cha mdawiri mfano wa tungule na macho makubwa ambayo
kila wakati yalionekanwa kama yanalengwalengwa na machozi. Alikuwa na pua ndogo,
nyembamba na chini ya pua hiyo ilipangana midomo miwili mizuri iliyokuwa haitulii kwa tabia
yake ya kuchekacheka, huku akionyesha safu mbili ya meno yake mazuri. Alikuwa na kichaka
cha nywele nyeusi zilizokoza ambazo zilianguka kwa utulivu juu ya mabega yake. Alikuwa si
mrefu lakini hakuwa mfupi wa kuchusha, na matege aliyokuwa nayo yalizidi kuutia haiba
mwendo wake wakati anapotembea” (1999:1).

Haya ni maelezo ya mwandishi kumhusu mhusika huyu ambayo yanatokea katika sehemu ya
mwanzo. Ingawa hasemi wazi wazi, uteuzi wake wa maneno unatuelekeza kuamini kuwa ana
mtazamo fulani kumhusu mhusika na ambao huenda ukatuelekeza kwenye njia fulani.

Mbinu ya kidrama.
Wamitila (2002), mbinu hii ya ki-muhakati (ki-mimesia), kama ilivyo katika tamthilia,
huonyesha wasifu wa mhusika wake. Pia mbinu hii inamwezesha msomaji au mhakiki kumjua na
kumweleza mhusika bila ya kuathiriwa na mtazamo wa mwandishi au msimulizi kumhusu.

Mbinu ya uzungumzaji nafsi wa ndani.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mbinu hii hulinganuliwa na nyengine inayojulikana kama
mkondo wa king’amuzi/kirazini. Mawaazo yanayopatikana katika mbinu hii huwa na
mshikamano wa muwala, mawazo hayo yamepangika kama unavyoweza kutokea katika
ung’amuzi nafsi wa kawaida, yaani pale endapo mhusika anapoongea peke yake.
Kwa upande mwengine, mkondo wa king’amuzi ni mbinu inayotumiwa kuonyesha mawazo
hayo au hisia za wahusika bila ya kuyahariri mawazo hayo au kuyapanga kwa namna yoyote ile
iwayo. Hii ni mbinu inayotumiwa sana katika uandishi wa unaokita kwenye tapo la usasaleo.
Mbinu ya uzungumzi nafsi wa ndani hujulikana kama “mjadala wa ndani” au “mjadala mdogo”.
Mjadala unaonekana hapa unazihusisha sauti mbili zinazohusika kwenye majibizano. Sifa
muhimu ni kuwa lazima maswali au majibu yanayopatikana yaibuke katika sauti ambazo
zinawakalisha mikabala, imani au sifa tofauti.

Mbinu ya kuwatumia wahusika wengine.
Wamitila (2002:26), badala ya kuyatumia majina ya wahusika, mwandishi anaweza kusawiri
mhusika kupitia kwa kuelezwa na wahusika wengine. Wahusika wanaweza kuelezwa na
wahusika wengine, yaani tunawajua kutokana na maneno ya wahusika wenzao. Hapa pana
tathmini ya mhusika ambayo ni ya ndani (kwa wahusika wengine), kuliko ya nje kama ya
masimulizi (mbinu ya kimaelezi).
Hata hivyo lazima tukumbuke maneno anayoyatamka mhusika A kumhusu mhusika B yanaweza
kuangaliwa kwa njia mbili. Kwanza, yanaweza kutusaidia kumwelewa B kwa kutufichulia
mambo ambayo hatuwezi kuyajua bila ya kuelezwa. Pili, inawezekana kauli anazozitamka A
kumhusu B zikatuonesha alivyo mhusika A kuliko alivyo B.

Mbinu ya ulinganuzi na usambamba.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002), mwandishi anaweza kuitumia mbinu za usambamba na
ulinganuzi katika kuwasawiri na kuwakuza wahusika wake. Ulinganuzi ni nini? Huu ni
ulinganishi kwa kinyume. Kuweko kwa mhusika ambaye ni kinyume cha mhusika fulani huweza
kuwa ni mojawapo ya uhusika.
Mwandishi anaweza pia kuwaweka wahusika au kuwaonyesha kwa namna ambazo ni sambamba
na kwa njia hii humfanya msomaji au mhakiki aziwazie tofauti au mfanano wa sifa zao. Ni
muhimu kukumbuka kuwa ulinganuzi sio tu mbinu ya uhusika bali hutumiwa katika usimulizi
wa matukio na ukuzaji wa dhamira na maudhui.
Wakati huo huo mwandishi anaweza kuwasawiri wahusika kwa namna ambavyo tabia zao
zinaonesha kupingana kwa aina fulani. Yaani tukimwangalia mhusika kwa makini, tunahisi
kuwa kuna kupingana kwa sifa fulani katika uhusika wake. Hapa tunasema kuwa za ki-nzani.

Mbinu ya majazi au matumizi ya majina.

Wamitila (2002), waandishi wa kazi za kifasihi huweza kuyatumia majina ya wahusika ambayo
huakisi mandhari zao, wasifu wao, itikadi zao, vionjo vyao na kadhalika. Uchunguzi wa majina
ya wahusika lazima uhusishwe na msuko, mbinu za utunzi, ucheshi, dhamira na maudhui na
itikadi au motifu katika kaziinayohusika.
Tunapozungumzia kulandana kwa wahusika na majina yao katika kazi faulani ya fasihi, ni kule
kuwiana kwa matendo ya wahusika na majina yao, sifa zao na majina yao, lugha yao na majina
yao, kujiamini kwao na jinsi majina yao yalivyo, elimu yao na majina yao, maana ya majina yao
na jinsi yanavyofanana na wao wenyewe ambapo msanii wa kazi ya fasihi huzitumia sifa hizi,
katika kusadifu hali fulani iliyozoeleka katika jamii.
Maelezo hayo yalikuwa na mchango mkubwa kwa mtafiti katika kusukuma mbele utafiti huu.
Hii inatokana kuwa Wamitila ameweza kuonesha na kufafanua vipengele vya msingi ambavyo
vilitumiwa na mtafiti katika kuchambua lengo la utafiti na hatimae kuweza kufikia lengo la
utafiti huu.
Aidha, kamusi ya BAKIZA (2010:208), wamefasili neno kulandana kuwa, linatokana na nomino
landa lenye maana ya kitendo cha kufanana na mtu ama kushabihiana. Landana pia ni kitendo
cha mtu kuwa na sura inayofanana na mwenzake; shabihiana.
Ingawa maelezo ya BAKIZA juu ya neno kulandana hayakuelezwa kwa mkabala wa kifasihi,
hata hivyo, maelezo hayo yalitoa mwanga kwa mtafiti, kuhusu maana halisi ya neno kulandana,
ambapo aliitumia dhana hiyo katika uchambuzi wa data zake.
Wamitila (2002:64), sadifa katika fasihi; kwake yeye, sadifa ni uzuri au ubaya. Sadifa ni utukiaji
wa matukio kwa wakati mmoja na aghalabu kwa namna ya kushangaza inayoashiria bahati.
Umuhimu wa dhana hii unatokana na kujitokeza kwake kwingi katika kazi kadhaa za fasihi ya Kiswahili. Kwa kuanzia ni muhimu kutaja kuwa sadifa hutumiwa kama mbinu au kipengele cha
msuko au kimtindo. Katika baadhi ya tanzu, sadifa ni kipengele muhimu katika muundo wake.
Tuisomapo hadithi ya Jamaadar ya Mui huwa Mwema, yanayaona matumizi ya sadifa kuhusiana
na Kotini na wahusika wengine. Vivyo hivyo katika riwaya za M.S.Abdulla. Katika riwaya za
M.S.Abdulla huwa sadifa jinsi matukio ya wahalifu yanavyokunjuka na hatimaye kufichuka.
Sadifa katika kazi hizi ni kipengele cha lazima.
Maelezo haya ya Wamitila tunaona kuwa yana mnasaba na mshabihiano mkubwa katika mada
yetu ya kuchunguza dhana zilizobebwa na wahusika na zinavyolandana na majina yao, hivyo ni
dhahiri kwamba kupitia maelezo haya tuliyatumia kama dira ya kufikia lengo la utafiti wetu.
Njogu na Chimerah (1999), wameeleza kuhusu suala la sadifa kwa wahusika katika riwaya ya
Siku Njema, ambapo wahusika Bi Rahma kasadifu vyema, Rashid Omar kasadifu na anakufa
lakini kifo chake si cha kifasihi, Zawadi anasadifu kuolewa na Kongowe, mtoto wa miaka kumi
na sita, ilihali yeye ana miaka ishirini na mitatu na akiwa na elimu ya juu. Pia wahusika wengine
waliohakikiwa ni Alice MacDonald, Vumilia Abdalla, Amina na Juma Mukosi.
Ufafanuzi wa huu uliofanywa na Njogu na Chimerah unaonekana kuwiana vyema na mada yetu
hii ya kuchunguza dhana zilizobebwa na wahusika na zinavyolandana na majina yao, hivyo kwa
kuzingatia mbinu hii pia mtafiti alipata msaada mkubwa uliomwezesha kufikia malengo ya
utafiti wake.

(Makala haya yaliandaliwa na Mwalimu Omukabe wa Omukabe wa Chuo Kikuu cha Kenyatta

Idara ya Kiswahili)

Dhana za falsafa ya historia katika riwaya.

Falsafa ya historia inahusu utaratibu maalumu na wenye kuzingatia umakini wa hali
ya juu unaoongoza tafakari juu ya sura anuwai za zama zilizopita na ufahamu wa
mambo ya kale. Falsafa ya historia inatuwezesha kuelewa kwamba historia
inajitokeza katika sura mbalimbali, kwani hakuna historia iliyo katika sura ya aina
moja. Pia, inatuwezesha kufahamu kwamba kuna ufahamu wa namna tofauti wa
historia. Hii inaweza kuwa kati ya mtu na mtu na, wakati mwingine, jamii na jamii.
Falsafa ya historia inajumuisha pia dhana muhimu ya historiografia


11.namna
maarifa ya historia yanavyojitokeza, na mikabala mikuu ya maarifa ya historia12
(VaŜíĉek, 2009). Kimsingi vipengele hivi, vinabainisha namna uga wa historia
ulivyo au unavyotakiwa kuwa. Kupitia vipengele hivi, tunaweza kujiegemeza kwa
sehemu ili kuonesha namna ambavyo vipengele hivi vinajitokeza katika riwaya za
Kiswahili na hivyo kutuwezesha kujenga hoja kwamba, riwaya zinafaa kufundishia
historia. Hii ina maana kwamba tunapozitalii riwaya za Kiswahili tunabaini
kujitokeza kwa mawazo mbalimbali ya msingi yanayojitokeza katika mjadala wa
falsafa ya historia


13. Pia, ieleweke kuwa falsafa hii ya historia ilienda ikibadilika
kutegemeana na wakati pamoja na mahali. Kutokana na ukweli huu, mawazo
mbalimbali yanayojitokeza kuhusiana na mjadala wa falsafa ya historia,
yanajitokeza katika vipindi tofauti na mahali tofauti (VaŜíĉek, 2009:31-35; Lemon,
2003:14-84). Baadhi ya mawazo hayo kuhusu maana na mielekeo ya historia
yanajirudia kwa namna sawa kabisa toka kipindi kimoja kwenda kipindi kingine
cha wakati. Wakati mwingine yanajirudia kwa namna inayokaribiana lakini si kwa
usawa kabisa. Mielekeo na maana ya historia inadhihirishwa kupitia hoja ambazo msingi wake ni katika falsafa ya historia ya vipindi na mahali tofauti. Hivyo basi, ni
muhimu kuifahamu mielekeo hii ili tuweze kuangalia namna inavyojitokeza hata
katika riwaya za Kiswahili. Mawazo kuhusu mielekeo na maana ya historia ni haya
yafuatayo:
Mosi, ni kujirudia kwa historia

14. Hii ni dhana inayojitokeza sana kwa baadhi ya
mikabala ya maarifa ya historia. Kinachoonekana hapa ni dhana ya umviringo wa
historia au uduara. Ambapo hoja ya msingi inayotolewa katika dhana hii ni juu ya
matukio ya kihistoria kuwa na tabia ya kujirudia. Kujirudia huku huhusisha wakati
pia.
Pili, kuhusu chanzo cha mabadiliko ya kihistoria


15. Mabadiliko haya, kwa baadhi ya
wataalamu wanaona ni kama yanayosababishwa na nguvu fulani iliyo nje ya uwezo
wa mwanadamu. Mawazo haya ndiyo yanayosababisha kuibuka kwa dhana ya
majaaliwa na kuandikiwa kwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu.
Tatu, ni nafasi ya mwanadamu katika kuibadilisha historia yake

16. Dhana hii
inalenga kutukuza uwezo alionao mwanadamu katika kubadilisha hali
iliyomzunguka. Dhana hii, inapingana na dhana inayomchukulia mwanadamu kama
kiumbe asiye na nafasi ya kubadilisha historia yake. Waumini wa dhana hii
wanapingana na suala la majaaliwa ya wanadamu. Hivyo basi, wanamweka mbele
mwanadamu kama chanzo cha mabadiliko yoyote ya kihistoria.
Nne, nafasi ya historia katika maisha. Hii inajikita katika kutazama nafasi ya
historia kumwezesha mwanadamu kujifunza mambo kadhaa ambayo hapo baadaye
atakutana nayo katika maisha

17. Mwelekeo au mtazamo huu unategemeana na imani iliyopo juu ya mtiririko wa historia. Kama ni ule wa kujirudia au kama ni ule wa
kila hatua ya historia kuwa ni ya kipekee, na hivyo kukosekana kwa chochote
kinachoweza kuwa fundisho kwa maisha ya baadaye.
Tano, ni mawazo yanayoegemea katika aina fulani ya historiografia. Kuna aina
nyingi za historiografia. Miongoni mwake ni pamoja na: historiografia ya kikabaila,
historiografia ya kibepari, historiografia ya kimapinduzi, historiografia ya kikoloni,
historiografia ya Kiafrika na historiografia ya kisasa. Kutokana na uhusiano uliopo
kati ya fasihi na historia, kazi nyingi za fasihi, na riwaya ikiwemo, hutoa mwangwi
wa historiografia iliyoongoza uandishi wa riwaya inayohusika. Pia, huweza kutoa
mwangwi wa historiografia mbili ambazo zinapambana kuweza kutawala.
Mwalimu yeyote wa historia anayetaka kufundisha historiografia anaweza
kuchagua riwaya inayoendana na histografia aliyoikusudia.

Changamoto na ufumbuzi wa riwaya za Kiswahili.

Licha ya kuwepo kwa mazingira mwafaka ya riwaya ya Kiswahili kutumika
kufundishia historia, tukiri kuwa kuna changamoto kadha wa kadha ambazo kwa
namna yoyote zinapaswa kushughulikiwa ipasavyo ili kufanikisha kwa uhakika
riwaya ya Kiswahili kutumika kufundishia historia. Changamoto hizi zinajadiliwa
katika sehemu hii kama ifuatavyo:

Mosi, uhaba wa kupatikana kwa riwaya zilizochapishwa kale. Hili ni tatizo kubwa
kwani miongoni mwa riwaya zinazobeba uhistoria ni zile zilizoandikwa zamani na
zikazingatia usawiri wa hali halisi ya wakati. Riwaya hizi nyingi hazipo katika
mzunguko na zinapatikana kwa watu wachache sana. Kutokana pia na mahitaji
yake kuwa ni kidogo hata wachapishaji wapya hawaoni haja ya kununua au kuomba
idhini ya kuchapisha upya riwaya hizo. Hivyo basi, ili riwaya zitumike kufundishia
historia ya Tanzania katika ukamilifu, kuna haja ya kufanya mipango ili riwaya hizi
ziweze kuchapishwa tena. Ni matarajio yetu kwamba jambo hili likiwekwa katika
mitalaa halitakuwa tatizo kuwapata wachapishaji.
Pili, kupuuzwa au kufifia kwa uandishi wa riwaya za kihistoria. Nchini Tanzania
waandishi wengi hawajishughulishi na uandishi wa riwaya zilizoegemezwa katika
matukio mengi ya kihistoria au matukio halisi. Hali hii ni tofauti na nchi nyingine
ambapo hata wataalamu kama vile wanajeshi wanapotoka katika vita fulani
ambavyo wameshiriki huandika masimulizi. Masimulizi haya baada ya muda fulani
huweza kuwa nyaraka muhimu za kufundishia historia. Pia hata kwa waandishi
ambao huandika kwa kutegemea kupata taarifa kutoka kwa wastaafu ambao kwa
namna fulani wana taarifa za msingi kuhusu tukio fulani la kihistoria, huwa
wanakuwa na ugumu wa kutoa ushirikiano kwa kuhofia kutoa siri za serikali.
Masimulizi mengi ya kihistoria yamefanywa na wageni tena mara nyingine
yameandikwa kwa lugha za kigeni. Hivyo basi, kuna haja ya kuwahamasisha
waandishi ikiwa ni pamoja na kutoa semina ya namna bora ya kuandika riwaya ya
kihistoria.
Tatu, changamoto ya viwanda vya uchapishaji nchini Tanzania. Kuna changamoto
kubwa ya miswada mbalimbali ya waandishi kupata mchapishaji aliye tayari
kuchapisha. Si kutokana na kuwa miswada hiyo haina ubora bali kinachoangaliwa
ni pamoja na hofu ya kukosa soko baada ya muswada unaohusika kuwa kitabu.
Pamoja na hayo, viwanda vya uchapishaji Tanzania huchapisha kwa gharama
kubwa ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Kenya. Hivyo
basi, changamoto hii inaweza kutatuliwa kwa kuhakikisha kuwa vitabu
vinavyotarajiwa vitakuwa na soko la uhakika. Hili litaonekana tu pale
vinapoingizwa katika mitalaa. Kwani wachapishaji wengi wamejikita zaidi
kuchapisha vitabu vinavyopatikana katika mitalaa ya ngazi mbalimbali za elimu.
Nne, ni changamoto juu ya hali ya usomaji nchini Tanzania. Kwa hakika riwaya ni
utanzu unaohitaji mazingira bora ya usomaji. Licha ya ukweli huu ni muhimu
kutambua kuwa mazingira ya usomaji na hali ya usomaji Tanzania siyo ya
kuridhisha. Kwa mfano, katika uzoefu wa kufundisha na kusoma fasihi katika shule
za sekondari, wanafunzi wengi hawasomi riwaya zinazohusika kutokana na sababu
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uvivu wa kusoma. Wanafunzi hawa wengi wanasoma tahakiki tu ili waweze kufaulu mitihani yao ya fasihi. Kama hali ya
usomaji wa riwaya ni duni hata kwa wanafunzi wanaosoma fasihi, itakuwaje sasa
kwa wale ambao hawasomi fasihi? Hivyo basi, mikakati madhubuti inahitajika kwa
ajili ya kuboresha mazingira ya usomaji pamoja na hali ya usomaji nchini Tanzania.
Hii inaweza kufanyika ikiwa ni pamoja na kuhamasisha usomaji kwa njia ya
kugawa vitabu vya bure, kuweka mashindano ya usomaji vitabu, viongozi wa
kiserikali na kisiasa kuifanya kuwa ajenda yao na mwisho kuleta mabadiliko kwa
watoto wadogo.
6.0 Hitimisho
Makala haya katika mjadala w

Riwaya za Kihistoria.

Riwaya za kihistoria ni tanzu za kimasimulizi ambazo huunda na kuitengeneza
historia kwa njia ya ubunifu. Ubunifu huu unajitokeza kupitia wahusika wa kubuni
au wahusika halisi ambao wameinuliwa kidogo katika namna ya utendaji wao
kuliko hali halisi. Pia, ubunifu huo unaweza kujitokeza kupitia utumiaji wa matukio
halisi ya kihistoria lakini yakaongezewa na wahusika wa kubuni pamoja na matukio
mengine yanayokusudia kuweka msisitizo wa ujenzi wa idili muhimu ya jamii kwa
kipindi hicho cha wakati (Mlaga, 2011; Gupta, 2007). Kundi hili la aina hizi za
riwaya katika fasihi ya Kiswahili limegawanyika katika makundi matatu. Msingi
wa mgawanyo huu ni kama ambavyo Tuner aliweka mgawanyo huu ili kukabiliana
na utata wa kubainisha sifa za riwaya za kihistoria. Makundi haya ya riwaya za
kihistoria ni pamoja na riwaya wazi (documented), riwaya fiche (disguised) na
riwaya za kubuni (invented). Aina hizi za riwaya za kihistoria zinafafanuliwa zaidi
moja baada ya nyingine katika mtiririko ufuatao:
Mosi ni riwaya wazi, hii ni aina ya riwaya ya kihistoria ambayo inatambulika kama
riwaya ya kihistoria hasa. Hii ni aina ya riwaya ya kihistoria inayojulikana kuwa ni
kongwe. Kimsingi aina hii ya riwaya ya kihistoria kwa sehemu kubwa hujitahidi
kuendana kwa ukaribu na vitabu vya historia. Katika aina hii ya riwaya mara nyingi
huhusisha watu na matukio halisi ya kihistoria. Pamoja na hivyo, riwaya za aina hii
huhakikisha msuko wake wa matukio ni wa kihistoria. Wahakiki wengi akiwemo
Mulokozi (1990) anaitazama aina hii ya riwaya kama ndio riwaya halisi ya
kihistoria.
Riwaya za aina hii zilifungamanishwa na falsafa kongwe ya historia ambayo
iliegemea katika imani juu ya ukweli mkamilifu, ukamilifu wa historia, usawiri wa
matukio kama yalivyotokea, kuitenganisha historia na ubunilizi, na kuikamilisha
historiografia ya kipindi husika. Sifa hizi zilikusudia kuitenganisha historia na
fasihi, jitihada hizi zilifanyika kuanzia mwishoni mwa karne ya kumi na nane kama tulivyobainisha.

Haikuwezekana kuitenga historia na fasihi kwa muda mrefu sana, kwani ilipofika
mwishoni mwa karne ya 19, ilionekana dhahiri kwamba vigezo vilivyowekwa
kuitofautisha historiografia na fasihi havitekelezeki (Braitenthaller, 2008).
Pamoja na hayo, aina hii ya riwaya ya kihistoria imekuwa na mabadiliko ya msingi.
Kwani kwa zama hizi si lazima sifa za riwaya wazi zote zijitokeze kwenye riwaya
zote za kihistoria. Riwaya ya kihistoria inaweza kuwa na sifa moja tu kati ya hizi
tulizozitaja. Mabadiliko haya, yamechochewa na mabadiliko ya falsafa ya historia
kutoka falsafa kongwe ya historia, mpaka falsafa ya historia ya zama hizi. Falsafa
hii mpya inaiangalia historia kama kitu kisichokuwa na ukweli mkamilifu, chenye
kubeba mapendeleo, kisichokuwa na ukweli wa aina moja, na kisichojitosheleza
kiushahidi. Katika makala haya, tumezingatia falsafa zote mbili za historia. Falsafa
hizi ni ile falsafa kongwe ya historia kwa upande mmoja, ambayo ndio msingi wa
riwaya kongwe za kihistoria , na kwa upande mwingine, ni falsafa ya historia za
zama hizi, ambayo kimsingi haiegemei katika kusisitiza usayansi wa historia na
jitihada za kutenganisha historia na fasihi.
Pili ni riwaya fiche (disguised), hizi ni riwaya za kihistoria ambazo hazihusishi
kwa uwazi matukio na watu halisi wa kihistoria. Licha ya kutobainisha wazi
matukio na watu halisi wa kihistoria, jambo linaloifanya aina hii ya riwaya
kuonekana kwamba ni ya kihistoria ni ushahidi wa kutosha ambao unamwonesha
mwandishi kuonesha shauku yake juu ya historia. Mwandishi huweza kuandika
historia fulani kwa ufiche ikiwa ni pamoja na kukwepa hali ya udhibiti kutoka
katika mamlaka. Kwa mfano, katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo kuna tukio
la kijana Tumaini kuamua kumpiga risasi mkuu wa wilaya kama hatua mojawapo
ya kuonesha kukerwa na namna ambavyo siasa ya Ujamaa ilivyoathiri maisha yake
kwa kumnyang’anya mali zake ambazo amezipata kwa tabu. Tukio kama hili
Wamitila (2003), analitafsiri kuwa ni tukio fiche la kihistoria linalorejelea historia
halisi ya Kupigwa kwa risasi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Kleruu na
mkulima aliyejulikana kwa jina la Mwamwindi. Tamthiliya ya Kaptula la Marx
nayo inaelezwa kubeba historia halisi kwa namna ya uficho. Riwaya za Shaaban
Robert kama vile Kufikirika na Kusadikika nazo zinaweza kutazamwa kama
zinazoeleza historia halisi ya kipindi cha ukoloni kwa namna ya uficho. Msingi wa
riwaya za namna hii ni pamoja na muktadha wa uandishi wake ambao husaidia
kubaini uhistoria katika riwaya inayohusika.
Tatu, ni riwaya ya kubuni (invented). Katika aina hii ya riwaya, wahusika na
matukio yanayosimuliwa yanakuwa ni ya kubuni tu. Kutokana na hali hiyo,
uhusiano wa mwandishi na kazi yake unakuwa ni kigezo muhimu sana katika kuifanya riwaya inayohusika kuwa ya kihistoria.

Fasihi na Historia.

Pamoja na uhusiano huo wa muda mrefu, ni vema ikatambulika kwamba
zimekuwepo harakati kadhaa za kutaka kuifuta kabisa historia hii ya uhusiano huo.
Wataalamu wa pande hizi mbili, kila upande kwa malengo yake katika kipindi
fulani cha wakati, walifanya majaribio kuondosha au kuufuta kabisa uhusiano huu.
Kwa upande wa wanafasihi walisukumwa na haja ya kuiona fasihi ikitambuliwa
kama utanzu unaojitegemea. Hii inatokana na ukweli kwamba kabla ya karne ya
ishirini, fasihi iliwekwa katika kapu moja na falsafa na historia. Jambo hili
lilionekana kama fedheha kwa wanafasihi ili kuondokana na kadhia hii, harakati
kadhaa za kuitofautisha fasihi na nyanja nyingine zilifanyika ili kudhihirisha kuwa
fasihi nayo inajitegemea na wala haihitaji kukamilishwa na nyanja nyingine.
Miongoni mwa harakati hizo ilikuwa ni pamoja na kuibua mikabala ya uhakiki
ambayo mielekeo yake ilikuwa ni kuiangaza kazi ya fasihi tu na wala si kuihusisha
na mambo mengine nje ya kazi ya fasihi5
.
Kwa upande wa wanahistoria nao, hawakuwa nyuma katika kufanya majaribio6
ya
kuitenga historia na fasihi. Kwa mawazo yetu, haja ya wanahistoria ya kujitenga na
fasihi ilitokana na dhana hasi iliyofungamanishwa na maana ya fasihi. Dhana hii
hasi ni kuhusu fasihi kutazamwa kama kitu cha kubuni na kufikirika7
. Kutokana na
maana hii fasihi ilionekana ni jambo ambalo si sahihi hata kidogo kuilinganisha na
historia ambayo ilionekana kukaribiana zaidi na sayansi ambayo haiegemei katika

2Hii ina maana kwamba wanahistoria na wanafasihi wote kwa pamoja wanapoandika historia
hutawaliwa na ulazima wa kuiumba upya historia husika kutegemeana na Idili za jamii
zinazotawala kwa kipindi husika.
3 Bentoncini (1987) anapojadili kazi bunilizi katika kipindi cha ukoloni nchini Tanganyika
(baadaye Tanzania). Anazitaja kazi za Habari za Wakilindi na Khabar al- Lamu au Habari za
Lamu ambazo ni historia za jamii mbili tofauti.
4 Tazama Mlaga (2011: 17).
5 Kuibuka kwa nadharia ya umbuji, uhakiki mpya, na hata baadhi ya mikabala ya kimuundo ni
sehemu ya harakati za kuthibitisha kuwa uga wa fasihi ni taaluma inayojitegemea na kujitosheleza.
6 Tunayaita kuwa ni majaribio kwa sababu hayakufanikiwa. Wanahistoria wengi leo hii wanakiri
juu ya mfanano uliopo kati ya historia na fasihi hususan katika masuala ya mbinu za kiuandishi na
hata juu ya dhana ya ubunaji.
7 Dhana hizi mbili zinatokana na maneno mawili ya Kiingereza ‘Fictious and Imaginative’. Kwa
maelezo zaidi juu ya athari ya fasihi kutazamwa katika msingi wa maana hii soma Blackwell Guide to literary theory(K,5-8).

Mambo ya kubuni na kufikirika. Usayansi huu wa historia8
uliegemezwa katika hoja
inayodai kwamba historia haina ubunaji, haina ukadiriaji wa matukio (haipunguzi
wala haiongezi). Hii ina maana kwamba usayansi wa historia umeegemezwa katika
namna ya uandishi wa historia.
2.3 Makubaliano ya Pamoja kati ya Wanahistoria na Wanafasihi
Baada ya kuziona harakati hizi za kila upande kujitenga na upande mwingine,
kunaweza kuibua swali la kwamba je, ni lini wataalamu wa pande hizi
wamekubaliana kuona uhusiano uliopo miongoni mwa nyanja hizi? Kimsingi kama
tulivyobainisha misingi ya uhusiano wa nyanja hizi mbili hapo juu, wataalamu wa
pande hizi mbili baada ya kipindi fulani cha wakati walipitia upya mtazamo wao
kuhusu uwanja uliohusika na mahusiano yake na uwanja mwingine (fasihi au
historia). Kwa upande wa fasihi, Nadharia ya Uhistoria Mpya9
ndiyo
inayofungamanishwa na kuihusianisha fasihi na historia. Mlaga (2011),
anatanabahisha kwamba wafuasi au waumini wa nadharia hii wanaupitia upya
mpaka uliopo kati ya historia na fasihi. Lengo la kuupitia upya mpaka kati ya fasihi
na historia linaelezwa vema na Mushengyezi (2003:94) anasema:
One of the major concerns of the New Historicism is to redraw the boundaries of history
as a discipline. New Historicists argue that it is misleading to compartmentalize history
and literary studies, or even to hierarchies one over the other: that is to present them as
independent disciplines, one real and the one fictional.
Jambo kuu moja ambalo wanauhistoria mpya wanalishughulikia ni kuweka mpaka upya
wa taaluma ya historia. Wanauhistoria mpya wanadai kwamba kuitenganisha historia na
fasihi au kuzipanga kwa kuzingatia ipi ni kuu ni upotoshaji. Hii ni sawa na kuzifanya
kuwa taaluma mbili zinazojitegemea, taaluma moja ikiwa inashughulika na uhalisi na
taaluma nyingine inashughulika na ubunaji (Tafsiri yangu).
Dondoo hili, linapoeleza juu ya nia ya kuupitia upya mpaka kati ya fasihi na
historia, inarejelea mpaka uliokuwa umewekwa na wanaumbuji, Wanauhakiki
Mpya, na hata Wanaumuundo leo10. Katika mikabala hii ya kinadharia mkazo
uliwekwa katika kuitofautisha kazi ya fasihi na nyanja nyingine na fasihi ikiwemo.
Pia, Wanauhistoria Mpya wanadai kwamba mambo mbalimbali katika historia
yanavuka mipaka ya kiwakati na kimaudhui. Ukweli huu unalifanya jambo
lililotokea karne ya 18 kuwa na umuhimu katika karne ya 21. Ukweli huu
unadhihirika kwa hakika iwe ni katika historia au katika fasihi. Hivyo basi, kwa kuegemea katika mkabala huu, tunajiridhisha pasipo shaka kuwa wanafasihi
(baadhi) wanakubali kwa hakika kwamba kuna uhusiano wa karibu kati ya fasihi na
historia.
Kwa upande wa historia, pia kuna makubaliano walau yanayoonesha kuwa
wanahistoria wanatambua uhusiano uliopo kati ya fasihi na historia. Baadhi ya
wanahistoria walianza kuutazama upya mtazamo wao wa kuiona historia kama ni
sayansi. Kwa mfano, E.H.Carr katika kitabu chake cha What is History (1961)
kama anavyonukuliwa na Gupta (2007) anadai kuwa historia si taaluma
inayoonekana kama iliyotuama (haibadiliki). Mtaalamu huyu aliamua kuifasili
historia kama mchakato endelevu wa mwingiliano kati ya mwanahistoria na ukweli
wake (uhalisi), na mjadala usiokwisha kati ya wakati uliopo na wakati uliopita. Hali
hii inaonesha kwamba historia huangaliwa kwa namna tofauti kadiri wakati
unavyopita; na hii inaonesha kwamba historia hubadilikabadilika.
Kukosekana kwa usayansi wa historia kunadhihirishwa zaidi na Levi Straus katika
kitabu chake The Savage Mind kama anavyonukuliwa na Gupta, (2007:25) kuwa:
… Historical facts are not given (original italics) facts as it is the historian or the agent of
history ‘who constitutes them by abstraction’. The construction of historical facts is thus
the matter of selection and point of view.
Data za kihistoria siyo kwamba hupatikana zikiwa tayari zimekamilika, kwani huwa ni
wajibu wa mwanahistoria mwenyewe kuzitengeneza kutokana na malengo au madhumuni
yake. Hivyo basi utengenezaji wa data za kihistoria hutawaliwa zaidi na mapendeleo na
mtazamo wa mwanahistoria mwenyewe (Tafsiri yangu ).
Dondoo hili linatupilia mbali hoja yoyote inayokusudia kuitenga fasihi na historia.
Historia na fasihi, kwa namna fulani, huhusiana katika ukadiriaji na ubunaji, hali
ambayo hujitokeza hasa pale kunapokuwa na haja ya kuziba mapengo kadhaa
yanayotokana na kukosekana kwa taarifa zinazohitajika.

8.Hoja hii imebainishwa katika maandiko ya Bury (1903) na Atoon (1902) kama wanavyonukuliwa
na Gupta (2007:5)
9. Uhistoria Mpya ni nadharia iliyoshika kasi katika miaka ya 1980, waasisi wake wakiwa ni Stephen Greenblatt na Michel Focault.Tazama Mlaga( 2011)

Riwaya za Kiswahili katika ufundishaji wa historia.

Riwaya ya Kiswahili kwa muda mrefu sasa imepewa nafasi kubwa na ya muhimu
katika div classmitalaa ya elimu katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki. Ni kuanzia
shule za sekondari hadi katika ngazi za elimu ya juu. Ina maana kwamba riwaya ya
Kiswahili imekuwa na dhima muhimu katika jamii pana ya

1 Makala haya mwanzo wake ni katika utafiti wa kuandaa tasnifu ya shahada yangu ya uzamili au
umahiri. Pamoja na hayo yamefanyiwa mabadiliko kadhaa.
Afrika Mashariki. Kwa mfano, miongoni mwa dhima za fasihi ambazo hubainishwa
ni pamoja na kuhifadhi historia ya jamii. Pamoja na ukweli huo, dhima hii huwa
haipati nafasi ya kuelezwa kwa kina. Pia, wakati mwingine mtazamo huu huweza
kuifanya historia kuonekana kama maarifa yaliyotuama na yanayopaswa kuelezwa
jinsi yalivyo bila kuongezwa au kupunguzwa katika utanzu wa riwaya. Hivyo basi,
kuna haja ya kuitumia riwaya ya Kiswahili kwa ukamilifu katika kuonesha dhima
hii ya fasihi kama dafina ya historia. Pamoja na hayo, kuna umuhimu wa kupanua
matumizi ya riwaya ili yasiishie kwa wanafunzi tu wa fasihi bali iwe pia kwa
wanafunzi wa historia na mtu yeyote aliye na haja ya kujifunza historia huku pia
akifurahia utamu wa riwaya ya Kiswahili. Ili kufanikisha malengo haya, makala
haya yanajikita katika kuhalalisha kwanza namna ambavyo riwaya inastahili kabisa
kuaminika kama nyenzo muhimu ya kuweza kufundishia maarifa ya historia bila
tatizo. Ili kuondoa woga wowote wa riwaya kutoaminika katika sehemu inayofuatia
tunajadili misingi ya riwaya kuweza kukubalika kuwa inafaa kutumika katika
kufundishia historia.
2.0 Misingi ya Riwaya Kuweza Kutumika Kufundishia Historia
Kuna misingi kadhaa inayotufanya tuweze kuitazama riwaya kama chombo
kinachofaa kutumika kufundishia historia. Misingi hii inabainisha kwa nini riwaya
na aina ipi ya riwaya inayofaa kutumika kufundishia historia. Sehemu hii inajibu
swali la kwa nini riwaya inajitosheleza kutumika kufundishia historia kwa ngazi
zote za elimu? Misingi hii inaainishwa na kujadiliwa katika sehemu hii inayofuatia.
2.1 Uhusiano wa Muda Mrefu kati ya Fasihi (riwaya) na Historia
Utanzu wa riwaya na uwanja wa historia vimekuwa na uhusiano wa muda mrefu
sana. Uhusiano huu unajitokeza hata katika maelezo ya Gupta (2007:1) anaposema:
The connection of history with literature is well known. In order to begin the present
project is essential to trace the importance of this relationship. Among the various literary
forms, the connection of the novel with history…
Muunganiko wa historia na fasihi unafahamika vema. Ili kuanza kazi hii ni muhimu kuutalii
umuhimu wa uhusiano huu. Kati ya tanzu mbalimbali za fasihi, muunganiko kati ya riwaya
na historia… (Tafsiri Yangu).
Dondoo hili linathibitisha hoja yetu kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya Fasihi na
Historia. Pia, katika kuangalia uhusiano huu ndipo itakapodhihirika ni kwa namna
gani riwaya zinafaa kutumika kufundishia historia. Katika kuangalia uhusiano huu
wataalamu mbalimbali (Gupta: 207; Mlaga, 2011) wanabainisha sababu za
mahusiano haya kuwa; Mosi, riwaya iliweka misingi yake katika kuiga kutoka
katika historia. Pili, dhana hizi mbili zinachangia muktadha wa kijamii,
kiutamaduni, kiitikadi pamoja na mbinu nyingine rasmi. Tatu, riwaya iwe ya
kihistoria au la, hujihusisha kikamilifu na historia. Nne, utanzu wa riwaya na historia vinategemea katika msingi wa  uumbaji upya wa historia kutegemeana na idili ya wakati wa uandishi.
Tano, hapo awali historia na fasihi zilikuwa
zimeungana.
Mwisho ni hoja ya mwanahistoria mkongwe Giambattista Vicco
(1668-1744) ambapo alibaini kuwa tendi za mshairi Homer (Illiad na Odyssey)
zinaeleza historia.
Hivyo basi, hoja hizi kimsingi zinaleta kwa pamoja utanzu wa fasihi na hisoria.

Dhana Ya Fasihi.

Fasihi kwa ujumla wake ni sanaa ya kutumia lugha ili kuwakilisha wazo fulani kwa hadhira kusudiwa. Hivyo tunaposema kuwa fasihi ni sanaa ya lugha inamaana kuwa fasihi huipamba lugha ya kawaida kuonekana isiyo ya kawaida ili kuwavutia watu na kuwakosha kihisia (Samweli, 2015). Fasihi imegawanyika katika tanzu kuu mbili, ambazo ni fasihi simulizi na fasihi andishi, Kazi hii itajikita hasa katika fasihi simulizi.
Fasihi sumulizi kama utanzu wa fasihi ulianza tangu kuwepo kwa mwanadamu. Mwanadamu asingeweza kuishi vyema katika mazingira yake kijamii bila kuwasiliana, na ili kuwasiliana alihitaji lugha. Lugha ilitumika pia katika maburudisho mbalimbali na huo ndio ukawa mwanzo wa fasihi pia. HIvyo utanzu huu wa fasihi ulianza tangu kuwepo kwa mwanadamu. Utanzu huu hutumia lugha ya masimulizi katika kufikisha ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Kwa hali hii basi Fasihi simulizi ni utanzu wa fasihi utumiao lugha ya masimulizi yamdomo kujikamilisha kidhima (Mnenuka, 2011).

Uainisho wa tanzu za fasihi simulizi na vipera vyake umezungukwa na utata mkubwa. Uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi umekuwa moja ya mambo magumusana katika fasihi hiyo. Ugumu wa uainishaji wa tanzu hizo hutokana na mambo kadhaa. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na yafuatayo;
Kuna vigezo vingi vinavyoweza kutumika katika uainishaji wa tanzu hizo. Vigezo hivi hutofautiana kutoka mwanazuoni mmoja hadi mwingine. Mfano wengine husema kuwa uainishaji huangalia umbile na tabia, na wengine huangalia majina ya tanzu na miundo yake.
Pia tanzu za fasihi simulizi ni nyingi na hutofautiana kati ya jamii na jamii. Kila jamii ina tanzu zake za fasihi simulizi ambazo zinaweza kuwa tofauti na tanzu za jamii nyingine. Inawezekana tanzu Fulani ikawepo katika jamii Fulani lakini isiwepo katika jamii nyingine au inaweza kuwepo lakini ikawa na tabia tofauti kabisa. Mfano katika jamii ya wasukuma na wahaya kuna majigambo ya wanawake (Samweli, 2015).
Tanzu hizo huingiliana, katika fasihi simulizi ni kawaida kwa tanzu kuingiliana, mfano methali huweza kuwa hadithi na hadithi kuwa methali. Hivyo, huwa vigumu kuiainisha tanzu hiyo.
Tanzu za fasihi simulizi hubadilika badilika kutegemeana na muktadha wa utendaji na wakati. Tanzu mpya huweza kuibuka na za zamani kufa. Hivyo ni vigumu kueleza kuna tanzu ngapi za fasihi simulizi labda pia itajwe uainishaji huo ni kwa wakati gani. Mfano utanzu wa nyimbo na kipera cha majigambo ya bongo freva liokuja miaka ya 1980 na kuendelea na kabla ya hapo haukuwepo.
Tanzu na vipera vya fasihi simulizi ni nyingi mno. Tofauti na fasihi andishi yenye tanzu na vipera vichache. Muda mrefu unahitajika kuzitafiti na kuziainisha kwa usahihi katika jamii mbalimbali za Kiafrika.

Fani za Uandishi/Kisanaa.

Hizi ni mbinu za Kiufundi zitumikazo na mwandishi/msimulizi wa kazi yoyote ya fasihi ambayo humlazimisha msomaji/hadhira kuisoma hadithi nzima ili kuzitambua.
Baadhi yazo ni kama vile:

  • Sadfa-Hii ni hali ambapo matukio hutendeka kwa pamoja bila ya kupangwa.
  • Kisengerenyuma-Hapa mwandishi hurejelea matukio yaliyofanyika nyuma.Hivyo humlazimu kubadilika wakati kuyasimulia tena.
  • Kisengerembele-Hapa mwandishi husimulia mambo yatakayotokea siku za halafu kwa kubadilisha wakati wa masimulizi.
  • Njozi-Hapa mwandishi hutumia ndoto kujaribu kufichua yaliyotendeka/yatakayotokea katika masimulizi/hadithi yake.
  • Upeo wa juu-Hapa mambo hufanyika kulingana na matakwa ya hadhira.
  • Upeo wa chini-Hapa mambo hufanyika kinyume na matarajio ya hadhira.Mara nyingi hutokea baada ya upeo wa juu.
  • Kinaya-Hii ni hali ambapo mambo hufanyika kinyume na matarajio katika hadithi.
  • Kejeli-Hapa kuna matumizi ya maneno ya dharau kwa madhumuni ya kukashifu kitendo fulani/mtu fulani katika hadithi.
  • Taharuki-Hii ni hali matukio ya hadhira/masimulizi humwacha msomaji/hadhira kinywa wazi na kumpatia hamu ya kutaka kusoma zaidi.Aghalabu hujitokeza paruwanja mwishoni mwa hadithi.