Aina za Shamirisho/Yambwa.

Shamirisho ni nomino katika sentensi inayoonyesha/inayoashiria mtendwa/kitendwa na mtendewa/kitendewa.Kuna aina tatu za shamirisho.

 1. Shamirisho Kipozi/Yambwa Tendwa.
 2. Shamirisho Kitondo/Yambiwa/Yambwa Tendewa.
 3. Shamirisho Ala/Kitumizi.

Shamirisho Kipozi.Hii ni nomino inayoathiriwa na kitenzi katika sentensi kwa njia ya moja kwa moja.K.m Mchezaji alipiga mpira.Shamirisho Kitondo.Hii ni nomino isiyoathirika na kitendo kwa njia ya moja kwa moja.K.mMtoto alimjengea mama nyumba.Shamirisho Ala.Hii ni nomino inayoonyesha kifaa kifaa kilichotumika kufanya kitendo.K.m Mkulima alilima shamba kwa jembe.(Maneno yaliyoandikwa kwa wino wa kukoleza ndio shamirisho)

Aina Za Ndege.

 1. Dudumizi/Shundi/Gude/Tipitipi-Huyu ni aina ya ndege asiyejenga kiota.
 2. Kanga-Huyu ni kuku wa porini aliye na madoadoa meupe.
 3. Kasuku-Ndege aliye na rangi nyingi za kupendeza na hodari wa kuiga.
 4. Kigotago-Ndege ambaye hupigapiga mti kwa mdomo ili kupata vidudu.
 5. Hondo-Ndege aliye katika jamii moja ya shundishundi aliye na maji ya kunde na hupaza sauti kwa kawaida yake.
 6. Chozi-Ndege mdogo aliye na rangi ya manjano.
 7. Chiriku-Ndege mdogo ambaye hupiga kelele nyingi sana.
 8. Keremkeremu-Ndege ambaye hupenda sana kula nyuki.
 9. Korongo-Ndege aliye na miguu mirefu na shingo ndefu.
 10. Kware-Ndege mdogo kuliko kuku aliye na miguu myekundu na na mwili hudhurungi.
 11. Mbuni-Huyu ni ndege anayekwenda kwa kasi na ambaye ni kubwa na hana uwezo wa kuruka.
 12. Mnandi-Ndege mkubwa mwenye shingo ndefu,miguu mifupi mithili ya bata, tumboni ana rangi nyeupe na hupenda kuishi majini kuwinda samaki.
 13. Minga-Ndege mwenye rangi kijani,miguu myekundu,hula nazi na hupatikana katika jamii ya tetere.
 14. Njiwa-Ndege ambaye hufugwa nyumbani na huwa katika jamii ya tetere.
 15. Sigi-Ni ndege mdogo aliye na manyoya meusi kichwani na rangi ya kijivu kifuani.
 16. Shakwe-Ndege wa pwani anayefafana na membe na anayependa kula samaki.
 17. Tetere-Ndege mdogo mwenye rangi ya kijivujivu,hufafana na njiwa.
 18. Yangeyange/Dandala-Ndege mweupe na ana kishungi.
 19. Tongo-Hili ni jina la jamii la ndege wadogo warukao katika makundi.
 20. Mumbi-Ndege mkubwa anayeaminika kuleta msiba kila mahali aendapo.
 21. Kirumbizi-Ndege mdogo mwenye mkia mrefu na ushungi, hupiga kelele alfajiri.
 22. Kunguru-Ndege mweusi ambaye mara nyingi huwa na doa jeupe shingoni.
 23. Kipanga-Ndege ambaye hula wanyama na ndege wadogowadogo.
 24. Batabukini-Huishi zaidi majini,ni sawa na bata.
 25. Bata-Ndege anayependa matope.Ni mkubwa wa kuku.

Aina za Viambishi.

Kuna aina mbalimbali ya viambishi kama ifuatavyo.

 1. Viambishi awali-Hivi ni viambishi vinayopachikwa/kuambatanishwa kabla ya mzizi wa kitenzi.K.m a-na-pik-a.a-na ni viambishi awali.
 2. Viambishi tamati-Hivi ni viambishi vinayopachikwa/kuambatanishwa baada ya mzizi wa vitenzi.K.m a-na-kul-a.a ni kiambishi tamati.

Dhima ya viambishi.Viambishi Awali.

 • Huonyesha nafsi, wakati na idadi.K.m a-na-chek-a.Hapa tunapata nafasi ya tatu, umoja, wakati uliopo,hali ya kuendelea.
 • Huonyesha uyakinishi/ukanushi.K.m a-naongea katika hali ya uyakinishi na ha-taongea katika hali ya ukanushi.

Viambishi Tamati

 • Hukamilisha maana ya neno.K.m a-na-kimbi haina maana bila kiambishi tamati a.
 • Huzalisha maneno mapya.K.m anapiga,anapigana

Aina za vihusishi.

Vihusishi ni aina ya maneno yanayoonyesha uhusiano baina/kati ya neno moja na jingine.Kuna aina mbalimbali za vihusishi kulingana na utendakazi wao.Dhima za vihusishi ni kama zifuatazo.

 • Hutumika kuonyesha uhusiano kiwakati.K.m Wanafunzi walienda darasani baada ya kusikiliza hotuba ya mwalimu mkuu.
 • Hutumika kuonyesha uhusiano wa mahali.K.m Walitembea kando ya barabara.
 • Hutumika kuonyesha uhusiano wa umilikaji.K.m Wageni waliokuja kwangu wameondoka.
 • Hutumika uhusiano wa sababu.K.m Polisi walimkamata kwa ajili ya wizi.
 • Hutumika kuonyesha uhusiano wa kulinganisha.K.m Yeye alipata alama ishirini zaidi ya mimi.

Kutokana na dhima za vihusishi tunapata aina zifuatazo za vihusishi.

 1. Vihusishi vya sababu
 2. Vihusishi vimilikishi
 3. Vihusishi vya kulinganisha
 4. Vihusishi vya kifaa/chombo/ala
 5. Vihusishi vya namna
 6. Vihusishi vya mahali
 7. Kihusishi ‘na’ cha mtenda

Aina za viunganishi.

Viunganishi ni aina ya maneno yanayotumika kuunganisha neno moja na jingine, sentensi moja na nyingine au kujaribu kuonyesha uhusiano kati ya dhana mbili au zaidi.Kuna aina mbalimbali za viunganishi kulingana na utendakazi wao katika sentensi.

 1. Vya kuonyesha sababu-Mifano ni kama vile madhali, maadamu,kwa minajili ya, kwa kuwa,ili, kwani, kwa vile n.k.K.m Mwanafunzi huyu hakuja shuleni jana madhali alikuwa mgonjwa.
 2. Vya kuonyesha masharti-Mifano ni kama vile ikiwa, iwapo, muradi n.k.K.m Ikiwa utasoma kwa bidii utafaulu.
 3. Vya kuonyesha tofauti-Mifano ni kama vile minghairi ya, lakini,ila,japo, ijapokuwa, ingawa,bali, bila, ingawaje, dhidi ya, ilhali, kinyume na n.k.K.m Tulifika salama nyumbani japo mvua ilikuwa ikinyesha.
 4. Vya kujumuisha-Mifano ni kama vile licha ya, aidha, pia, fauka ya, isitoshe, zaidi ya, pamoja na, vilevile, mbali na n.k Tulishinda mechi ile licha ya kulemewa vipindi vyote viwili vya mchezo.
 5. Vya kulinganisha-Mifano ni kama vile vile,kuliko,sawa na,kefule, sembuse,seuze, kulingana na n.k.K.m Bwana yule alimla kuku mzima sembuse kifaranga.
 6. Vya kuonyesha mfuatano wa matukio-Mifano ni kama vile kisha,halafu n.k.Alikula kisha akanywa maji.
 7. Vya kuonyesha uwezekano-Mifano ni kama vile labda, pengine,au, ama, huenda n.k.K.m Ama Kiswahili au Kiingereza ndio lugha bora kwake.

Aina za virai.

Kirai ni kipashio cha kimuundo kinachoundwa kwa neno moja au zaidi ambacho hakina muundo wa kiima na kiarifu.Kuna aina mbalimbali za virai kama zifuatazo.

 1. Kirai Nomino(KN)-Hiki ni kifungu cha maneno ambacho neno lake kuu ni nomino.K.mVijana kwa wazee walihudhuria mkutano wa jana.
 2. Kirai Kitenzi (KT)-Hiki ni kifungu cha maneno ambacho neno lake kuu ni kitenzi.K.m Kucheza kwetu kuliwafurahisha walimu.
 3. Kirai Kivumishi(KV)-Hiki ni kifungu cha maneno ambacho neno lake kuu ni kivumishi.K.m Ng’ombe wanne walisombwa na mafuriko.
 4. Kirai Kiunganishi (KU)-Hiki ni kifungu cha maneno ambacho neno lake kuu ni kiunganishi.K.m Wanafunzi walisoma kwa bidii ijapokuwa hawakufaulu vema.
 5. Kirai Kihusishi (KH)-Hiki ni kifungu cha maneno ambacho neno lake kuu ni kihusishi.K.m Wanafunzi walikuwa wakitembea kando ya barabara.
 6. Kirai Elezi(KE)- Hiki ni kifungu cha maneno ambacho neno lake kuu ni kielezi.K.m Mtoto alilala kitandani kifudifudi.

Aina za viwakilishi.

Kiwakilishi ni neno linalotumika/linalosimamia nomino.Katika Kiswahili kuna viwakilishi mbalimbali kama zifuatazo.

 1. Viwakilishi vya sifa-Hutumika kwa niaba ya nomino kuonyesha sifa yake.K.m Vitamu vimeliwa.
 2. Viwakilishi vya A-Unganifu-Hutumika kwa niaba ya nomino kwa kuonyesha kinachomiliki nomino hiyo.K.m Cha mkufu mwanafu hali.
 3. Viwakilishi vya nafsi-Hutumika kwa niaba ya nafsi.Mifano yazo ni mimi, sisi, wewe, nyinyi,yeye,wao.Sisi tulikula tukashiba.
 4. Viwakilishi vya virejeshi-Hutumia amba- rejeshi au O-rejeshi kurejelea nomino.K.m Kinachotafutwa hakipatikani?
 5. Viwakilishi vya idadi-Hapa kuna makundi mawili.Kuna vile vya idadi kamili.K.m Wawili ndio walikuja mkutanoni.Pia kuna vile vya idadi isiyodhihirika.K.m Wengi walionyesha ukakamavu.
 6. Viwakilishi viashiria-Hutumika kurejelea nomino bila kutaja.K.m Haya,hayo, yale.Yale yamenywewa na ng’ombe kitambo!
 7. Viwakilishi visisitizi-Hivi hutumika kutulia mkazo nomino kwa kurudiarudia kiashiria chake.K.m Wawa hawa ndio waliokamatwa mwaka uliopita.
 8. Viwakilishi vimilikishi-Hivi hutumika kwa niaba ya nomino kwa kutumia vimilikishi.K.m -angu,-etu,-ako,-enu,-ake,-ao.k.m Wangu wamelala.

Aina za mashairi.

Kuna aina mbalimbali za mashairi kwa kuzingatia kigezo cha mishororo.

 • Tathmina-Hili ni shairi lenye mshororo mmoja katika kila ubeti.
 • Tathnia-Hili ni shairi lenye mishororo miwili katika kila ubeti.
 • Tathlitha-Hili ni shairi lenye mishororo mitatu katika kila ubeti.
 • Tarbia-Hili shairi lenye mishororo minne katika kila ubeti.
 • Takhmisa-Hili ni shairi lenye mishororo tano katika kila ubeti.
 • Tasdisa-Hili ni shairi lenye mishororo sita katika kila ubeti.
 • Usaba-Hili ni shairi lenye mishororo saba katika kila ubeti.
 • Unane-Shairi lenye mishororo minane katika kila ubeti.
 • Utisa-Shairi lenye mishororo tisa katika kila ubeti.
 • Ukumi-Shairi lenye mishororo kumi katika kila ubeti.

Aina za bahari ya mashairi.

Kuna aina mbalimbali za mashairi kwa kuzingatia kigezo cha bahari.

 1. Sakarani-Hili ni shairi lenye bahari zaidi ya moja.
 2. Ukara-Hili ambalo vina vya kipande kimoja hubadilika kutoka ubeti moja hadi mwingine ilhali vina vyaupande mmoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
 3. Ukaraguni-Hili ni shairi ambalo vina vya kati na vile vya mwisho hubadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
 4. Kikwamba-Hili ni shairi ambalo neno au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa ili kutanguliza mshororo au ubeti unaofuata.
 5. Mtiririko-Hili ni shairi ambalo vina vya kati vya mwisho havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi ule wa mwisho.
 6. Mathnawi-Hili ni shairi ambalo lina vipande viwili yaani ukwapi na utao.
 7. Ukawafi-Hili ni shairi ambalo lina vipande vitatu yaani ukwapi,utao na mwandamizi.
 8. Ngojera-Hili ni shairi la majibizano kati ya watu wawili.
 9. Madhuma-Hili ni shairi ambalo kipande kimoja hutoa swali na kipande kingine hutoa jawabu.
 10. Sabilia-Hili ni shairi lisilokuwa na kibwagizo.
 11. Msuko-Hili ni shairi ambalo mshororo wake wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo ya awali.
 12. Pindu/Mkufu/Nyoka- Hili ni shairi ambalo neno la mwisho/Kifungu cha maneno cha mwisho katika kila ubeti hutumika kuanza ubeti ufuatao.
 13. Utenzi-Hili ni shairi ambalo ni ndefu na lina kipande kimoja katika kila ubeti.

Aina za vitenzi.

Kitenzi ni neno linalofafanua jinsi kitendo fulani kilivyofanyika.Pia hufahamika kama kiarifa.Kuna aina mbalimbali za vitenzi kama zifuatazo:Kitenzi Kikuu/Halisi.(T)Hiki ni kitenzi kinachosheheni ujumbe muhimu wa kiarifu cha sentensi.K.m Baba anafyeka.Majukumu ya vitenzi vikuu ni:

 • Kuonyesha hali ya tendo
 • Kuonyesha nafsi
 • Kueleza tendo lililofanywa na mtenda/mtendwa
 • Kuonyesha wakati tendo lilipofanyika
 • Kuonyesha kauli mbalimbali za tendo

Kitenzi Kisaidizi.(Ts)Hiki ni kinachotoa taarifa kuhusu uwezekano,hali au wakati wa jambo kutendeka.Jukumu kuu ni kupiga jeki kitenzi Kikuu kufikisha ujumbe.K.m Anapaswa kusoma, alikuwa anapika, alitaka kufyeka n.kVitenzi visaidizi lazima vitumike na vitenzi halisi kwa kuwa hubeba viambishi vya wakati.Kitenzi Kishirikishi.(t)Hiki ni kitenzi kinachounganisha vipashio vingine katika sentensi.Majukumu ya vitenzi vishirikishi ni kama yafuatayo:

 • Kuonyesha sifa fulani ya mtu
 • Kuonyesha umilikishi wa kitu chochote
 • Kuonyesha kazi au cheo anayofanya mtu
 • Kuonyesha mahali
 • Kuonyesha umoja wa vitu au watu
 • Kuonyesha msisitizo

Kuna aina mbili za vitenzi vishirikishi:Vitenzi vishirikishi vikamilifu.Hivi huchukua viambishi viwakilishi vya nafsi ,njeo na hali.Vitenzi vishirikishi vipungufu.Hivi havichukui viambishi viwakilishi vya nafsi,njeo na hali.